Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

77. SURAT AL-MURSALAAT

(Imeteremka Makka)

Lilio muhimu kabisa katika yaliyo kusanywa na Sura hii tukufu ni maneno yaliyo khusu kufufuliwa, na Kiyama, na dalili za kuthibitisha kuwa kitatokea, na kutishwa kwa waliyo yakataa hayo, na kurudishwa kutishwa huko kwa "Ole wao" mara kumi, na kuwatisha kwa unyonge na adhabu itayo wapata; na kubashiriwa wachamngu kwa starehe na neema watazo zikuta, na mwisho wake masaibu yatayo wapata makafiri wasio iamini Qur'ani.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole! *

2. Na zinazo vuma kwa kasi! *

3. Na zikaeneza maeneo yote! *

4. Na zinazo farikisha zikatawanya! *

5. Na zinazo peleka mawaidha! *

6. Kwa kuudhuru au kuonya, *

7. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa! *

8. Wakati nyota zitakapo futwa, *

9. Na mbingu zitakapo pasuliwa, *

10. Na milima itakapo peperushwa, *

11. Na Mitume watakapo wekewa wakati wao, *

12. Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo? *

13. Kwa siku ya kupambanua! *

14. Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini? *

15. Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha! *

16. Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia? *

17. Kisha tukawafuatilizia walio fuatia? *

18. Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu! *

19. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

20. Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa? *

21. Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti? *

22. Mpaka muda maalumu? *

23. Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria. *

24. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

25. Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya *

26. Walio hai na maiti? *

27. Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu? *

28. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

29. Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha! *

30. Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu! *

31. Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako. *

32. Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba! *

33. Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano! *

34. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

35. Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu, *

36. Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru. *

37. Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! *

38. Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia. *

39. Ikiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi! *

40. Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! *

41. Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem, *

42. Na matunda wanayo yapenda, *

43. Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. *

44. Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema. *

45. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

46. Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu! *

47. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

48. Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami. *

49. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! *

50. Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani