Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

73. SURAT AL-MUZZAMMIL

(Imeteremka Makka)

Katika Sura hii Mwenyezi Mungu amemuamrisha Mtume wake asimame sehemu kubwa ya usiku kwa ajili ya Sala na kusoma Qur'ani kwa utulivu. Akawa anasimama yeye na kikundi cha wale walio kuwa pamoja naye. Kisha Mwenyezi Mungu aliwapunguzia na akawaamrisha Sala, na Zaka, na Sadaka, na Kuomba maghfira.
Na miongoni ya hayo akamuamrisha avumilie kwa wayasemayo wale wanao kadhibisha, na awaachilie iwapate adhabu aliyo waahidi Mwenyezi Mungu; na Yeye amewaonya makafiri kwa mfano wa adhabu iliyo mshukia Firauni na walio kuwa pamoja naye, walipo muasi Mtume wa Mola wao Mlezi, na  akawakhofisha kwa vitisho vya Kiyama.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ewe uliye jifunika! *

2. Kesha usiku kucha, ila kidogo tu! *

3. Nusu yake, au ipunguze kidogo. *

4. Au izidishe - na soma Qur'ani kwa utaratibu na utungo. *

5. Hakika Sisi tutakuteremshia kauli nzito. *

6. Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na maneno yake yanatua zaidi. *

7. Kwani hakika mchana una shughuli nyingi. *

8. Na lidhukuru jina la Mola wako Mlezi, na ujitolee kwake kwa ukamilifu. *

9. Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipo kuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa wako. *

10. Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kwa vizuri. *

11. Na niache Mimi na hao wanao kanusha, walio neemeka; na wape muhula kidogo! *

12. Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unao waka kwa ukali kabisa! *

13. Na chakula kinacho kwama kooni, na adhabu inayo umiza. *

14. Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga! *

15. Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyo mtuma Mtume kwa Firauni. *

16. Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika mshiko wa mateso. *

17. Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo itawafanya watoto wadogo waote mvi? *

18. Hapo mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa. *

19. Kwa hakika hili ni kumbusho. Mwenye kutaka atashika njia ya kwendea kwa Mola wake Mlezi. *

20. Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhaalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo, na mshike Sala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. *   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani