Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

56. SURAT AL-WAAQIA'H

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanzia kwa kusimulia Tukio la Kiyama, na matokeo yatayo ambatana na Tukio hilo. Kisha ikasimulia kuwa viumbe Siku hiyo watakuwa namna tatu. Ikafuatia hayo kwa kufafanua kwa kutosha walio andaliwa kila fungu katika hao, ikiwa ni neema zinazo wafikiana na cheo chao, au ni adhabu inayo nasibiana na ukafiri wao na uasi wao.
Kisha Aya zikaweka wazi baada ya hayo yanayo onekana katika neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na athari za uweza wake katika viumbe, na makulima, na maji, na moto; na yanayo hitajika kutokana na athari hizi kumsabihi Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtakasa.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Litakapo tukia hilo Tukio *

2. Hapana cha kukanusha kutukia kwake. *

3. Literemshalo linyanyualo, *

4. Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso, *

5. Na milima itapo sagwasagwa, *

6. Iwe mavumbi yanayo peperushwa, *

7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu:- *

8. Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani? *

9. Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni? *

10. Na wa mbele watakuwa mbele. *

11. Hao ndio watakao karibishwa *

12. Katika Bustani zenye neema. *

13. Fungu kubwa katika wa mwanzo, *

14. Na wachache katika wa mwisho. *

15. Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa. *

16. Wakiviegemea wakielekeana. *

17. Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele, *

18. Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi. *

19. Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa. *

20. Na matunda wayapendayo, *

21. Na nyama za ndege kama wanavyo tamani. *

22. Na Mahurulaini, *

23. Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa. *

24. Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda. *

25. Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, *

26. Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama. *

27. Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani? *

28. Katika mikunazi isiyo na miba, 29. Na migomba iliyo pangiliwa, *

30. Na kivuli kilicho tanda, 31. Na maji yanayo miminika, *

32. Na matunda mengi, *

33. Hayatindikii wala hayakatazwi, *

34. Na matandiko yaliyo nyanyuliwa. *

35. Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, *

36. Na tutawafanya vijana, *

37. Wanapendana na waume zao, hirimu moja. *

38. Kwa ajili ya watu wa kuliani. *

39. Fungu kubwa katika wa mwanzo, *

40. Na fungu kubwa katika wa mwisho. 3 *

41. Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni? *

42. Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka, *

43. Na kivuli cha moshi mweusi, *

44. Si cha kuburudisha wala kustarehesha. *

45. Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa. *

46. Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa, 47. Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa? *

48. Au baba zetu wa zamani? *

49. Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho *

50. Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu. *

51. Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha, *

52. Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu. *

53. Na kwa mti huo mtajaza matumbo. *

54. Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka. *

55. Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu. *

56. Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo. *

57. Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? *

58. Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? *

59. Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji? *

60. Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi 61. Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua. *

62. Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki? *

63. Je! Mnaona makulima mnayo yapanda? *

64. Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha? *

65. Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu, *

66. Mkisema: Hakika sisi tumegharimika; *

67. Bali sisi tumenyimwa. *

68. Je! Mnayaona maji mnayo yanywa? *

69. Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? *

70. Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru? *

71. Je! Mnauona moto mnao uwasha? *

72. Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji? *

73. Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani. *

74. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu. *

75. Basi naapa kwa maanguko ya nyota, *

76. Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua! *

77. Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu, *

78. Katika Kitabu kilicho hifadhiwa. *

79. Hapana akigusaye ila walio takaswa. *

80. Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. *

81. Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza? *

82. Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha? *

83. Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, *

84. Na nyinyi wakati huo mnatazama! *

85. Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. *

86. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, *

87. Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? *

88. Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, *

89. Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. *

90. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, *

91. Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia. *

92. Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, *

93. Basi karamu yake ni maji yanayo chemka, *

94. Na kutiwa Motoni. *

95. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. *

96. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa. *   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani