Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

44. SURAT ADDUKHAN

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanza kwa kusimulia khabari za Qur'ani, ya kwamba imeteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika usiku wa Lailatul Qadri ulio barikiwa, kwa ajili ya kuonya na Tawhid, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Na kwamba hii Qur'ani ni Haki, Kweli tupu. Hali kadhaalika Sura imesimulia khabari za kufufuliwa, na kwamba hayo hayana shaka ndani yake, na imezibisha hoja za wanao yakanya hayo, na ikawarudi washirikina. Ikalinganisha baina ya washirikina wa Makka na wenzao walio watangulia, nao ni kaumu ya Firauni. Ikaeleza mapatilizo ya Mwenyezi Mungu yaliyo washukia hao. Tena ikatilia mkazo kwamba Siku ya Kiyama ndiyo siku iliyo pangwa ya kuutenga ukafiri na upotovu wote. Na ikasimulia malipo ya wakosefu kwa siku hiyo na malipo ya walio ongoka. Na ikamalizika kama ilivyo anzia kwa mazungumzo juu ya Qur'ani, na kwa kuwaonya wanao kadhibisha Ujumbe wa Mtume s.a.w. kuwa nao wangojee balaa na masaibu yatakayo washukia.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim *

2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha, *

3. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. *

4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima, *

5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. *

6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. *

7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini. *

8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo. *

9. Lakini wao wanacheza katika shaka. *

10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri, *

11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu! *

12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. *

13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha. *

14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu. *

15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile! *

16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa. *

17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu. *

18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. *

19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi. *

20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. *

21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami. *

22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu. *

23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. *

24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa. *

25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! *

26. Na mimea na vyeo vitukufu! *

27. Na neema walizo kuwa wakijistareheshea! *

28. Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe. *

29. La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula. *

30. Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha, *

31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka. *

32. Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe. *

33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi. *

34. Hakika hawa wanasema: *

35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi. *

36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. *

37. Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu. *

38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. *

39. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui. *

40. Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote. *

41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa. *

42. Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. *

43. Hakika Mti wa Zaqqum, *

44. Ni chakula cha mwenye dhambi. *

45. Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni *

46. Kama kutokota kwa maji ya moto. *

47. (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu! *

48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka. *

49. Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! *

50. Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka. *

51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani, *

52. Katika mabustani na chemchem, *

53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, *

54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini. *

55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani. *

56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu, *

57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa. *

58. Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka. *

59. Ngoja tu, na wao wangoje pia. *   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani