Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

42. SURAT ASH-SHUURA

(Imeteremka Makka)

Hii ni Sura ya Makka, na idadi ya Aya zake ni 53, na imeitwa Ash-shuura, yaani "Kushauriana" kwa sababu inavyo waongoza Waumini waendeshe mambo ya jamii zao kwa kushauriana, ili ipatikane Haki, na uthibiti uadilifu. Na Sura hii imekusanya mambo mengi ya Dini na hoja za itikadi.
Imefungua Sura kwa kuisifu Qur'ani yenyewe kwa kuwa ni Wahyi (Ufunuo) ulio toka kwa Mwenyezi Mungu, ikayarudisha matusi ya makafiri, na ikashughulikia kumpoza Mtume s.a.w., na tena baada ya hayo ikaingilia kuthibitisha uweza wa Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani na ukatukuka utawala wake, na ikaeleza kukanya kwa baadhi ya watu juu ya kuwa hoja zake ziwazi zinazo onyesha kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kubainisha khitilafu zao katika kufahamu Haki. Na baada yake Sura hii ikatilia mkazo uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya kila kitu. Kisha ikathibitisha kuwa msingi wa sharia ni mmoja, na ikaashiria kuwa wapo wanao kufuru juu ya hivyo. Hali kadhaalika imeashiria kuwa Vitabu vyote vya mbinguni vinaongoza kwendea Haki. Na Sura imelaani shirki ya washirikina, na kukhitalifiana kwao katika Haki kwa udhalimu tu. Na pia imelaani kule kuhimiza kwao, wanao kadhibisha,  kuhimiza Kiyama kwa maskhara. Na ikatoa uwongozi kwa wafuasi wake wawalinganie watu kwenye Dini, kama ilivyo eleza ubora wa upole wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na Sura hii imehadharisha kuzama katika kuiwania dunia tu peke yake. Na ikabainisha uovu wa hali ya makafiri na wema wa hali ya Waumini katika Akhera. Na Sura ikawalaumu wale walio mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kwa kumwambia kaizua Qur'ani, hali wao wameshindwa hata kuleta Sura moja tu mfano wake. Kisha ikatangaza kuwa Mwenyezi Mungu ameikubali toba ya Waumini, na ikatangaza hikima ya kuzigawa riziki kwa watu kwa mpango wa hikima. Hawakuwa wote matajiri, kwa kuchelea wasipande jeuri, wala wasiwe wote mafakiri wakateketea. Bali amewakunjulia baadhi na amewadhikisha wengine.
Na akadhihirisha baraka za mvua, na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa jambo hili, na kwamba masaibu ya dunia ni kwa sababu ya maasi. Kisha Subhanahu akakariri kwa njia nyingine hali za Waumini na wanao kadhibisha huko Akhera, na madhila yatayo wapata wanao kadhibisha. Na akataka wafanye haraka kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kabla uhai haujakata fursa ya kutenda. Kadhaalika Sura imeshughulika kumpoza  Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. na kubainisha uweza wake Subhanahu kumtunukia amtakaye watoto wa kike, na wa kiume mwenginewe, na mchanganyiko kwa wa tatu, na kumnyima kabisa wa nne. Kisha Sura ikataja njia za Mwenyezi Mungu kusema na Manabii wake, na ikakhitimisha kwa kubainisha Njia ya Haki Iliyo Nyooka ambayo inayo pasa kuifuata.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim *

2. A'yn Sin Qaf *

3. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima anavyo kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako. *

4. Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi. Na Yeye ndiye Mtukufu, Mkuu. *

5. Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. *

6. Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao. *

7. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni. *

8. Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi. *

9. Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu. *

10. Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na kwake Yeye narejea. *

11. Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. *

12. Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu. *

13. Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye. *

14. Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo wahangaisha. *

15. Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake. *

16. Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali. *

17. Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa Haki, na Mizani. Na nini kitakacho kujuulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama ipo karibu? *

18. Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanao amini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanao bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa. *

19. Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku ampendaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mtukufu. *

20. Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika mavuno yake, na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini katika Akhera hana fungu. *

21. Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo itolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua basi wangeli katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu. *

22. Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa. *

23. Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika kujikurubisha. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani. *

24. Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliomo vifuani. *

25. Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa, na anayajua mnayo yatenda. *

26. Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu. *

27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki waja wake, basi bila ya shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona. *

28. Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kwisha kata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa. *

29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama alio waeneza. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo. *

30. Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi. *

31. Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu. *

32. Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini kama vilima. *

33. Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru. *

34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo yatenda hao watu. Naye husamehe mengi. *

35. Na ili wajue wanao jadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia. *

36. Basi vyote mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio amini, na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi, *

37. Na wanayo yaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapo kasirika wao husamehe, *

38. Na wanao mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulicho waruzuku wakawa wanatoa, *

39. Na ambao wanapo fanyiwa jeuri hujitetea. *

40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu. *

41. Na wanao jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu. *

42. Bali lawama ipo kwa wale wanao wadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika nchi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu. *

43. Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. *

44. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana mlinzi baada yake. Na utawaona wenye kudhulumu watakapo iona adhabu wanasema: Je! Ipo njia ya kurudi? *

45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika wapatao khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima. *

46. Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote. *

47. Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo epukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukingia. *

48. Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyo yatanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru. *

49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume, *

50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza. *

51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima. *

52. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. *

53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu. *   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani