Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

1. SURAT AL-FAATIH'A

(Imeteremka Makka)

Sura hii iliteremka Makka kabla ya Hijra, kuhamia Mtume s.a.w. Madina. Imeitwa Al-Faatih'a, yaani Kifungulio kwa kuwa ndiyo sura ya mwanzo katika mpango wa Msahafu Mtukufu, nayo ni sura ya mwanzo iliyo teremka kwa utimilivu wake. Na sura hii inakusanya jumla ya yaliyomo katika Qur'ani na kama kwamba huu ni mukhtasari wake, na baadaye yatakuja mambo kwa tafsili, babu-babu.
Na makusudio ya Qur'ani ni: Kubainisha Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu; na kubainisha ahadi na bishara kwa Muumini mtenda mema; na kubainisha ahadi na onyo kwa kafiri na mtenda maovu; na kubainisha ibada; na kubainisha njia ya kufanikiwa duniani na Akhera; na hadithi za walio mt'ii Mwenyezi Mungu wakafuzu, na hadithi za walio muasi wakaangamia.
Sura  Al-Faatih'a inakusanya kwa ufupi na kwa kuashiria makusudio haya, na kwa hivyo ndio ikaitwa pia "Ummul Kitaab" yaani "Msingi wa Kitabu".
 

1. KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.1

2. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote;2

3. Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu;3

4. Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo. 4

5. Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada.5

6. Tuongoe njia iliyo nyooka,6

7. Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea. 7


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani