Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanyia tenge. Kimetengenezwa vizuri, ili kiwaonye watu adhabu kali itokayo kwake, na kiwape khabari njema wenye kuamini, ambao wanafanya vitendo vizuri, kwamba watapata malipo mema, wakae humo milele. Ni Kitabu ambacho Aya zake zimelindwa, kisha zimepambanuliwa kutoka kwa Mwenye hekima, Mwenye ujuzi. Haitakifikia batili mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa. Hicho ni Kitabu kisicho shaka ndani yake, ni Muongozo kwa wamchao. Malaika Jibril (a.s) ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwaimarisha wale walioamini, na kuwa Muongozo na khabari njema kwa wenye kumnyenyekea. Si maneno yaliyozushwa, bali ni hakikisho la yale yaliyokuwa kabla yake, na ni maelezo ya kila kitu, na ni Muongozo na Rehema kwa watu wenye kuamini.
Rehema na Amani zimshukie Mtume Muhammad s.a.w aliyemleta kwa uongofu na dini ya haki ili ishinde dini zote ijapokuwa watachukia washirikina.
Na ziwashukie Rehema na Amani Aali zake (watu wa nyumba ya Mtume) waliosafishwa na kutakaswa sana. Ambao waliomwamini Mtume na wakamtukuza na wakamsaidia na wakaifuata Nuru iliyoteremshwa parnoja naye, hao ndio wenye kufuzu. Mwenyezi Mungu amekuwa radhi nao, na wao wamekuwa radhi naye, hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu, sikilizeni! hakika kundi la Mwenyeezi Mungu ndilo linalofuzu.
Na laana ya kudumu iwashukie maadui zao, ambao siku hiyo watatoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia kwenye mradi (wao). Macho yao yatainama, unyonge utawafunika, hiyo ndiyo siku waliyokuwa wakiahidiwa. Siku ambayo hautawafaa madhalimu udhuru wao, na watapata laana, mahala pao patakuwa pabaya.
Kwa Mukhtasari sana, tafsiri hii imeandikwa ikiwa ina mikondo mitatu:
Tarekh, Siasa na Fiq'h. Hii ni kuonyesha hali ya matukio ya kitarekh, siasa na elimu (fiq'h) kwa kuzingatia utambulisho wake kama ifuatavyo:
Tarekh, ni: Kufahamisha wakati. Yaani, watu walioishi katika zama hizo:
Waislamu, mayahudi, wakristo, makafiri wengine, wakafanya waliyoyafanya. mema au maovu, hao ndio walengwa.
Siasa, ni: Itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi wake, utamaduni na mwendo mzima wa maisha ya jamii hiyo.
Ukisoma Qur'an na tarekh ya Kiislamu utakuta kwamba: Uislaamu ni dini na dola, kwa hiyo, siasa imekuwa na fungamano kubwa na dini.
Tunasema kwamba:
Mwanasiasa, kazi yake ni kuisaidia serikali katika kutunga sheria na uongozi mzuri, na kuwasaidia raia katika kufahamiana na serikali. Na wala siyo
kuwasaidia madhalimu katika kuudhuru umma, kwa sababu, katika "Uislaamu, hakuna baya ambalo huwa ni zuri kwa ajili ya siasa, wala hakuna haramu ambayo huwa halali katika siasa. Kwa hiyo: Uongo, fitna, rushwa, na mfano wa haya yanayofanywa na baadhi ya wanasiasa khasa katika siku za kampeni, ni haramu.
Fiq'h, tamko hili pamoja na minyumbuko yake, limekaririwa katika Qur'an mara ishirini, ambalo linafidisha elimu/ kufahamu. Kwa kuwa Our'an inazungumza lugha ya Kiarabu, italazimu kuzihusisha elimu zinazoizunguka lugha hii, kwa ajili ya kupata majibu muafaka yanayohusu maana na matumizi ya maneno yaliyotumika katika Lugha ya Kiarabu.
Basi, ikiwa Mwenyeezi Mungu ameniwafikisha katika kazi hii ya tafsiri,
alhamdulillah, hilo ndilo nitarajialo na kulitamania, na bila shaka hiyo ni katika fadhila ya Mwenyeezi Mungu peke yake. Na kama si hivyo, basi a'saa,
kwa mwanzo huu nitakuwa nimepasua njia mbele ya ndugu zangu
-twalabatul Ilmi" na katika hayo washindanie wenye kushindana.
Kuliko kukejeli, kukatisha tamaa, na kudharau kazi nzima, ambayo imegharimu gharama kubwa sana. Kazi hii imechukua muda mrefu, imechukua taklifu kubwa kwa kufuatilia Maswadir mbalimbali kwa kina
Kirefu. Lakini, pamoja na tahadhari kubwa hiyo, bado mambo mawili ya
msingi yapo mbele yangu ninayatambua:
(a) Upungufu wa kibinadamu nilio nao.
(b) Uchache wa maarifa nilio nao.
Kwa hiyo, natarajia kwa kila atakayeona mapungufu haya yameathiri
Tarjama au tafsiri, tafadhali atuzindue kwa kuwasiliana nasi, ili katika chapa inayofuata ushauri wake uzingatiwe inshaallah.
Ee Mola! tuonyeshe haki, tuifahamu kuwa ni haki, uturuzuku kuifuata. Na
tuonyeshe batili, tuifahamu kuwa ni batili, uturuzuku kuiepuka. Waswallallahu a’laa Muhammadin wa Aalihi At-twayyibiina At-twahiriin.
ALI JUMAA MAYUNGA 1/11/2001