KUBADILI JINA

Tarehe 9/6/2000 nilipotangaza mabadiliko ya jina, kuwa: Kuanzia sasa naitwa "ALI" badala ya jina la awali "OMAR" Kwa hiyo, nitaitwa "Ali Jumaa Mayunga" wakati wote, popote, na kwa vyovyote. Mabadiliko haya jamii iliyapokea kwa hisia tofauti, hasa hisia mbili kuu zilitawala baina ya jamii hiyo: Itikadi ya kimadhhabi, na itikadi ya kishetani:

(a) Itikadi ya kimadhhabi: Wenye hisia hii waliamini kuwa, nimebadilisha jina la "Omar" kuepuka kufanana na sahaba wa Mtume s.a.w Omar bin Khattab Al-Adawy. Kwanini? Wanasema wenye hisia hii kuwa: Kwa sababu Mashia Ithna ashari wanamuona ni muovu.

(b) Itikadi ya kishetani: Wenye hisia hii waliamini kuwa: nimebadilisha jina la "Omar" kwa sababu ya ushauri wa waganga. Kwa kuwa nilipatwa na tukio kubwa la kuunguliwa nyumba yangu, vikateketea ndani yake vitu vyote isipokuwa vitabu vya dini. Hilo, wenye hisia hii wanaona: Lazima yalipita mazingara, na wachawi wakanishauri kuwajina la "OMAR" sasa halinifai... Hizi ndizo hisia kuu zilizotawala katika jamii. Kabla sijataja msimamo wangu, nataka nionyeshe hapa matukio mawili ya kitarekh. La'alla yatawasaidia wenye hisia hizo kufahamu Darsa zima hii ya mtu kubadili jina.

(a) Abdur Rahman bin Abibakar At-Taymi, alisilimu kabla ya Fat-hu Makka, ambaye akiitwa katikazama za jaahiliya: Abdul kaaba, au Abdul uzza. Kisha Mtukufu Mtume s.a.w akamwita: Abdur Rahman baada ya kusilimu.

Taz: Tahdhibut Tahdhib J.6 Uk. 146-147

(b) Abdur Rahman bin Zaid bin Khattab Al-Adawy, aliyezaliwa katika zama za Mtume s.a.w akaitwa: Muhammad. Kisha Omar bin Khattab akambadilisha jina akamwita: Abdur Rahman.

Taz: Tahdhibut Tahdhib J.6 Uk. 179

Kwa hiyo, natija ya Darsa hii inasema: Kubadili jina ni Sunnatun Fiiliyyatun. Ama kuhusu mkosi wa jina la Omar au Umar, kwa sababu zozote walizonazo wenye hisia hii, majibu yake ni haya yafuatayo."

Ali bin Abi Talib (a.s) ni Wasii na Khalifa wa Mtume Muhammad s.a.w baada yake. Imam Ali (a.s) ameoa na amezaa, jumla ya watoto wake wa kiume na wa kike hawapungui ishirini na sita, ambao ni:Hasan, Husein, Zaynabul Kubra, Zaynabus Sughra ambaye kun-ya yake ni Ummul Kulthum, (Mama yao ni Bibi Fatima bint Muhammad s.a.w) Muhammad ambaye kun-ya yake ni Abul Qasim, (Mama yake ni Khawla bint Jaafar bin Qays Alhanafiya) Omar na Ruqayya ambao ni mapacha, (mama yao ni Ummu Habiba bint Rabia) Abas, Jaafar, Uthman, Abdallah, (Mama yao ni Ummul Baniina bint Hizami bin Khalid bin Daarimi) Muhammadul Asghar ambaye kun-ya yake ni Abubakar, Ubaydullah, (Mama yao ni Layla bint Masuud Addarimiyya) Yahya, Awn, (Mama yao ni Asmaa bint Umays Al-khath-amiyya) Ummul Hasan, Ramla, (Mama yao ni Ummu Masuud bin Ur-wa bin Masuud Ath-Thaqafy) Nafisa, Zaynabus Sughra, Ruqayyatus Sughra, Ummu Haani, Ummul Kirami, Jamana ambaye kun-ya yake ni Ummu Jaafar, Umama, Ummu Salama, Maymuna, Khadija, Fatima, (a.s.).

Taz: Kashful ghumma J.2  Uk. 67

Zingatia: Miongoni mwa watoto wa Imam kuna: Abubakar, Omar, Uthman.

Sasa, baada ya kuonyesha matukio ya kitarekh hapa, msimamo wangu wa kubadili jina uko wazi mbele ya msomaji. Bila shaka Darsa hii imeonyesha wazi kuwa: Kubadili jina ni Sunnatun Fiiliyyatun.