DIBAJI

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.

Kila sifa njema ni zake Mwenyeezi Mungu Bwana wa Viumbe wote, Muumba Mbingu na Ardhi.

Ni fadhila zisizo kifani, ambazo yeye Muumba wa yote amezijaalia zinifikie mja kama mimi. Alhamdu lillah.

Fahari ya kazi hii ni ya kipekee, ambayo ni adimu kupatikana, hali ambayo haikanushiki. Nilipojiwa na Sheikh wangu Ali Jumaa Mayunga na akanieleza juu ya jambo la kusoma Mswada wa Tafsiri yake hii, Wallahi, niliduwaa, manusura niseme vingine. Lakini niliona kila lililo gumu hufanywa ndipo likawa gumu au likapunguzwa ugumu. Kwa hali hiyo nilipiga moyo konde nikasema: Naam nitayari.

Alhamdu Lillah, nimeipokea na baada ya kuisoma tafsiri hii ambayo Aalim wetu mfasiri Ali Jumaa Mayunga amejionyesha kwa vitendo kwamba, alikusudia kutupa hidaya ambayo niya thamani kubwa mno. Pia amejieleza kwa uwazi kwamba anacho anachokifahamu kile ambacho Mwenyezi Mungu amemjaalia.

Tafsiri hii imepewa sifa nyingi kielimu, lakini nitataja tatu tu, nazo ni: Ya kwanza, utumiaji wa maneno ambayo ni ya muafaka kwa kila atakae yasoma kwa ufasihi na wepesi wa kufahamika na kwa ufupi zaidi. Pili, ameepuka sana utumiaji wa lugha za istiara ili kusiwe na haja ya kugonga vichwa kutafuta undani wa maana sanifu. Na sifa ya tatu, Aalim wetu amejitahidi kwa nguvu zake zote awe ndani ya mipaka ya haki ya yale ambayo ndiyo Mwenyeezi Mungu alikusudia kutueleza, yaani hakutia lolote ambalo halimo ndani ya Aya anazoziandika. Huu ni mchango mkubwa mno ambao tafsiri hii itautoa kwa kila atakeisoma ataupokea. Yaani hamna neno nje ya Aya za Mwenyeezi Mungu.

Tafsiri ya Qur'an hii, ni tafsiri sahihi na ni tafsiri isiyo hofu yoyote, ni lulu ya asili. Tumshukuru Mola kutujaalia Aalim wetu Sheikh Ali Jumaa Mayunga kutukumbuka sisi wasomao. Sisemi imekamilika, lakini kwa kiasi cha yale niyafahamuyo mimi, nasema yana dalili zote za kuwa ni kazi iliyo tuwama na ukamilifu.

Zaidi ya yote, tafsiri nyingi tulizozizowea isipokuwa chache tu, huwa hazina marejeo, lakini humo Sheikh kwa hakika na kwa Lillahi, amekusudia kuwapa Waislam wenziwe mengi kati ya yale wasiyoyaelewa vizuri kama si kutokuyafahamu kamwe. Humu yaelekea Sheikh amechukua taabu kubwa ingawa kwake sitaabu, lakini kwa nia Swalih ametumia vitabu vingi sana tena vilivyo maarufu na bora, akavitumia kuwa kama mapitio na marejeo ya usahihi wa hayo aliyoyatoa katika ufafanuzi wa Aya nyingi sana, na kuonyesha uzuri wa matokeo ya haki, kweli na yaliyokuwa dhahiri katika visa na asili ya uletwaji wa Aya kwa Bwana Mtume (s.a.w).

Itakuwa fahari kubwa kwetu na kwa mtu yeyote kama atajitahidi mpaka ajaaliwe kukipata kitabu au Tafsiri hii ya Qur'an ya Sheikh Ali Jumaa Mayunga. Humo mna Kiswahili cha aina bora kabisa alichokitumia, pia ukweli wa maelezo yake na uzuri wa matokeo ya shughuli za kiroho. Tafsiri hii ni nzuri kwa sababu kama zilizoelezwa huko nyuma.

• Lugha safi,

• Lugha laini,

• Lugha yenye kuwekwa wastani.

• Na mwisho, uelezaji wa kiualimu.

Tafadhali msomaji wa tafsiri hii, usiwe na hofu wakati utakapokuwa unaisoma, utakuwa unaisoma Qur'an yako kwa lugha yako, wala hamna matatizo au upotofu wa aina yoyote.

Namshukuru Mwenyeeezi Mungu kunipa pumzi za kuniwezesha kusoma na kuweza kuandika haya ninayo yaandika.

Swala na Salamu zimwendee Bwana wa Mabwana Mtume Muhammad (s.a.w). Inshallah tuwe wasornaji wema na tumuombee Msafiri wetu Mwenyezi Mungu ampe uwezo, afya na nia ya kutufanyia kama haya tena.

KATIBU MTENDAJI MKUU

 USANIFU KISWAHILI TANZANIA

UKUTA

21-9-1999