98 SUURATUL BAYYINA

Sura hii imeteremshwa Madina na ina Aya 8

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Wale waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina, hawakuwa wenye kuachana na waliyo nayo mpaka iwafikie hoja.

2. Ni Mtume aliyetoka kwa Mwenyeezi Mungu anayewasomea kurasa zilizotakaswa.

3. Ndani yake zimo Sharia madhubuti.

4. Wala hawakufarikiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwafikia hoja.

5. Wala hawakuamrishwa ila kumwabudu Mwenyeezi Mungu kwa kumtakasia yeye dini, hali wameshikamana na haki, na wanasimamisha swala na kutoa zaka, na hiyo ndiyo dini madhubuti.

6. Hakika wale waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina wamo katika Moto wa Jahannam watakaa milele humo, hao ndio waovu wa viumbe.

7. Hakika wale walioamini na kutenda mema, hao ndio werna wa viumbe.[1]

8. Malipo yao kwa Mola wao ni Mabustani ya milele yanayopita mito chini yake, watakaa humo milele Mwenyeezi Mungu amewaridhia nao wamemridhia (malipo) hayo ni kwa yule anayemuogopa Mola wake.


[1] Aya 7

 WAFUASI WA IMAM ALI WATAFUZU

Iliposemwa: "hakika wale walioamini na kutenda mema, hao ndio wema wa viumbe."

Imepokewa kwa Jaabir bin Abdillah anasema: Tulikuwa tumeketi na Mtume (s.a.w.w) mara akatokea Ali bin Abi Talib, Mtume (s.a.w.w) akasema: "Naapa kwa ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, hakika huyu (Ali) na Shia (wafuasi) wake lazima ni wenye kufaulu siku ya Kiyama." Pale pale Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya hii. 98:7.

Taz: Fat’hul Bayani fyi Maqasidil Qur'an J.5  Uk. 337

Tafsirut Tabari J.30 Uk. 171

Addurrul Manthur  J.6  Uk. 643

 Alburhan fyitafsiril Qur'an   J.4  Uk. 491

Almizan fyitafsiril Qur'an     J.20 Uk. 482

Tafsirus Saafi   J.5  Uk. 355

 Fafhul Qadiir   J.5  Uk. 678

Ruuhul Maany  J.30 Uk. 370