Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Ole wao wenye kupunguza (vipimo).
2. Ambao wanapojipimia kwa watu hupokea kamili.
3. Na wanapowapimia kwa kipimo au kwa mizani wao hupunguza.
4. Je hawafikiri hao kuwa watafufuliwa?
5. Katika siku kubwa.
6. Siku watakaposimama watu mbele ya Mola wa walimwengu.
7. Sivyo, hakika daftari ya waovu imo gerezani.
8. Na nini kitakujulisha gereza ni nini?
9. Ni hukumu iliyoandikwa.
10. Ole wao siku hiyo kwa wenye kukadhibisha.
11. Ambao wanaikadhibisha siku ya hukumu.
12. Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka mwenye dhambi.
13. Anaposomewa Aya zetu, husema: Ni visa vya watu wa zamani.
14. Sivyo, bali yametia kutu juu ya nyoyo zao (waovu) waliyokuwa wakiyachuma.
15. Sivyo hakika kwa Mola wao, siku hiyo watakingiwa pazia.
16. Kisha wao hasa wataingia katika Moto.
17. Ndipo wataambiwa: Haya ndiyo mliyokuwa mkiyakadhibisha.
18. Sivyo hakika maandishi ya watu wema yamo katika mahala patukufu.
19. Na nini kitakujulisha mahala patukufu ni nini?
20. Ni hukumu iliyoandikwa.
21. Wataiona walio karibu (na Mwenyeezi Mungu).
22. Hakika watu wema watakuwa katika neema.
23. Wakiwa juu ya viti vya fahari wakitazamana.
24. Utaona katika nyuso zao mng'ao wa neema.
25. Watanyweshwa kinywaji halisi kilichofunikwa.
26. Mwisho wake (ni harufu ya) miski, na katika hayo, basi washindane wenye kushindana.
27. Na cha kuchanganyia ni Tasnim.
28. Ni chemchem watainywa (watu) walio karibu (na Mwenyeezi Mungu).
29. Kwa hakika wale waliokosa walikuwa wakiwacheka Waumini.
30. Na walipopita karibu yao walikonyezana.
31. Na waliporudi kwa watu wao walirudi wakishangilia.
32. Na walipowaona walisema: Hakika hao ndio hasa waliopotea.
33. Na hawakupelekwa kuwa walinzi juu yao.
34. Basi leo, walioamini watawacheka makafiri.
35. Wakiwa juu ya viti vya fahari wakitazama.
36. Je, makafiri wamelipwa yale waliyokuwa wakiyafanya?