Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Sema: Imefunuliwa kwangu kuwa, kundi moja la majinni lilisikia (Qur'an) likasema: Hakika tumesikia Qur'an ya ajabu.
2. Inaongoza kwenye uongofu, kwa hiyo tumeamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.
3. Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu umetukuka, hakujifanyia mke wala mwana.
4. Na kwa hakika mpumbavu miongoni mwetu alikuwa akisema maneno ya upuuzi juu ya Mwenyeezi Mungu.
5. Nasi tulikuwa tukidhani kuwa watu na majinni hawatasema uongo juu ya Mwenyeezi Mungu.
6. Na hakika kulikuwa na watu miongoni mwa wanadamu wakijikinga kwa watu miongoni mwa majinni, hivyo wakawazidishia kiburi.
7. Na kwa hakika wao walidhani kama mlivyodhani nyinyi kuwa, Mwenyeezi Mungu hatamtuma yeyote.
8. Nasi tuliigusa mbingu tukaiona imejaa walinzi wenye nguvu na nyota zing'aazo.
9. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza, lakini anayetaka kusikiliza sasa atakuta kimondo kikimvizia.
10. Nasi hatujui kama shari inatakiwa kwa wale wanaokaa ardhini au Mola wao anawatakia muongozo?
11. Na hakika katika sisi wamo wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tulikuwa njia mbalimbali.
12. Nasi tulijua kuwa hatuwezi kumshinda Mwenyeezi Mungu katika nchi wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.
13. Nasi tulipousikia muongozo, tukauamini, basi anayemwamini Mola wake hataogopa khasara wala ubaya.
14. Nasi wamo miognoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu waovu lakini aliyesilimu basi hao ndio waliotafuta uongofu.
15. Ama wale waovu, basi wamekuwa kuni za Jahannam.[1]
16. Na kama wangelishika kwa imara njia (iliyonyooka) tungeliwanywesha maji kwa wingi.
17. Ili tuwajaribu kwa hayo, na anayepuuza kumkumbuka Mola wake atamsukuma kwenye adhabu ngumu.
18. Na kwa hakika Misikiti yote ni ya Mwenyeezi Mungu basi msimuombe mwingine pamoja na Mwenyeezi Mungu.
19. Na kwa hakika mja wa Mwenyeezi Mungu aliposimama kumuomba (Mola wake) walikuwa karibu kumuangukia.
20. Sema: Ninamuomba Mola wangu tu wala simshirikishi na yeyote.
21. Sema kwa hakika mimi similiki kwa ajili ya dhara juu yenu wala kheri.
22. Sema bila shaka hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyeezi Mungu, wala sitapata makao ya salama ila kwake yeye tu.
23. Ila kwa kufikisha (ujumbe) utokao kwa Mwenyeezi Mungu na amri zake, na atakayemuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, basi bila shaka atapata Moto wa Jahannam watakaa humo milele.
24. Hata watakapoyaona wanayoahidiwa ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu na mwenye idadi ndogo.
25. Sema: Sijui kama yako karibu mliyoahidiwa na Mola wangu atayawekea muda mrefu.
26. Ni mjuzi wa siri wala hamdhihirishii yeyote siri yake.
27. Isipokuwa Mtume aliye mridhia, basi hakika yeye humuwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.
28. Ili ajue (Mtume) kuwa: Wamekwisha fikisha ujumbe wa Mola wao, na anayajua (Mwenyeezi Mungu) yote waliyo nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.
[1] Aya 15
MTUME AMUAGIZA ALI KUWAPIGA WAOVU
Amesema Mtume s.a.w kumwambia Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa: "Utapigana na Naakithiin na Qaasitiin na Maariqiin."
Taz: Tafsirul Basair: J.49 Uk. 446
Mustadrak alaa Sahihayn: J.3 Uk.150
Muntakhbu kanzu U'mmal: .1.5 Uk. 499
Tarekh Bughdad: J.8 Uk. 340
NAAKITHUUN, ni vile vita vya Jamal katika mwaka wa thelathini na sita Hijria, Imam Ali alipigana na majeshi yaliyoongozwa na Mwana Aisha (mkewe Mtume) watu kiasi elfu kumi waliuliwa. Mapigano hayo yalifanyika katika ardhi ya Basra.
Kwa hiyo, Naakithuun ni Mwana Aisha, Twaiha, na Zubeir pamoja na wafuasi wao. Ndio walioamuriwa kupigwa, kwa sababu ni waovu.
QAASITUUN, ni vile vita vya Siffin. Baadaye mwishoni mwa mwaka wa thelathini na sita Hijria, Imam Ali (a.s) alipigana na majeshi yaliyoongozwa na Muawiya bin Abi Sufyan. Mapigano haya yalifanyika katika eneo la Siffin.
MAARIQUUN, ni vile vita vya Nahrawan. Katika mwaka wa thelathini na saba Hijria, Imam Ali (a.s) alipigana tena na majeshi ya Muawiya katika eneo la Nahrawan. Siku moja, Mtume s.a.w alimshika mkono Imam Ali bin Abi Talib (a.s) akasema: "Huyu ni Kiongozi wa watu wema, na atawapiga waovu, atalipwa (mema) atakayemsaidia, ataangamizwa atakayemwacha."
Taz: Ihqaqul haqqi: J.4 Uk. 234-239
Lisanul Mizaan: J.l Uk. 197
Tarekh Bughdad: J.2 Uk. 377
MUAWIYA NA AMMAR
Katika vita vya Siffin, alipouliwa Ammar bin Yaasir na majeshi ya Muawiya, Amru bin A's alimkumbusha Muawiya kauli ya Mtume s.a.w afiyosema juu ya Ammar: "Ammar atauliwa na kundi potovu." Muawiya akamjibu: Wewe hujui, sisi hatukumuua Ammar, aliyemuua ni Ali aliyemleta hapa akakutana na panga zetu.
Taz: Tafsirul Basair: J.49 Uk. 489
Assunanul Kubra: J.8 Uk- 189
Imam Ali (a.s) alipoambiwa hayo, akajibu: Ikiwa ni hivyo, basi Hamza ameuliwa na Mtume s.a.w. kwa sababu, yeye ndiye aliyemtoa kwake akampeleka eneo la Uhud akakutana na panga za Makuraish wakamuua! Muawiya akakosa la kujibu.
QUR'AN YAFANYWA CHAMBO
Katika vita vilivyopiganwa Nahrawan baina ya Imam Ali (a.s) na Muawiya, yalipozidiwa majeshi ya Muawiya, Amru bin A's akamshauri Muawiya:
Tutundike Misahafu katika ncha ya mikuki, kisha tuinue juu na tuyaambie majeshi ya Ali: Hii Qur'an ndiyo Hakimu kati yetu na nyinyi. Sasa, wako watakaokubali kusitisha mapigano kwa kuiheshimu Qur'an, na wako watakao kataa, Hapo patakuwa pametokea farka mbili miongoni mwao, na hilo litasababisha udhaifu katika jeshi.
Jamaa wakainua Misahafu juu, na kusema: "Kati yetu sisi na nyinyi tuhukumiwe na Qur'an" Imam Ali akawajibu: "KALIMATU HA'QQIN YURAADU BIHA BAATILUN" Yaani, Tamko (lililosemwa ni) kweli (lakini) lengo lake ni batili." Hapo baadhi ya wanafiki wakamtaka Imam Ali (a.s) kusitisha mapigano kwa kuiheshimu Qur'an waliyoinua maadui. Na Waislamu wenye msimamo wakawa pamoja na Imam Ali (a.s).
Wanafiki wakajitenga, wakatoka katika twaa ya Imam wao (Imam Ali)
Wakajikusanya Harawraa (Katika kijiji cha Kufa) kupanga maasi yao. Aliyeongoza maasi hayo ni Abdullah bin al-Kawaa, na wafuasi wake ni; Itabu bin Al-aawar, Abdullah bin Wahb Ar-Raasy, Urwa bin Jariir, Yazid bin Abin aaswim Almahaariby, Harquus bin Zuhayr Al-bajaly (anayejulikana kwa jina la) Dhuth thadya. Tangu siku hiyo, kikundi hiki kinaitwa: Khawariji. Maana ya Khawariji ni: Watu waliompinga Imam Ali bin Abi Talib (a.s).
Khawariji wamegawanyika makundi manane:
(a) Almahkama
(b) Albayhasiyya
(c) Al-Izaraqa
(d) An-Najdiyya
(e) Al-Ibadhiyya
(f) As-Sufriya
(g) Al-Ajaaridah
(h) Ath-Tha'alabah
Taz: Tafsirul Basair: J.44 Uk. 433-434
Tafsirul Basair: J.49 Uk. 531-561