70 SUURATUL MAA'RIJI

Sura hii imeteremshwa Makka,  na ina Aya 44

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea.

2. Juu ya makafiri, hapana awezaye kuizuia.[1]

3. Kutoka kwa Mwenyeezi Mungu, Mwenye utukufu mkubwa.

4. Malaika wa Roho hupanda kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini.

5. Basi subiri kwa subira njema.

6. Kwa hakika wanakiona kiko mbali (hicho Kiyama).

7. Nasi tunakiona kiko karibu.

8. Siku mbingu itakapokuwa kama shaba iliyoyeyuka.

9. Na milima itakuwa kama sufi.

10. Wala jamaa hatamuuliza jamaa (yake).

11. Ingawa watafanywa waonane, mwenye kosa atapenda ajikomboe katika adhabu ya siku hiyo kwa kulipa watoto wake.

12. Na mke wake na ndugu yake.

13. Na jamaa zake waliomzunguka.

14. Na (kulipa) vyote vilivyomo katika ardhi, kisha aokoke.

15. Sivyo, kwa hakika huo ni Moto uwakao.

16. Unaobabua ngozi ya mwili.

17. Utamwita kila aliyegeuza mgongo na akageuka.

18. Na akakusanya kisha akahifadhi.

19. Kwa hakika binadamu ameumbwa hali ya kuwa mwenye pupa.

20. Inapomgusa shari huwa mwenye fazaa.

21. Na inapomgusa kheri huwa anaizuilia.

22. Ila wanaoswali.

23. Ambao wanadumisha swala zao.

24. Na ambao katika mali zao iko sehemu maalumu.

25. Kwa ajili ya aombaye na anayezuilika kuomba.

26. Na ambao wanasadiki siku ya malipo.

27. Na ambao wanaogopa adhabu (itokayo) kwa Mola wao.

28. Hakika adhabu ya Mola wao si ya kusalimika.

29. Na ambao wanahifadhi tupu zao.

30. Isipokuwa kwa wake zao au wale waliomilikiwa na mikono yao, basi hao hawalaumiwi.

31. Lakini anayetaka kinyume cha hayo, basi hao ndio wanaoruka mipaka.

32. Na ambao wanaangalia amana zao na ahadi zao.

33. Na ambao ni imara katika ushahidi wao.

34. Na ambao wanazihifadhi, swala zao.

35. Hao ndio watakuwa katika Mabustani wakiheshimiwa.

36. Basi imekuwaje wanaokufuru wanakufia kwa haraka.

37. Vikosi vikosi, kwa upande wa kulia na kwa upande wa kushoto.

38. Je kila mmoja wao anatumai kwamba ataingizwa katika Bustani ya neema?

39. Sivyo, hakika tumewaumba katika kile wanachokijua.

40. Basi naapa kwa Mola wa mashariki zote na magharibi zote kwamba sisi tunaweza.

41. Kuwabadili (na kuleta) walio wema kuliko wao, na sisi hatushindwi.

42. Basi waache wapige porojo na wacheze mpaka waione siku yao wanayoahidiwa.

43. Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia kwenye mradi (wao).

44. Macho yao yatainama, unyonge utawafunika, hiyo ndiyo siku waliyokuwa wakiahidiwa.


[1] Aya 1-2

 AANGAMIZWA KWA KUKATAA KUTOA BAIA

Katika Mwaka wa kumi Hijria Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w alipokuwa akirejea kutoka Makka ambapo alikuwa ameongozana na Waislamu zaidi ya laki moja. Alipofika njia panda katika bonde la Khom, njia ziendazo Madina, Misri na Iraq, Hiyo ilikuwa siku ya Alhamisi tarehe kumi na nane mwaka wa kumi Hijria majira ya asubuhi, hapo Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya "Ewe Mtume! fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake 5:67.

Baada ya kushuka Aya hii, Mtume aliushika mkono wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) akasema: "Ambaye mimi natawalia mambo yake, basi huyu Ali nimtawala wake."

Maswahaba wakatoa BAIA (kiapo cha utiifu) lakini swahaba Harith bin Nuuman Alfihri alikataa na akaonyesha dharau mbele ya Mtume s.a.w na papo hapo Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya "Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea, juu ya makafiri hapana awezaye kuizuia."

Taz: Tafsirul Basair:    J.49 Uk. 7

Tafsirul Qurtubi:          J.18 Uk. 278

Shawahidut Tanzil:      J.2  Uk. 286

Alfutuuhatul ilahiyya (Aljamal)  J.4  Uk. 404