Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Nuun. (Naapa kwa) kalamu na yale wanayoyaandika.
2. Kwa neema ya Mola wako wewe si mwenda wazimu.
3. Na kwa hakika una malipo yasiyokatika.
4. Na bila shaka una tabia njema, Tukufu.
5. Basi karibuni utaona, na wao pia wataona.
6. Ni nani mwenye kichaa, miongoni mwenu.
7. Hakika Mola wako anajua sana aliyepotea katika njia yake, na yeye anajua sana walio ongoka.
8. Basi usiwatii waliokadhibisha.
9. Wanapenda ungelikuwa laini (kwao) nao wakawa laini.
10. Wala simtii kila mwapaji sana, aliye dhalili.
11. Msengenyaji aendaye akitia fitina.
12. Azuiye kheri, arukaye mipaka, mwenye hatia.
13. Mwenye roho ngumu, (na) juu ya hayo, mwana wa haramu.
14. Ingawa ni mwenye mali na watoto.
15. Anaposomewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa zamani.
16. Karibuni tutamtia kovu juu ya pua.
17. Hakika tumewajaribu kama tulivyowajaribu wenye bustani, walipoapa kwamba watayakata (matunda yake) itakapokuwa asubuhi.
18. Wala hawakusema: Insha allah.
19. Basi uliizingia (bustani) msiba mkubwa utokao kwa Mola wako na hali wao walikuwa wanalala.
20. Kwa hiyo ikawa kama iliyong'olewa.
21. Asubuhi wakaitana.
22. Kwamba: Nendeni mapema shambani kwenu ikiwa mnataka kuvuna.
23. Basi walikwenda na huku wakinong'onezana.
24. Kuwa: leo masikini asiingie humo mwenu.
25. Na wakaenda asubuhi, hali wanao uwezo wa kuzuia.
26. Basi walipoliona wakasema: Bila shaka tumepotea.
27. Bali tumenyimwa.
28. Mbora wao akasema: Je, sikukuambieni mbona hamumtukuzi (Mwenyeezi Mungu?).
29. Wakasema: Utukufu ni wa Mola wetu, hakika tulikuwa madhalimu.
30. Basi wakakabiliana wakilaumiana.
31. Wakasema: Ole wetu! hakika tulikuwa tumeruka mipaka.
32. Huenda Mola wetu atatubadilishia (shamba) lililo bora kuliko hili, hakika sisi tunajipendekeza kwa Mola wetu.
33. Kama hivyo itakuwa adhabu, na adhabu ya akhera ni kubwa zaidi laiti wangelijua.
34. Hakika wamchao (Mwenyeezi Mungu) watakuwa na bustani zenye neema kwa Mola wao.
35. Je, tuwafanye wanaotii sawa na waovu?
36. Mmekuwaje mnahukumu namna gani?
37. Au mnacho kitabu mnachokisoma.
38. Hakika yatakuwamo kwa ajili yenu mnayoyachagua.
39. Au je, mnavyo viapo juu yetu vinavyofika mpaka siku ya Kiyama, kuwa nyinyi mtapata mnayoyahukumu?
40. Waulize: Ni nani miongoni mwao mdhamini wa hayo?
41. Au je, wana washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli.
42. Siku ambayo yatakapokuwa matendo makali, na wataitwa kusujudu lakini hawataweza.
43. Macho yao yatainama, unyonge utawafunika, na hakika walikuwa wakiitwa kusujudu walipokuwa salama.
44. Basi niache na anayeikadhibisha hadithi hii, karibuni tutawavuta kidogo kidogo kwa mahala wasipopajua.
45. Na ninawapa muda, kwa hakika shauri langu ni madhubuti.
46. Au je, unawaomba malipo nao wanaelemewa na gharama?
47. Au iko kwao (elimu ya) siri nao wanaiandika?
48. Basi subiri hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama mmezwa na Samaki (Nabii Yunusu) alipomwita (Mwenyeezi Mungu) na hali yeye alikuwa mwenye huzuni nyingi.
49. Kama isingelimfikia neema kutoka kwa Mola wake, bila shaka angelitupwa ufukoni na hali yakuwa mwenye kulaumiwa.
50. Lakini Mola wake alimchagua na akamfanya miongoni mwa watu wema.
51. Na wale makafiri hukurubia kukutelezesha kwa (udokozi wa) macho yao, wanaposikia mawaidha (yao) na husema: Hakika yeye ni mwenda wazimu.
52. Na hayakuwa haya ila ni ukumbusho kwa walimwengu.