Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Ewe Nabii! Mnapowaacha wanawake, basi waacheni katika wakati wa eda zao, na fanyeni hesabu ya (siku) za eda, na mcheni Mwenyeezi Mungu, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao wala wasitoke wenyewe, mpaka wafanye jambo la ufasiki ulio wazi. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyeezi Mungu na anayeruka mipaka ya Mwenyeezi Mungu, basi hakika amejidhulumu nafsi yake. Hujui pengine Mwenyeezi Mungu atatokeza jambo jingine baada ya haya.[1]
2. Basi wanapofikia muda wao, ndipo muwaweke kwa wema, au achaneni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyoagizwa yule anayemwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu, (Mwenyeezi Mungu) humtengenezea njia ya kuokoka.
3. Na humpa riziki kwa mahala asipopatazamia, na anayemtegemea Mwenyeezi Mungu basi yeye humtoshea, kwa hakika Mwenyeezi Mungu anatimiza kusudi lake, hakika Mwenyeezi Mungu amekwisha kiwekea kila kitu kipimo.
4. Na wale waliokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (pia ndiyo eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi. Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi.
5. Hiyo ni amri ya Mwenyeezi Mungu aliyoiteremsha kwenu, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu humfutia maovu yake na humpa malipo makubwa.
6. Wawekeni humo humo mnamokaa nyinyi kama mpatavyo, wala msiwadhuru kwa kuwatia katika dhiki, na kama wakiwa na mimba, basi wagharamieni mpaka wajifungue.
Na kama wakikunyonyesheeni, basi toeni Malipo yao na shaurianeni kwa wema, na kama mkiona udhia baina yenu, basi amnyonyeshee (mwanamke) mwingine.
7. Mwenye wasaa agharimu kadri ya wasaa wake, na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, basi atoe katika kile alichompa Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu hamkalif'ishi mtu yeyote ila kwa kadri alivyompa, karibuni Mwenyeezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraja.
8. Na miji mingapi iliyovunja amri ya Mola wake na Mitume yake, basi tuliihesabu hesabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.
9. Basi ikauonja ubaya wa mambo yao, na mwisho wa mambo yao ilikuwa khasara.
10. Mwenyeezi Mungu amewaandalia adhabu kali, basi mcheni Mwenyeezi Mungu enyi wenye akili mlioamini, hakika Mwenyeezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho.
11. Mtume anayekusomeeni Aya za Mwenyeezi Mungu zinazobainisha, ili kuwatoa wale walioamini na wakatenda mema. katika giza kuwapeleka kwenye nuru, na anayemwamini Mwenyeezi Mungu na kutenda mema) atamwingiza katika Pepo zipitazo mito chini yake. watakaa humo milele. Bila shaka Mwenyeezi Mungu amekwishampa riziki nzuri.
12. Mwenyeezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba na ardhi mfano wa hizo. amri zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyeezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa elimu.
[1] Aya' 1
TALAKA NA TARATIBU ZAKE
Talaka (kuacha mke), kwa kuwa talaka haipatikani kabla ya kutimia tendo la ndoa, ni vyema basi kutaja hapa japo kwa ufupi somo la ndoa. Ili kujua mke anapatikanaje, kwa kuzingatia sifa zipi, hapa yafuatayo ni mafundisho ya Mtume s.a.w kuhusu kupata mke bora:
Anasema Mtume s.a.w kuwa: "(Mtu) hakujenga jengo lolote katika Uislaamu lenye kupendeza zaidi kwa Mwenyeezi Mungu kuliko kuowa."
Taz: Wasailush shia, j.20 Uk. 14
Aliulizwa Imam Jaafar As Saadiq (a.s) kuwa: "Mtu anayetaka kuposa, anaruhusiwa kumwangalia mposwaji? Imam akajibu, ndiyo, si vibaya mwanamume kumwangalia mwanamke anayetaka kumuowa. Amwangalie uso wake na nyuma (ya maungo) yake."
Taz: Al-waafy J.21 Uk. 372
Anasema Mtume s.a.w kuwa: "Oweni mwanamke bikra mwenye kizazi, wala msiowe mwanamke mzuri wa kupendeza (lakini) asiye na kizazi, kwa sababu mimi nitajifakhiri kwenu kwa umma zingine siku ya Kiyama."
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 54
"Hakika (msichana) bikra ni kama tunda lilioko mtini, litakapowiva na lisichumwe huharibiwa najua, kisha hupukutishwa na upepo. Ndivyo hivyo hivyo msichana bikra anapobaleghe, hana dawa yoyote isipokuwa mume, na kama si hivyo basi hatasalimika na fisadi, kwa sababu wao ni binadamu. Mtu mmoja akauliza, tuwaoze kwa kina nani? Mtume akajibu: Kwa mume anayefaa. Akauliza: Mtu mwenye kufaa ni yupi? Mtume akajibu: Waumini wao kwa wao ndio wenye kufaa."
Taz: Wasailush shia J.20 .Uk. 62
"Hakika Mwenyeezi Mungu amekuhalalishieni tupu tatu: Utupu wa mwanamke aliyeolewa kwa ndoa ya kudumu, na utupu wa mwanamke aliyeolewa kwa ndoa ya mut-a, na utupu wa mwanamke aliyemilikiwa na mikono yenu."
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 86
KUMWINGILIA
Unapomwingilia mke useme: "Bismillahi wabillahi allahumma jannibnii shaitwana wajannibish shaitwana maa razaqtanii."
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 1.36
Mtume amekataza kumwingilia mke mwanzo wa kuandama mwezi, na tarehe kumi na tano ya mwezi, na mwisho wa mwezi.
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 128
Ni kosa kumwingilia mke na hali wameelekea kibla (na hali ya kukipa mgongo).
Mume asimwingilie mke katika meli (wakati ikienda).
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 138
Ni haramu kumwingiha mke katika utupu wa nyuma.
Taz: Wasailush shia J.20 Uk. 142
Ni hararnu kumwingilia mke hali amevaa pete iliyo na jina la Mwenyeezi Mungu au Aya ya Qur'an.
Taz: Wasailu shia J.20 Uk.148
Vile vile majina ya Mitume na Maimam.
Iliposemwa: "Basi waacheni katika wakati wa eda zao" Kumwacha mwanamke wakati wa eda yake, ni kumwacha wakati akiwa katika twahara (hana hedhi wala nifasi) ambayo hakuingiliwa.
Maana ya talaka ni: Mtu kumwacha mkewe talaka moja ya rejea, kisha akabaki bila ya kuolewa mpaka muda wa eda yake umalizike.
Maneno yanayokubaliwa katika kuthibiti talaka ni: Wewe mwenye kuachika, Fulani umeachika, Wewe kaa eda.
Maneno haya sawa sawa yatatamkwa au kuandikwa, yatathibitisha kuwa ni talaka, kama mwenye kuacha atasema: Wewe nimekuacha talaka mbili au tatu, au kumi au...... hapo itazingatiwa kuwa ni talaka moja tu.
Katika kuacha mke ni lazima kuzingatia mambo yafuatayo:
1. Kumwacha wakati akiwa katika tohara (hayumo katika hedhi wala nifasi) ambayo hakuingiliwa.
2. Kushuhudisha mashahidi wawili wanaume walio waadilifu.
3. Kutomtoa nyumbani mwake, wala yeye (mwanamke) asitoke.
4. Muda atakaobaki nyumbani mwake, akae kwa adabu na heshima, akifanya uovu uliowazi, kama kuzini, au ugomvi baina ya familia ya mtalaka wake, hapo atatolewa katika nyumba hiyo. Akiwa nyumbani mwake anayo haki ya kupata huduma zote za kibinadamu. Na hii ni kwa mke aliyeachwa talaka ya kurejewa tu.
5. Muda wa eda, kwa Mwanamke asiyetokwa na hedhi kwa sababu zozote, ni miezi mitatu.
6. Mwanamke anayepata hedhi. muda wa eda yake ni tohara tatu.
7. Mwanamke mwenye mimba muda wa eda yake ni kuzaa, hata kama dakika moja baada ya kuachwa.
Lakini, mwanamke aliyeachwa, baina ya kukaa kwake eda, akagundua kuwa anayo mimba, basi atasubiri muda wa miezi tisa. Mimba ikiwamo ,itazaa, na eda imekwisha, ikiwa hana mimba, basi akae eda (baada ya hapo) kwa miezi mitatu.
8. Mwanamke aliyefiwa na mume, muda wa eda yake ni miezi minne na siku kumi ikiwa hana mimba. Na kama ana mimba, na akazaa kabla ya kutimia miezi minne na siku kumi, basi baada ya kuzaa atakaa eda miezi minne na siku kumi.
Na ikiwa atazaa usawa na miezi minne na siku kumi, itamlazimu baada ya kuzaa akae eda miezi minne na siku kumi.
Taz: Wasailush shia, j.22 Uk. 240
9. Mwanamke mwenye mimba akiachwa, basi wakati wowote akizaa. anafaa kuolewa pale pale, isipokuwa hataingiliwa mpaka damu ya uzazi ikatike.
Taz: Wasailush shia, j.22 uk. 272
10. Mwanamke aliyejikhuluu, au aliyeachwa mara tatu, na anaye dada, basi mwanamume aliyekuwa mume anaweza kumuoa dada ya mwanamke aliyejikhuluu, au dada ya mwanamke aliyeachwa mara tatu, hata kabla ya muda wa eda yake kwisha.
Taz: Wasailush shia J.22 Uk. 270
Kujikhuluu, maana yake ni: Kujikomboa.
11. Ikiwa mume ana wake wanne, kisha akamuwacha mmoja, basi hataruhusiwa kuoa mpaka muda wa eda ya mwanamke aliyemwacha umalizike.
Taz: Wasailush shia J.22 Uk. 269
KUREJEA
(a) Kurejea ni, Kumrejesha mwanamke aliyeachwa kwenye ndoa yake ya awali.
Hakuna kurejea kwa mwanamke aliyeachwa mara tatu, au kwa mwanamke aliyeishiwa muda wake wa eda. Yaani, mwanamke aliyeachwa mara tatu, hawezi kurudi kwa bwana aliyemwacha mpaka: Aolewe na mwanamume mwingine na amwingilie, kisha amwache, akae eda mpaka ishe. Hapo anaruhusiwa yule bwana aliyemwacha mwanzo kumuoa.
Na, mwanamke aliyeishiwa muda wake wa eda, harejewi, isipokuwa huposwa akaolewa.
(b) Kurejea yaweza kuwa kwa matamko, yakiandikwa au kusemwa: "Fulani nimekurejea" ''Nimekurudisha katika ndoa yangu' Haya yatasemwa au kuandikwa kwa lugha yoyote wanayofahamiana wenyewe (aliyeacha na aliyeachwa).
(c) Kurejea yaweza pia kuwa kwa kitendo, kama: Kumbusu, kumwingilia akiwa macho na akili timamu.
(d) Bwana akisha tamka kumrejea, pale pale huthibiti kuwa ni mke, hata kama yule bibi atakataa kurejewa.
(e) Mume kukataa talaka kuwa: "Hakuitoa" basi hiyo ni dalili ya kumrejea mke.
(f) Katika kurejea mke, mashahidi si lazima wawepo.
Taz: Tahriirul Wasiila J.2 Uk. 310
Sharaaiul Islaami J.3 Uk. 30
Fiq-hul Imam Jaafar J.6 Uk. 48-52