Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Vinamtukuza Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, Mfalme, Mtakatifu, Mwenve nguvu, Mwenye hekima.
2. Yeye ndiye aliyeleta Mtume katika watu wasiojua kusoma, anayetokana nao, anawasomea Aya zake na kuwatakasa na kuwafunza Kitabu na hekima, na ingawa kabla (ya haya) kwa hakika walikuwa katika upotovu dhahiri.
3. Na (amemleta) kwa wengine miongoni mwao walio bado kuungana nao, na yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
4. Hayo ni fadhili ya Mwenyeezi Mungu anampa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye fadhili kuu.
5. Mfano wa wale waliopewa Taurali kisha hawakuichukua. ni kama mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa, mfano mbaya mno wa watu waliozikadhibisha Aya za Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
6. Sema: Enyi Mayahudi kama mnadai kuwa nyinyi ni wapenzi wa Mwenyeezi Mungu pasipokuwa watu wengine, basi yatamanini mauti ikiwa mnasema kweli.
7. Lakini hawatayatamani kabisa kwa sababu ya yale iliyoyatanguliza mikono yao, na Mwenyeezi Mungu anawajua madhalimu.
8. Sema: Hakika mauti yake mnayoyakimbia bila shaka yatakutana nanyi, kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri, ndipo atakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.
9. Enyi mlioamini! inaponadiwa kwa ajili ya swala siku ya Ijumaa, basi nendeni upesi kumtaja Mwenyeezi Mungu na acheni biashara, hiyo ni bora kwenu ikiwa mnajua.
10. Na itakapokwisha swala basi tawanyikeni katika ardhi na tafuteni fadhili za Mwenyeezi Mungu, na mtajeni Mwenyeezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.
1 1. Na wanapoiona biashara au mchezo wanavikimbilia na wanakuacha umesimama, sema: Yaliyoko kwa Mwenyeezi Mungu ni bora kuliko mchezo na biashara, na Mwenyeezi Mung.u ni Mbora wa watoa riziki.