Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Mwenyeezi Mungu amekwisha sikia usemi wa mwanamke, yule aliyejadiliana nawe kwa sababu ya mumewe, na akashtaki mbele ya Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu anayasikia majibizano yenu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
2. Wale miongoni mwenu wawaitao wake zao mama, wao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale waliowazaa, na kwa hakika wao wanasema maneno mabaya na ya uongo, na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye msamaha.
3. Na wale wawaitao wake zao mama, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema, basi wampe uhuru mtumwa kabla ya kugusana, hayo ndiyo mnayoagizwa, na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyatenda.
4. Na asiyepata (mtumwa) basi afunge saumu miezi miwili inayoandamana kabla ya kugusana, na asiyeweza, basi awalishe masikini sitini, (mmeambiwa) hayo ili mmwamini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na hiyo ni mipaka ya Mwenyeezi Mungu, na kwa makafiri iko adhabu yenye kuumiza.
5. Hakika wale wanaompinga Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. watadhalilishwa kama walivyodhalilishwa wale waliotangulia na tumekwisha teremsha Aya zilizo wazi, na makafiri watapata adhabu ifedheheshayo.
6. Siku Mwenyeezi Mungu atakayowafufua wote, ndipo atawaambia yale waliyoyatenda, Mwenyeezi Mungu ameyadhibiti, na wao waliyasahau, na Mwenyeezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
7. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu anajua viliyomo mbinguni na viliyomo ardhini? Hawashauriani kwa siri watatu ila yeye ni wa nne wao, wala watano ila yeye ni wa sita wao, wala wachache kuliko hao wala zaidi ila yeye huwa pamoja nao popote walipo. Kisha siku ya Kiyama atawaambia waliyoyatenda hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
8. Je huwaoni wale waliokatazwa kunong'onezana, kisha wakayarudia waliyokatazwa, na wananong'onezana juu ya mambo ya dhambi na ya jeuri na ya kumuasi Mtume? na wafikapo kwako wanakuamkia kwa (maamkio) asiyokuamkia Mwenyeezi Mungu, na husema katika nyoyo zao: Mbona Mwenyeezi Mungu hatuadhibu kwa haya tusemayo? Jahannam itawatosha, wataingia hapo na mahala pabaya sana pa kurudia.
9. Enyi mlioamini! mnaponong'ona, basi msinong'one juu ya mambo ya dhambi na ya jeuri na ya kumuasi Mtume, bali zungumzeni juu ya wema na ucha Mungu na mcheni Mwenyeezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa.
10. Kwa hakika mazungumzo (mabaya) yanatokana na shetani ili awahuzunishe wale walioamini. lakini hawezi kuwadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, na Waumini, basi wamtegemee Mwenyeezi Mungu tu.
11. Enyi mlioamini! mnapoambiwa: Fanyeni nafasi katika vikao, basi fanyeni nafasi, Mwenyeezi Mungu atakufanyieni nafasi na inaposemwa simameni. basi simameni. Mwenyeezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.
12. Enyi mlioamini! mnaposema siri na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya kumsemeza hayo ni bora kwenu na ni safi sana, ikiwa hamkupata (cha kutoa) basi Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.[1]
13. Je, nyinyi mnaogopa kuwa hamtaweza kutanguliza sadaka kabla ya kumsemeza kwenu? Basi msipotenda (haya) na Mwenyeezi Mungu amekusameheni. Basi simamisheni swala na toeni zaka na mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.
14. Je huoni wale waliofanya urafiki na watu aliowakasirikia Mwenyeezi Mungu? hao si miongoni mwenu wala si miongoni mwao, na huapa kwa uongo hali wanajua.
15. Mwenyeezi Mungu amewaandalia adhabu kali, kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda na mabaya.
16. Wamefanya kiapo chao kuwa ngao, wakaepuka njia ya Mwenyeezi Mungu basi itakuwa kwao adhabu ifedheheshayo.
17. Mali zao na watoto wao havitawafaa kitu mbele ya Mwenyeezi Mungu. hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.
18. Siku atakayowafufua Mwenyeezi Mungu wote, ndipo wataapa kwake kama wanavyoapa kwenu, na wanadhani kuwa wana kitu, oh! kwa hakika wao ni waongo hasa.
19. Shetani amewatawala, kwa hiyo akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyeezi Mungu! kwa hakika kundi la shetani ndilo lenye kukhasirika.
20. Bila shaka wale wanaompinga Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa waliodhalilika.
21. Mwenyeezi Mungu amekwisha andika; lazima nitashinda Mimi na Mitume wangu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye heshima.
22. Hupati watu wanaomuamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, kuwa wanawapenda wale wanaompinga Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao. Hao ndio ambao (Mwenyeezi Mungu) ameandika nyoyoni mwao imani na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake, na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito chini yake, humo watakaa milele Mwenyeezi Mungu amekuwa radhi nao, na wao wamekuwa radhi naye, hao ndio kundi la Mwenyeezi Mungu, Sikilizeni! hakika kundi la Mwenyeezi Mungu ndilo linalofaulu.
[1] Aya 12
IMAM ALI AZUNGUMZA FARAGHA NA MTUME
Mtu wa kwanza kutoa sadaka na akapata nafasi ya kuzungumza na Mtume faragha, ni Imam Ali bin Abi Talib (a.s) Kisha ikashuka Aya ya 13 ya sura hii hii kuondoa sharti ya kutoa sadaka. Ibn Umar anasema: "Ali bin Abi Talib alikuwa ana mambo matatu, laiti mimi ningekuwa na moja tu katika hayo, ingependeza mno kwangu mimi kuliko kuwa na ngamia mwekundu: Kumuoa F'atima, na kupewa bendera siku ya Khaybara, na kupata Aya tun Najwaa (Aya ya 12 ya sura hii").
Kwa ajili hii, Imam Ali (a.s) anasema: "Hakika katika Kitabu cha Mwenyeezi Mungu kuna Aya ambayo hakuna yeyote kabla yangu aliyeitumia (maagizo yake) wala hakuna yeyote baada yangu atakayeitumia, ni Ayatun Najwaa. Nilikuwa na dinari moja nikaiuza kwa dirhamu kumi kwa hiyo nikawa kila ninapotaka kuzungumza faragha na Mtume mimi natoa dirhamu moja kisha hukumu hii ikafutwa kwa Aya ya 13 ya sura hii hii (Almujaadilah)."
Taz: Fat’hulbayani flyimaqasidil Qur'an J.14 Uk. 28
Alburhan fyitafsiril Qur'an J.4 Uk. 307-308
Majmaul bayani fyitafsiril Qur'an J.5 Uk. 252
Addurrul Manthur J.6 Uk. 272