Kwa jma la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Enyi mlioamini! msitangulize (kusema) mbele ya Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
2. Enyi mlioamini! msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa sauti kubwa kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi visije vitendo vyenu vikaharibika na hali hamtambui.
3. Kwa hakika wale wanaoinamisha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyeezi Mungu hao ndio Mwenyeezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa kumuogopa Mwenyeezi Mungu, watapata msamaha na malipo makubwa.
4. Kwa hakika wale wanaokuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawafahamu.
5. Na kama wangelingoja mpaka uwatokee, ingekuwa bora kwao, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Enyi mlioamini! kama fasiki akikujieni na khabari yoyote, basi pelelezeni. msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu va yale mliyoyatenda.
7. Na jueni kwamba Mtume wa Mwenyeezi Mungu yuko pamoja nanyi, lau yeye angekutiini katika mambo mengi lazima mngetaabika. Lakini Mwenyeezi Mungu ameipendezesha kwenu imani na ameipamba nyoyoni mwenu, na amekufanyeni mchukie ukafiri na ufasiki na uasi, hao ndio walio ongoka.
8. Kwa fadhili za Mwenyeezi Mungu na neema zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
9. Na ikiwa makundi mawili katika Waumini wanapigana, basi fanyeni suluhu kati yao, na ikiwa moja la hayo linamdhulumu mweziwe, basi lipigeni lile Iinaloonea mpaka lirudie katika amri ya Mwenyeezi Mungu. Na kama likirudi, basi yapatanisheni baina yao kwa uadilifu, na hukumuni kwa haki, hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.
10. Kwa hakika wenye kuamini tu ndio ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Mwenyeezi Mungu, ili mrehemewe.
11. Enyi mlioamini! wanaume wasiwadharau wanaume wenzao huenda wakawa bora kuliko wao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao, huenda wakawa bora kuliko wao. Wala msitukanane kwa kabila wala, msiitane kwa majina mabaya (ya kejeli) jina baya baada ya imani ni uovu, na asiyetubu, basi hao ndio madhalimu.
12. Enyi mlioamini! jiepusheni sana na dhana kwani dhana ni dhambi wakati mwingine, wala msipeleleze, wala baadhi yenu wasiwatete wengine. Je, mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? mnalichukia hilo na mcheni Mwenyeezi Mungu, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kupokea toba Mwenye kurehemu.
13. Enyi mlioamini kwa hakika tumekuumbeni kutokana na mwanaume na mwanamke, na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane, hakika aliye mtukufu zaidi kati yetu kwa Mwenyeezi Mungu ni aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye khabari.
14. Walisema wanaokaa jangwani: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu, maana imani haijaingia nyoyoni mwenu, na mkimtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
15. Kwa hakika wenye kuamini ni wale tu waliomwamini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakapigania dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, hao ndio wakweli.
16. Sema: Je, mtamjulisha Mwenyeezi Mungu dini yenu, na hali Mwenyeezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na ardhini, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
17. Wanakusimbulia kwa kuingia kwao Uislamuni. sema msifanye kuwa ni ihsani kwangu kusilimu kwenu, bali Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekufanyieni ihsani kwa kukuongozeni katika Uislaamu, ikiwa nyinyi ni wa kweli.
18. Bila shaka Mwenyeezi Mungu anayajua yaliyofichikana mbinguni na ardhini, na Mwenyeezi Mungu anaona mnayoyatenda.