Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Haa Mym.
2. Uteremsho wa Kitabu utokao kwa Mwenyeezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
3. Bila shaka katika mbingu na ardhi mna mazingatio kwa ajili ya wenye kuamini.
4. Na katika umbo lenu na katika wanyama aliowatawanya mna mazingatio kwa watu wenye yakini.
5. Na (katika) kupishana usiku na mchana na (katika) riziki aliyoteremsha Mwenyeezi Mungu kutoka mawinguni na akaifufua kwayo ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya pepo, mna mazingatio kwa watu wanaozingatia.
6. Hizo ndizo Aya za Mwenyeezi Mungu tunazo kusomea kwa ukweli, basi hadithi gani watakayoiamini baada ya Mwenyeezi Mungu na Aya zake?
7. Kuangamia ni kwa kila atungaye uongo, mwenye dhambi.
8. Anayesikia Aya za Mwenyeezi Mungu zikisomwa juu yake, kisha anashikilia kujivuna kama kwamba hakuzisikia, basi mpe khabari ya adhabu yenye kuumiza,
9. Na anapojua kidogo katika Aya zetu hizo huzifanyia mzaha, hao ndio watakaokuwa na adhabu yenye kufedhehesha.
10. Na nyuma yao iko Jahannam, wala waliyoyachuma hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi waliowashika badala ya Mwenyeezi Mungu, na watapata adhabu kubwa.
11. Huu ni muongozo, na wale waliozikataa Aya za Mola wao watakuwa na adhabu yenye maumivu iumizayo.
12. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekutiishieni bahari ili humo zipite jahazi kwa amri yake na ili mtafute fadhili yake na mpate kushukuru.
13. Na amekutiishieni vilivyomo mbinguni, na vilivyomo ardhini vyote vimetoka kwake, bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu
wanaotafakari.
14. Waambie wale walioamini wawasamehe wale wasioziogopa siku za Mwenyeezi Mungu ili awalipe watu kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.
15. Mwenye kutenda wema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kufanya uovu ni juu yake, kisha mtarudishwa kwa Mola wenu.
16. Na kwa hakika tuliwapa wana wa Israeli Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawapa vitu vizuri na tukawafadhili kuliko walimwengu.
17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri, lakini hawakukhitilafiana ila baada ya kuwafikia elimu, kwa uasi baina yao (tu), hakika Mola wako atahukumu kati yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.
18. Kisha tumekuweka juu ya Sharia (njia nyoofu) hasa katika amri, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wale wasiojua.
19. Kwani wao hawatakufaa chochote mbele ya Mwenyeezi Mungu, na hakika madhalimu ni marafiki wao kwa wao, na Mwenyeezi Mungu ni Rafiki ya wenye kumcha (yeye).
20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu, na ni muongozo na rehema kwa watu wenye yakini.
21. Je, wanafikiri wale waliofanya maovu kuwa tutawafanya kama wale walioamini na kutenda mema kwamba rnaisha yao na mauti yao yawe sawa? Ni mabaya wanayoyahukumu.
22. Na Mwenyeezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa.
23. Je, umemuona yule aliyefanya tamaa yake kuwa mungu wake, na Mwenyeezi Mungu akampoteza licha ya elimu na akapiga muhuri juu ya masikio yake na moyo wake, na kumtia kitanga machoni pake basi nani atamuongoza baada ya Mwenyeezi Mungu? Basi je, hamkumbuki?
24. Na walisema: Haukuwa (uhai) ila uhai wetu wa dunia, tunakufa na tunaishi wala hakuna kinachotuangamiza isipokuwa ulimwengu. Lakini wao hawana elimu ya hayo ila wanadhani tu.
25. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: WaletenJ baba zetu ikiwa nyinyi ni wakweli.
26. Sema Mwenyeezi Mungu anakupeni uhai kisha anakufisheni, kisha atakukusanyeni siku ya Kiyama, haina shaka, lakini watu wengi hawajui.
27. Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyeezi Mungu na siku kitakapotokea Kiyama, siku hiyo wataangamia washikao batili.
28. Na utaona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa kwenye kitabu chake: Leo mtalipwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
29. Hili daftari letu linakuambieni kweli: Bila shaka tulikuwa tukiyaandika yale mliyokuwa mkiyatenda.
30. Lakini wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaingiza katika rehema yake, huko ndiko kufanikiwa kuliko dhahiri.
31. Na wale waliokufuru (wataambiwa) Je, hazikuwa Aya zangu zikisomwa kwenu nanyi mkajivuna na mkawa watu waovu.
32. Na iliposemwa: Hakika ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni kweli na Kiyama hakina shaka, mkasema: Hatujui Kiyama ni nini, hatudhani ila kukisia tu wala hatuna yakini.
33. Na ubaya wa waliyoyatenda utawadhihirikia na yatawazunguka yale waliyoyafanyia mzaha.
34. Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyosahau mkutano wa siku yenu hii, na mahala penu ni Motoni, wala hamna wasaidizi.
35. Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyeezi Mungu na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hawatakubaliwa udhuru (wao).
36. Basi sifa zote njema ni za Mwenyeezi Mungu Muumba wa mbingu na Muumba wa ardhi, Muumba wa walimwengu.
37. Na ukubwa niwake mbinguni na ardhini, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.