Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu,
1. Haa Mym.
2. Uteremsho utokao kwa Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
3. Ni Kitabu kinachoelezwa Aya zake, Our'an yenye uwazi kwa watu wanaojua.
4. Itowayo khabari njema na ionyayo, lakini wengi wao wamepuuza, kwa hiyo hawasikii.
5. Na wakasema: Nyoyo zetu zi katika vifuniko kwa yale unayo tuitia, na katika masikio yetu mna uzito, na baina yetu na yako pana pazia, basi fanya nasi pia tunafanya.
6. Sema: Bila shaka mimi ni mtu kama nyinyi, ninaletewa Wahyi kwamba:
Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu, basi kuweni sawa kwa ajili yake, na mtakeni msamaha, na ole kwa washirikina.
7. Ambao hawatoi zaka nao ndio huikataa Akhera.
8. Hakika wale walioamini na kutenda mema yatakuwa kwao malipo yasiyokoma.
9. Sema; Je, kwa hakika mnamkataa aliyeumba ardhi katika nyakati mbili, na mnampa washirika? Huyo ndiye Mola wa walimwengu.
10. Na akaweka humo milima juu yake na akabarikia humo na akapima humo chakula chake katika nyakati nne, ni sawa kwa waulizao.
11. Kisha akaielekea mbingu na hali i moshi, ndipo alipoiambia (mbingu) na ardhi: Njooni mkipenda au msipende, vyote viwili vikasema: Tumekuja hali ya kuwa wenye kutii.
12. Basi akazifanya mbingu saba katika nyakati mbili, na kila mbingu akaifunulia kazi. yake, na tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa na kuilinda, hicho ndicho kipimo cha Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
13. Basi kama wakipuuza, sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi.
14. Walipowafikia Mitume mbele yao na nyuma yao, (wakaambiwa) Msiabudu ila Mwenyeezi Mungu tu. Wakasema: Angelitaka Mola wetu, bila shaka angeteremsha Malaika, na hakika sisi tunayakataa mliyotumwa nayo.
15. Basi A'di walitakabari katika ardhi bila ya haki na wakasema: Ni nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi? Je, hawakuona kwamba, Mwenyeezi Mungu aliyewaumba ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Nao walikuwa wakizikataa Aya zetu.
16.Basi tuliwapelekea kimbunga katika siku ya mkosi ili tuwaonjeshe adhabu ya fedheha katika maisha ya dunia, na bila shaka adhabu ya Akhera yafedhehesha zaidi, nao hawatasaidia.
17. Na Thamudi tuliwaongoza lakini walipenda upofu kuliko kuongoka, basi mngurumo wa adhabu ifedheheshayo ukawashika kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
18. Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa wakijilinda (na mabaya).
19. Na siku watakayokusanywa maadui wa Mwenyeezi Mungu kwenye Moto, nao watapangwa makundi makundi.
20. Hata watakapoufikia, ndipo masikio yao, na macho yao, na ngozi zao vitatoa ushahidi juu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.
21. Nao wataziambia ngozi zao. Mbona mnatushuhudia? Zitasema:
Mwenyeezi Mungu aliyekitamkisha kila kitu ndiye ametutamkisha, naye alikuumbeni mara ya kwanza na kwake mtarudishwa.
22. Na hamkuwa wenye kujificha ili masikio yenu na macho yenu na ngozi zenu visitoe ushahidi juu yenu, bali mlidhani ya kwamba Mwenyeezi Mungu hayajui mengi katika yale mnayoyafanya.
23. Na hiyo dhana yenu mliyomdhania Mola wenu imekuangamizeni, na mmekuwa miongoni mwa wenye khasara.
24. Hawa wakisubiri, Moto ndiyo makazi yao, na kama wakitoa udhuru pia hawatakuwa miongoni mwa wanaokubaliwa.
25. Na tukawawekea marafiki waliowapambia yale yaliyo mbele yao na nyuma yao, na kauli imelazimika juu yao katika mataifa yaliyopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu, hakika wao walikuwa wenye khasara.
26. Na walisema waliokufuru, Msisikilize Qur'an hii na ipigieni makelele (inaposomwa) huenda mtashinda.
27. Basi waliokufuru kwa hakika tutawaonjesha adhabu kali na kwa hakika tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
28. Hayo ndiyo malipo ya maadui wa Mwenyeezi Mungu, Moto, humo watakuwa na nyumba ya kukaa milele, ndiyo malipo kwa sababu walikuwa wakizikataa Aya zetu.
29. Na wale waliokufuru watasema: Mola wetu! tuonyeshe (makundi) mawili yaliyotupoteza miongoni mwa majinni na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
30. Hakka wale wanaosema: Mola wetu ni Mwenyeezi Mungu. kisha wakaendelea kwa kudumu kuwateremkia Malaika (wakiwaambia): Msiogope wala msihuzunike, na furahieni Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.
31.Sisi ni Walinzi wenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata mtakavyoviomba.
32.Ni takrima itokayo kwa Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
33. Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye kwa Mwenyeezi Mungu na kufanya vitendo vizuri na akasema: Hakika mimi ni miongoni mwa watii.
34.Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Zuia (ubaya) kwa yaliyo mema zaidi, na mara yule ambaye baina yako na yeye pana uadui atakuwa kama rafiki mkubwa.
35.Lakini (jambo hili) hawatapewa ila wale wanaosubiri, wala hawatapewa ila wenye bahati kubwa.
36. Na kama shetani akikushawishi kwa tash'wishi, basi jikinge kwa Mwenyeezi Mungu bila shaka yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
37.Na katika dalili zake ni usiku na mchana na jua na mwezi, msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyeezi Mungu aliyeviumba, ikiwa nyinyi mnamwabudu yeye tu.
38. Na kama wakitakabari, basi walioko kwa Mola wako wanamsabihi usiku na mchana nao hawachoki.
39. Na katika dalili zake ni kwamba, wewe unaiona ardhi inatulia lakini tunapoiteremshia maji inashtuka na kuumuka. Hakika aliyeihuisha ardhi lazima ndiye Mwenye kuhuisha wafu, hakika yeye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
40. Kwa hakika wale wanaozipotoa Aya zetu hawatufichi. Je, atakayetupwa Motoni ni bora au atakayekuja kwa amani siku ya Kiyama? Fanyeni mnavyopenda, kwa hakika yeye anayaona mnayoyafanya.
41. Kwa hakika wale wanaoyakataa mawaidha yanapowafikia (tutawaadhibu) bila shaka hicho ni Kitabu chenye kuheshimika.
42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.
43. Hukuambiwa ila ni yale yale waliyoambiwa Mitume wa kabila yako kwa hakika Mola wako ni Mwenye kusamehe na Mwenye adhabu yenye kuumiza.
44. Na lau kama tungeliifanya Qur'an kwa lugha ya kigeni, lazima wangelisema: Kwa nini Aya zake hazikupambanuliwa? Lo! Lugha ya kigeni na Mwarabu! sema: Huo ni muongozo na ponyo kwa wale walioamini, na wale wasioamini katika masikio yao mna uziwi, nayo kwao imezibwa hawaioni, hao ndio watakaoitwa kutoka mahala pa mbali.
45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake, na lau isingekuwa kauli iliyotangulia kutoka kwa Mola wako, lazima wangehukumiwa (sasa hivi) na kwa hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
46. Mwenye kutenda mema ni kwa nafsi yake, na mwenye kutenda ubaya ni juu ya nafsi yake, na Mola wako si dhalimu (hata kidogo) kwa waja (wake).
47. Ujuzi wa kujua Kiyama unarudishwa kwake. Na matunda hayatoki katika vifuniko vyao wala mwanamke hachukui mimba wala hazai ila kwa ujuzi wake. Na siku atakayowaita: Wako wapi washirika wangu? Watasema: Tunakiri kwako, kuwa, hakuna shahidi miongoni mwetu.
48. Na wale waliokuwa wakiwaabudu zamani watawapotea, na watadhani kuwa hawana pa kukimbilia.
49. Mwanadamu hachoki kuomba dua ya kheri na inapompata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
50. Na kama tukimuonjesha rehema yetu baada ya dhara iliyomgusa bila shaka atasema: Hii ndiyo yangu, wala sidhani kuwa Kiyama kitatokea, na kama nilirudishwa kwa Mola wangu, bila shaka yako mema kwake yaliyowekwa kwa ajili yangu. Basi tutawajulisha wale waliokufuru hayo waliyoyatenda na lazima tutawaonjesha adhabu ngumu.
51. Na tunapomneemesha mwanadamu. Hugeuka na kujitenga upande na inapomgusa shari huomba sana.
52. Sema: Mnaonaje, ikiwa kama (maneno) haya yametoka kwa Mwenyeezi Mungu kisha mkayakataa, ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule aliye katika upinzani wambali?
53. Tutawaonyesha dalili zetu katika nchi za mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba hayo ni kweli. Je, haikutoshi kwamba, Mola wako ni shahidi wa kila kitu?
54. Tahadharini bila shaka wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao. Angalieni! hakika yeye amekizunguka kila kitu.