36 SUURA YAASIIN

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 83

Kwa jina la mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

1. Yaa syn.

2. Naapa kwa Qur'an yenye kutengenezwa vizuri.

3. Hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.

4. (Uko) juu ya njia iliyonyooka.

5. Ni uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

6. Ili uwaonye watu ambao hawakuonywa baba zao, basi wao wameghafilika.

7. Bila shaka kauli (ya adhabu) imehakiki juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.

8. Hakika sisi tumeiweka minyororo shingoni mwao nayo inafika videvuni kwa hiyo vichwa vyao vikainuliwa.

9. Na tumeweka kinga mbele yao na kinga nyuma yao na tumewafunika kwa hiyo hawaoni.

10. Ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye hawataamini.

11. Unaweza kumuonya yule tu anayefuata mawaidha na akamuogopa Rahmani kwa siri, basi mpe khabari za furaha kwa kupata msamaha na malipo yenye heshima.

12. Kwa hakika sisi tunawahuisha wafu, na tunayaandika waliyoyatanguliza na nyayo zao, na kila kitu tumekihifadhi katika daftari lenye kubainisha.

13. Na wapigie mfano (wa) wakazi wa mji Mitume walipoufikia.

14. Tulipowapelekea (Mitume) wawili nao wakawakadhibisha, basi tukawazidishia nguvu kwa (Mtume) wa tatu, nao wakasema: Kwa hakika sisi tumetumwa kwenu.

15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi, wala Mwenyeezi Mungu hakuteremsha chochote, nyinyi mnasema uongo.

16. Wakasema: Mola wetu anajua, bila shaka sisi tumetumwa kwenu.

17. Wala si juu yetu ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.

18. Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu, kama hamtaacha lazima tutakupigeni mawe, na bila shaka itakufikieni kutoka kwenu adhabu yenye kuumiza.

19. Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe, je, kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu mnaopindukia mipaka.

20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mji akasema: Enyi watu wangu! wafuateni Mitume.

21. Mfuateni asiyekuombeni malipo, na hao wameongoka.

22. Na nimekuwaje nisimwabudu yule aliyeniumha na kwake mtarejeshwa.

23. Je, niishike miungu mingine badala yake? kama Mwenyeezi Mungu akipenda kunidhuru, uombezi wao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.

24. Kwa hakika ndipo nitakuwamo katika upotovu ulio wazi.

25. Bila shaka nimemwamini Mola wenu, basi nisikilizeni.

26. Ikasemwa: Ingia Peponi. Akasema: Laiti watu wangu wangejua.

27. Jinsi Mola wangu alivyonisamehe na akanijaalia miongoni mwa walioheshimiwa.

28. Na hatukuwateremshia watu wake jeshi kutoka mbinguni baada yake, wala hatukuwa wateremshao.

29. Haukuwa ila ukelele mmoja tu, na mara wakawa waliozimika.

30. Ni sikitiko kwa waja, hakuwafikia Mtume yeyote ila walikuwa  wanamfanyia mzaha.

31. Je, hawaoni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao, hakika wao hawarejei kwao?

32. Na hapana (atakayebaki) ila wote watahudhurishwa mbele yetu.

33. Na alama kwa ajili yao ni ardhi iliyokufa, tunaifufua na tukatoa ndani yake nafaka nayo wakaila.

34. Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu na kupitisha chemchem ndani yake.

35. Ili wale katika matunda yake, na haikuvifanya mikono yao, je, hawashukuru?

36. Ametukuka aliyeumba dume na jike katika (vitu) vyote katika vile ivioteshavyo ardhi, na katika, nafsi zao, na katika vile wasivyovijua.

37. Na usiku ni alama kwao, toka humo tunauvuta mchana mara wao wamo gizani.

38. Na jua linapita kuendea kituoni pake hicho ni kipimo cha Mwenye nguvu, Mwenye kujua.

39. Na mwezi tumeupimia vituo mpaka ukarudia kuwa kama kole la mtende kuukuu.

40. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana na vyote vinaogelea katika njia.

41. Na ni alama kwao kuwa tulichukua kizazi chao katika majahazi yaliyo shehenewa.

42. Na tukawaumbia mfano wake ambavyo wanavipanda.

43. Na kama tungetaka tungewagharikisha, wala wasingeokolewa.

44. Ha kwa rehema zitokazo kwetu na kuwanufaisha kwa muda kidogo.

45. Na wanapoambiwa: Ogopeni yaliyoko mbele yenu na yaliyoko nyuma yenu mpate kurehemewa.

46. Na haiwafikii dalili yoyote katika dalili za Mola wao ila huwa wenye kuipuuza.

47. Na wanapoambiwa: Toeni katika yale aliyokupeni Mwenyeezi Mungu, wale waliokufuru huwaambia walioamini: Je, tumlishe ambaye Mwenyeezi Mungu akipenda atamlisha? Nyinyi hammo ila katika upotovu dhahiri.

48. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini ikiwa mnasema kweli?

49. Hawangojei ila mlio mmoja utakaowashika nao watakuwa katika hali ya kugombana.

50. Na hawataweza kuusia wala hawatarejea kwa watu wao.

51. Na itapigwa baragumu ndipo watatoka makaburini kwenda mbiombio kwa Mola wao.

52. Watasema: Ole wetu! nani ametufufua malaloni petu? Haya ndiyo aliyoahidi Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, na Mitume walisema kweli.

53. Haitakuwa ila mlio mmoja ndipo wote wataletwa mbele yetu.

54.Basi leo nafsi haitadhulumiwa chochote wala hamtalipwa ila yale mliyokuwa mkitenda.

55. Hakika watu wa Peponi leo wamo katika shughuli wakifurahi.

56. Wao na wake zao katika vivuli wakiegemea juu ya viti vya fahari.

57. Yatakuwamo matunda kwa ajili yao, na watapata watakavyovitaka.

58. Amani, ndio neno litokalo kwa Mola Mwenye kurehemu.

59. Na jitengeni leo enyi waovu.

60. Je. sikukuagizeni enyi wanadamu! msimwabudu shetani, hakika yeye ni adui aliye dhahiri kwenu.

61. Na kwamba mniabudu Mimi, hii ndio njia iliyonyooka.

62, Na bila shaka amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu Je, hamkuwa mkifikiri?

63. Hii ndiyo Jahannam mliyokuwa mkiahidiwa.

64. Leo ingieni kwa sababu mlikuwa mkikufuru.

65. Siku hiyo tutapiga muhuri juu ya vinywa vyao, na mikono yao tatuzungumza, na miguu yao itatoa ushahidi kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.

66. Na kama tungependa tungeyapofua macho yao, wakawa wanaiwania njia, lakini wangeionaje?

67. Na kama tungetaka tungewaharibu majumbani mwao, basi wasingeweza kwenda wala kurudia.

68. Na tunayempa umri (mrefu) tunampindisha katika umbo, basi je, hawafahamu?

69. Wala hatukumfundisha shairi, wala haimpasi, huo sio ila ni ukumbusho na Qur'an ibainishayo.

70. Ili amuonye aliye hai na ihakikike kauli juu ya makafiri.

71. Je, hawaoni kuwa tumewaumbia katika vile ilivyovifanya mikono yetu, wanyama nao wanawamiliki?

72. Na tumewatiishia (wanyama) hao basi baadhi yao wanawapanda na wengine wao wanawala.

73. Na katika hao wanapata manufaa na vinywaji, basi je, hawashukuru?

74. Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyeezi Mungu wapate kusaidiwa.

75. (Lakini) hawawezi kuwasaidia, nalo ni jeshi lao litakaloletwa.

76. Basi isikuhuzunishe kauli yao bila shaka sisi tunajua wanayoyaficha na wanayoyatangaza.

77. Je, Mwanadamu hatambui kuwa tumemuumba kwa tone la manii? Lakini amekuwa mgomvi dhahiri.

78. Na akatupigia mfano na kusahau umbo lake, akasema: Nani atakayeihuisha mifupa na hali imesagika?

79. Sema; Ataihuisha Aliyeiumba mara ya kwanza, naye ni Mjuzi wa kila (namna ya) kuumba.

80. Ambaye amekufanyieni moto katika mti mbichi, ndipo nanyi kwa (mti) huo mkauwasha.

81. Je, aliyeziumba mbingu na ardhi hana uwezo wa kuumba mfano wao? Naam, naye ni Muumbaji Mkuu, Mjuzi.

82. Hakika amri yake anapotaka chochote hukiambia: Kuwa, na kinakuwa.

83. Basi atukuzwe yeye ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu, na kwake mtarejea.