Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili, na tatu tatu na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
2. Rehema anayoifungua Mwenyeezi Mungu kwa watu, hakuna wa kuizuia, na aizuiayo hakuna wa kuipeleka isipokuwa yeye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
3. Enyi watu! kumbukeni neema za Mwenyeezi Mungu zilizoko juu yenu, Je, yuko muumba mwingine asiyekuwa Mwenyeezi Mungu anayekupeni riziki kutoka mbinguni na ardhini? Hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, basi wapi mnakopinduliwa?
4. Na kama wanakukadhibisha, basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyeezi Mungu.
5. Enyi watu! bila shaka ahadi ya Mwenyeezi Mungu, ni haki, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala mdanganyaji asiwadanganye juu ya Mwenyeezi Mungu.
6. Kwa hakika shetani ni adui yenu, basi mfanyeni adui, analiita kundi lake ili liwe katika watu wa Moto uwakao.
7. Waliokufuru itakuwa kwao adhabu kali na wale walioamini na wakatenda mema, wao watapata msamaha na malipo makubwa.
8. Je, Yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake na akaliona kuwa jema, bila shaka Mwenyeczi Mungu humpoteza anayetaka na humuongoza anayetaka. Kwa hiyo roho yako isitoke kwa majonzi juu yao kwani Mwenyeezi Mungu anajua yale wanayoyafanya.
9. Na Mwenyeezi Mungu ndiye anayetuma pepo ziyatimue mawingu nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, na kwa hayo tukaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, hivyo ndivyo ulivyo ufufuo.
10. Anayetaka heshima, basi heshima yote ni ya Mwenyeezi Mungu tu, kwake hupanda maneno mazuri, na kitendo kizuri hukipandisha. Na wale wanaofanya hila ya maovu, hao watapata adhabu kali, na hila yao ndiyo itakayoangamia.
11. Na Mwenyeezi Mungu amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai ila kwa elimu yake (Mwenyeezi Mungu) Na mwenye kupewa umri hapewi umri (zaidi) wala hapunguziwi umri wake ila yamo Kitabuni, bila shaka hayo ni rahisi kwa Mwenyeezi Mungu.
12. Na bahari mbili haziwi sawa: Hii ni tamu yenye ladha, knywaji chake kinateremka uzuri, na hii (nyingine) ni chumvi yenye uchungu ila katika zote mnakula nyama mbichi na mnatoa mapambo mnayoyavaa na ndani yake unaziona jahazi zikikata (maji) ili mpate fadhili yake na mpate kushukuru.
13. Huingiza usiku katika mchana na huingiza mchana katika usiku na amevitiisha jua na mwezi, vyote vinapita mpaka muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyeezi Mungu, Mola wenu, Mwenye ufalme na wale mnaowaabudu kinyume chake, wao hawamiliki hata utando wa kokwa ya tende!
14. Kama mkiwaomba (masanamu hao) hawasikii maombi yenu, na kama wakisikia hawatakujibuni, na siku ya Kiyama watakataa shirki yenu, wala hatakuambia (yoyote) kama (Mwenyeezi Mungu) Mwenye khabari.
15.Enyi watu! nyinyi ndiyo wenye haja kwa Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
16. Kama akitaka atawaondoeni na ataleta viumbe wapya.
17. Na jambo hili si gumu kwa Mwenyeezi Mungu.
18. Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwengine, na kama aliye elemewa na mzigo akimwita (mwingine) mzigo wake hautachukuliwa hata kidogo ingawa yeye ni jamaa. Hakika unawaonya wale tu wanaomuogopa Mola wao kwa siri na wanasimamisha swala. Na anayejitakasa basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake, na marudio ni kwa Mwenyeezi Mungu.
19. Na kipofu na mwenye macho hawawi sawa.
20. Wala giza na nuru.
21. Wala kivuli na joto.
22. Wala hawawi sawa wazima na wafu kwa hakika Mwenyeezi Mungu humsikilizisha amtakaye, nawe huwezi kuwasikilizisha waliomo makaburini.
23. Wewe siye ila ni Muonyaji tu.
24. Bila shaka sisi tumekutuma kwa haki ili ubashiri na uonye, na hakuna taifa lolote ila alipita humo Muonyaji.
25. Na kama wanakukadhibisha, basi walikwisha kadhibisha wale wa kabla yao, Mitume wao waliwafikia kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na kwa Kitabu chenye nuru.
26. Kisha niliwakamata wale waliokufuru, basi kuchukia kwangu kulikuwaje.
27. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu ameteremsha maji mawinguni, na kwa hayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na (mingine) myeusi sana.
28. Na katika watu na wanyama wanaotambaa na wanyama (wengine) pia rangi zao ni mbali mbali. Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyeezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale tu wenye ujuzi, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwingi wa kusamehe.
29. Kwa hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyeezi Mungu wanasimamisha swala, na katika yale tuliyowapa wanatoa kwa siri na kwa dhahiri, wanatumai biashara isiyoangamia.
30. Ili awape malipo yao sawa sawa na kuwazidishia fadhili zake, hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye shukrani.
31. Na Kitabu tulichokufunulia ndicho haki kinasadikisha yaliyokuwa kabla yake. Bila shaka Mwenyeezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye khabari, Mwenye kuona.
32. Kisha tumewapa Kitabu wale tuliowachagua miongoni mwa waja wetu. Basi yuko miongoni mwao anayejidhulumu, na yuko miongoni mwao anayeshika njia ya katikati, na yuko miongoni mwao anayepita mbele katika mema kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, hiyo ndiyo fadhili kubwa.
33. Mabustani ya milele watayaingia humo watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na mavazi yao humo yatakuwa hariri.
34. Na watasema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu aliyetuondolea huzuni, kwa hakika Mola wetu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye shukrani.
35. Ambaye kwa fadhili zake ametuweka katika nyumba ya kukaa, humo haitugusi taabu wala humo hautugusi mchoko.
36. Na wale waliokufuru watakuwa na Moto wa Jahannam, hawatahukumiwa wapate kufa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyomlipa kila asiye na shukrani.
37. Na humo watapiga makelele: Mola wetu! tutoe (Motoni) tutafanva vitendo vizuri visivyokuwa vile tulivyokuwa tukifanya. Je, hatukukupeni umri (mwingi) akumbuke mwenye kukumbuka, na alikufikieni Muonyaji, basi onjeni, na hakuna msaidizi kwa ajili ya madhalimu.
38. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbingu na ardhi, bila shaka yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
39. Yeye ndiye aliyekufanyeni makhalifa katika ardhi. na anayekufuru, basi kufru yake ni juu yake, na kufru za makafiri haziwazidishii mbele ya Mola wao ila chuki, wala kufru za makafiri haziwazidishii ila hasara.
40. Sema: Mmewaona washirika wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu? Nionyesheni ni sehemu ipi ya ardhi waliyoiumba au wanayo shirika katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na dalili wazi wazi? Lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu.
41. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu huzuia mbingu na ardhi zisiondoke, na kama zikiondoka hakuna yeyote wa kuzizuia baada yake. Bila shaka yeye ni Mpole, Mwingi wa kusamehe.
42. Na waliapa kwa Mwenyeezi Mungu kiapo chao kilicho kikubwa; Akiwafikia Muonyaji bila shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipowafikia Muonyaji basi hakuwa zidishia ila chuki.
43. Kwa ajili ya kutakabari katika ardhi, na kufanya vitimbi vibaya, na vitimbi vibaya havimteremkii ila yule aliye vifanya. Basi hawangoji ila desturi (ya Mwenyeezi Mungu) iliyokuwa kwa watu wa zamani. Lakini hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyeezi Mungu, wala hutakuta mageuko katika kawaida ya Mwenyeezi Mungu.
44. Je, hawakusafiri katika ardhi na kuona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliotangulia hali walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao? Na hakuna kitu kiwezacho kumshinda Mwenyeezi Mungu mbinguni wala ardhini bila shaka yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uwezo.
45. Na kama Mwenyeezi Mungu angeliwaadhibu watu kwa sababu ya yale waliyoyachuma, asingeliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini yeye anawaakhirisha mpaka muda maalumu, basi itakapowafikia ajali yao, hapo bila shaka Mwenyeezi Mungu anawajua vyema waja wake.