Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kiirehemu.
1. Alif Lam Myim
2. Uteremsho wa Kitabu kisicho shaka ndani yake, umetoka kwa Mola wa walimwengu.
3. Je, wanasema amekitunga mwenyewe? Bali hicho ni haki itokayo kwa Mola wako ili uwaonyeshe watu wasiofikiwa na Muonyaji kabla yako, huenda wataongoka.
4. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika nyakati sita, kisha ukakamilika (uumbaji wake) katika Arshi. Nyinyi hamna mlinzi wala muombezi isipokuwa yeye tu, je, hamfikiri?
5. Hutengenezajambo toka mbinguni mpaka ardhini, kisha linapanda kwake siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu mnayo tumia katika kuhesabu.
6. Huyo ndiye ajuaye mambo ya ghaibu na ya dhahiri, Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
7. Ambaye ametengeneza umbo la kila kitu, na akaanzisha umbo la mwanadamu kwa udongo.
8. Na akakifanya kizazi chake kwa mbegu ya maji yaliyo hafifu.
9. Kisha akamtengeneza na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona na nyoyo (za kufahamu) ni kidogo tu mnayoyashukuru.
10. Nao husema: Je, tutakapotoweka ardhini, kwa vyovyote tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao hawakubali kuwa watakutana na Mola wao.
11. Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu, kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu.
12. Na ungeliwaona waovu wakiinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao (na kusema): Mola wetu! tumekwisha ona na tumekwisha sikia. basi turudishe, tutafanya vitendo vizuri, hakika (sasa) tumethibitisha.
13. Na tungelitaka, tungempa kila mtu muongozo wake, lakini imehakiki kauli iliyotoka kwangu. Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wote hawa majinni na watu.
14. Basi onjeni (adhabu) kwa sababu ya kusahau mkutano wa siku yenu hii hakika sisi tutakusahauni, na onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
15. Hakika wanaoziamini Aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa kwazo huanguka kusujudu na humtukuza Mola wao kwa kutaja sifa zake, nao hawatakabari.
16. Huachana mbavu zao kutoka vitandani, kumuomba Mola wao kwa khofu na tumaini, na hutoa katika yale tuliyowapa.
17. Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
18. Je Muumini anaweza kuwa sawa na yule aliye fasiqi? Hawawi sawa.
19. Ama wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, basi watakuwa nazo Busatani za makazi (mazuri) ndio pakufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda.
20. Lakini wale waliofanya uovu, basi makazi yao ni Motoni, watakapotaka kutoka humo watarudishwa humo na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkikadhibisha.
21. Na kwa hakika tutawaonjesha adhabu hafifu kabla ya adhabu kubwa, labda watarejea.
22. Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa Aya za Mola wake kisha huzikataa? Hakika sisi ni wenye kuchukua kisasi kwa waovu.
23. Na bila shaka tulimpa Musa Kitabu, basi usiwe na shaka kwa kukutana na Mwenyeezi Mungu, na tukakifanya muongozo kwa wana wa Israeli.
24. Na tukawafanva miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu waliposubiri, na walikuwa wakiziyakinisha Aya zetu.
25. Hakika Mola wako ndiye atakayehukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.
26. Je, hayawaongozi (kuona) ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao vilivyokuwa vikitembea katika maskani yao? Bila shaka katika hayo mna mazingatio (makubwa) je, hawasikii?
27. Je, hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kame kisha kwa (maji) hayo tunaiotesha mimea wanayokula wanyama wao, na wao wenyewe, je, hawaoni?
28. Na wanasema: Ushindi huu utatokea lini ikiwa mnasema kweli?
29. Sema: Siku ya ushindi wale waliokufuru imani yao haitawafaa, wala hawatapewa muda wa kungoja.
30. Basi jiepushe nao, na ngoja, kwa hakika wao (pia) wanangoja.