Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Twaa Syn Mym.
2. Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.
3. Tunakusomea khabari za Musa na Firaun kwa haki kwa ajili ya watu wanaoamini.
4. Hakika Firaun alitakabari katika ardhi na akawafanya watu wa huko (kuwa katika) mkundi makundi, akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na kuwaacha hai wanawake wao, hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu.
5. Na tunataka kuwafanyia hisani wale waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya viongozi na kuwafanya warithi.
6. Na kuwapa nguvu ardhini, na kuwaonyesha katika hao Firaun na Hamana na majeshi yao yale waliyokuwa wakiyaogopa.
7. Na tulimfunulia mama ya Musa kuwa mnyonyeshe, na utakapomkhofia, basi mtie mtoni na usiogope wala usihuzunike, kwa hakika sisi tutamrudisha kwako, na tutamfanya miongoni mwa Mitume.
8. Na wakamuokota watu wa Firaun ili awe adui kwao na huzuni. Kwa hakika Firaun na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.
9. Na mkewe Firaun akasema: Kiburudisho cha macho kwangu na kwako, msimuue, huenda atatunufaisha, au tumpange kuwa mtoto hali hawatambui.
10. Na moyo wa mama ya Musa ukawa mtupu, alikuwa karibu kudhihirisha (siri) kama tusingeliuimarisha moyo wake ili awe miongoni mwa wenye kuamini.
11. Na akamwambia dada yake (Musa): Mfuate, Basi yeye akamwangalia kwa mbali bila wao kujua.
12. Na tukamharamishia wanyonyeshaji tangu mwanzo, na (dada yake) akasema: Je, nikuonyesheni watu wa nyumba watakaomlea kwa ajili yenu, na pia watakuwa wema kwake?
13. Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike, na ajue kwamba ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui.
14. Na (Musa) alipofikia baleghe yake na akastawi, tulimpa hukumu na elimu na hivyo ndivyo tunavyowalipa wenye kufanya mema.
15. Na aliingia mjini wakati wenyeji wake walikuwa katika ghafla, na akakuta humo watu wawili wakipigana, huyu katika jamaa zake na huyu katika adui zake. Ndipo Musa akampiga ngumi, na akammaliza akasema: Hiki ni kitendo cha shetani bila shaka yeye ni adui, mpotezaji wa dhahiri.
16. Akasema: Mola wangu! bila shaka nimedhulumu nafsi yangu! basi nisamehe, naye akamsamehe, kwa hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
Akasema: Mola wangu! kwa sababu umenineemesha basi sitakuwa kabisa msaidizi wa waovu.
18. Na alikwenda mjini asubuhi akiogopa, akiangalia, mara yule mtu aliyeomba msaada kwake jana, akamwita; Musa akamwambia Bila shaka wewe ni mkosaji dhahiri.
19. Basi alipotaka kumkamata yeye aliye adui yao wote wawili, kasema: Ewe Musa! Je, unataka kuniua kama ulivyomuua mtu jana? wewe hutaki ila kuwa jabari katika nchi wala hutaki kuwa miongoni mwa watu wazuri.
20. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio, akasema: Ewe Musa! hakika wakubwa wanashauriana kukuua, basi ondoka, kwa hakika mimi ni miongoni mwa wakutakiao mema.
21. Basi (Musa) akatoka akiogopa, akiangalia huku na huku, akasema: Mola wangu! niokoe katika watu madhalimu.
22. Na alipoelekea upande wa Madyan, akasema: Hakika Mola wangu ataniongoza njia iliyo sawa.
23. Na alipoyafikia maji ya Madyan akakuta kundi la watu wakinywesha (wanyama wao) na akakuta nyuma yao wanawake wawili wakizuia (wanyama wao) akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi mpaka wachungaji warudishe (wanyama wao) na baba yetu ni mzee sana.
24. Basi (Musa) akawanyweshea, kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu! hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayoniteremshia.
25. Basi akamjia mmoja katika wale wawili akitembea kwa haya, akasema: Baba yangu anakuita ili akulipe malipo ya kutunyweshea. Basi alipomfikia na akamsimulia kisa chote, akasema: Usiogope, umekwisha okoka katika watu madhalimu.
26. Akasema mmoja ya wale wawili: Ewe baba! Muajiri, hakika mbora uwezaye kumuajiri ni ambaye mwenye nguvu, mwaminifu.
27. Akasema mimi nataka nikuoze mmojawapo katika binti zangu hawa kwa kunitumikia miaka minane, na kama ukitimiza kumi ni hiari yako, lakini mimi sitaki kukutaabisha utanikuta inshaa-Allah miongoni mwa watu wema.
28. Akasema (Musa: Mapatano) hayo yamekwisha kuwa baina yangu na baina yako, muda mmoja wapo nitakaomaliza, basi nisidhulumiwe, na Mwenyeezi Mungu ni Mlinzi juu ya hayo tunayoyasema.
29. Basi Musa alipotimiza muda, akasafiri pamoja na watu wake, akaona moto upande wa mlima: Akawaambia watu wake: Ngojeni, hakika nimeona moto labda nitakuleteeni khabari za huko au kijinga cha moto ili muote.
30. Basi alipoufikia aliitwa kutoka upande wa kulia wa bonde, katika kiwanja kilichobarikiwa, kutoka mtini, kwamba: Ewe Musa! hakika Mimi ndiye Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.
31.Na kwamba: Tupa fimbo yako. Basi alipoiona ikichezacheza kama nyoka akageuka kurudi nyuma, na hakurudi. Ewe Musa! Njoo mbele na usiogope, kwani wewe ni miongoni mwa waliosalimika.
32. Ingiza mkono wako kifuani mwako utatoka mweupe pasipo ubaya, na vutia mkono wako kwako kutuliza khofu, basi hizo zitakuwa dalili mbili zitokazo kwa Mola wako kwa ajili ya Firaun na wakuu wake, bila shaka wao ni watu waasi.
33. (Musa) akasema: Mola wangu! hakika mimi nilimuua mtu kati yao, kwa hiyo naogopa wataniua.
34. Na ndugu yangu Harun ni fasaha zaidi kuliko mimi kwa usemi, basi mtume pamoja nami awe msaidizi, kunisaidia, hakika mimi naogopa kuwa watanikadhibisha.
35. (Mwenyeezi Mungu) akasema: Karibuni tutautia nguvu mkono wako kwa ndugu yako, na tutakupeni ushindi hata hawatakufikieni, kwa sababu ya Miujiza yetu nyinyi na watakaokufuateni mtashinda.
36. Basi alipowafikia Musa na Miujiza yetu wazi wazi, wakasema: Hayakuwa haya ila ni uchawi uliotungwa, wala hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa zamani.
37. Na Musa akasema: Mola wangu ndiye amjuaye sana yule ajae na muongozo kutoka kwake, na yule atakayekuwa na mwisho wa makazi (mema) hakika madhalimu hawafaulu.
38. Na Firaun akasema; Enyi wakuu! simjui kwa ajili yenu mungu asiye kuwa mimi. Basi ewe Hamana! niwashie moto juu ya udongo, na unijengee mnara ili nimchungulie Mungu wa Musa, na kwa hakika namdhani kuwa ni katika waongo.
39. Na alijivuna yeye na majeshi yake katika nchi pasipo haki, na walidhani kuwa hawatarudishwa kwetu.
40. Basi tukamuadhibu yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini,basi angalia ulikuwaje mwisho wa madhalimu.
41. Na tukawafanya viongozi waitao kwenye moto, na siku ya Kiyama hawatasaidiwa.
42. Na tukawafuatishia laana katika dunia hii; na siku ya Kiyama wao watakuwa miongoni mwa wenye hali mbaya.
43. Na bila shaka tulimpa Musa Kitabu baada ya kuviangamiza vizazi vya kwanza, kiwaangazie watu na kiwe muongozo na rehema, ili wapate kukumbuka.
44. Na hukuwa upande wa magharibi tulipompelekea (Musa) amri wala hukuwa miongoni mwa walioshuhudia.
45. Lakini sisi tuliumba umma nyingi na umri ukawa mrefu juu yao, wala hukuwa mkazi pamoja na watu wa Madyan kuwasomea Aya zetu, lakini sisi tulikuwa tunapeleka (Mitume).
46. Wala hukuwa upande wa mlima tulipomuita (Nabii Musa) lakini (kutumwa kwako) ni rehema ya Mola wako, ili uwaonyeshe watu wasiofikiwa na muonyaji kabla yako, huenda watakumbuka.
47. Na isije ukawafikia msiba kwa yale iliyoyatanguliza mikono yao, kisha waseme, Mola wetu! mbona hukutupelekea Mtume nasi tungefuata Aya zako na tungekuwa miongoni mwa walioamini.
48. Lakini ilipowafikia haki kutoka kwetu, wakasema: Mbona hakupewa kama yale alivopewa Musa? Je, hawakuyakataa yale aliyopewa Musa zamani? walisema: Ni wachawi wawili wanaosaidiana na akasema: Hakika sisi wote tunawakataa.
49. Sema: Basi leteeni kitabu kitokacho kwa Mwenyeezi Mungu ambacho kinamuongozo ulio bora kuliko hivi viwili ili nikifuate, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
50. Lakini kama hawakukujibu, basi jua kuwa wanajifuatia tu matamanio yao na ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayejifuatia matamanio yake pasipo muongozo utokao kwa Mwenyeezi Mungu? Bila shaka Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
51. Na kwa hakika tuliwafululizia maneno ili wapate kukumbuka.
52. Wote tuliowapa Kitabu kabla ya (Qur'an) hii wao wanaiamini.
53. Na wanaposomewa, husema: Tunaiamini, bila shaka hii ni haki itokayo kwa Mola wetu, kwa hakika kabla ya haya tulikuwa wenye kujisalimisha.
54. Hao ndio watakaopewa malipo yao mara mbili kwa kuwa walisubiri, na huondoa ubaya kwa wema, na kutoa katika yale tuliyowapa.
55. Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao na kusema: Sisi tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Amani juu yenu, sisi hatutaki (kujibizana na) wajinga.
56. Kwa hakika wewe huwezi kumuongoza umpendaye, lakini Mwenyeezi Mungu humuongoza amtakaye naye ndiye anaewajua sana waongokao.
57. Na wakasema: Kama tukifuata muongozo pamoja nawe tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je, hatukuwakalisha mahala patakatifu na pa amani, yanakovutiwa matunda ya kila aina kuwa riziki itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui.
58. Na tumeiangamiza miji mingapi iliyojifakharisha juu ya maisha yao! Hayo ni makazi yao yasiyokaliwa baada yao ila kidogo, na sisi tulikuwa warithi.
59. Na Mola wako haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika mji wao mkuu, awasomee Aya zetu: Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wamekuwa madhalimu.
60. Na chochote mlichopewa, basi ni matumizi kwa maisha ya dunia na mapambo yake, lakini kilichoko kwa Mwenyeezi Mungu ni bora na kitabaki, basi je, hamfahamu.
61. Je, yule tuliyemwahidi ahadi nzuri tena atakayoipata anaweza kuwa sawa na yule tuliyemstarehesha kwa starehe ya maisha ya dunia, kisha siku ya Kiyama awe miongoni mwa waliohudhurishwa?
62. Na siku atakapowaita, na atasema wako wapi washirika wangu ambao mlikuwa mkidai?
63. Watasema wale iliyothibiti juu yao kauli: Mola wetu hawa ndio tuliowapoteza, tuliwapoteza kama vile tulivyopotea, tunajiepusha nao mbele yako, hawakuwa wakituabudu sisi.
64. Na itasemwa: Waiteni washirika wenu. Basi wataiona adhabu, laiti wangelikuwa wenye kuongoka.
65. Na siku atakayowaita na atasema: Je, mliwajibu nini Mitume?
66. Basi zitawapotea siku hiyo khabari, nao hawataulizana.
67. Basi ama aliyetubia na akaamini na akafanya vitendo vizuri, ni hakika atakuwa miongoni mwa wenye kufaulu.
68. Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua (amtakaye) kwao hakuna hiari, Mwenyeezi Mungu ameepukana na upungufu, na yuko juu kabisa kuliko wale wawashirikishao (naye).
69. Na Mola wako anayajua yanayoficha vifua vyao na wanayoyadhihirisha.
70. Naye ndiye Mwenyeezi Mungu, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, sifa zote njema mwanzoni na mwishoni ni zake tu. Na hukumu ni yake, nanyi mtarudishwa kwake.
71. Sema: Niambieni, kama Mwenyeezi Mungu akiufanya usiku ukukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyeezi Mungu, atakayewaleteeni mwanga? Basi je, hamsikii?
72. Sema: Niambieni, kama Mwenyeezi Mungu akiufanya mchana ukukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyeezi Mungu atakayekuleteeni usiku mnao starehe humo? Basi je, hamuoni?
73. Na kwa rehema zake amekufanyieni usiku na mchana ili mtulie humo na mtafute fadhili zake na ili mpate kushukuru.
74. Na siku atakayowaita na kusema: Wako wapi washirika wangu ambao mlikuwa mkidai?
75. Na tutatoa katika kila umma shahidi na tutasema: Leteni dalili zenu, ndipo watajuwa kuwa haki iko kwa Mwenyeezi Mungu na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua.
76. Hakika Karuni alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwaasi, na tulimpa khazina ambazo funguo zake ziliwaelemea kundi la watu wenye nguvu. Walipomwambia watu wake: Usijigambe, hakika Mwenyeezi Mungu Hawapendi wanaojigamba.
77. Na utafute makazi ya Akhera kwa yale aliyokupa Mwenyeezi Mungu wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Mwenyeezi Mungu alivyokufanyia wema, wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi, bila shaka Mwenyeezi Mungu hawapendi mafisadi.
78. Akasema: Hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu niliyo nayo. Je, hukujua kwamba Mwenyeezi Mungu ameviangamiza kabla yake vizazi vingi waliokuwa wenye nguvu zaidi kuliko yeye na wenye mkusanyo mwingi zaidi? Na waovu hawataulizwa kwa makosa yao.
79. Basi akawatokea watu wake katika pambo lake, wakasema wale wanaotaka maisha ya dunia: Laiti tungelipata kama alivyopewa Qaruni, hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
80. Na wakasema wale waliopewa elimu Ole wenu! Malipo ya Mwenyeezi Mungu ni mazuri kwa yule anayeamini na kufanya vitendo vizuri, wala hawatapewa isipokuwa wenye kufanya subira.
81. Basi tukamdidimiza yeye (Karuni) na nyumba yake ardhini, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyeezi Mungu. wala hakuwa miongoni mwa wenye kujisaidia.
82. Na wakawa wanasema wale waliotamani cheo chake jana: Alaa kumbe! Mwenyeezi Mungu humzidishia riziki amtakaye miongoni mwa waja wake na hudhikisha (riziki ya anayemtaka) Asingetufanyia hisani Mwenyeezi Mungu bila shaka angetudidimiza. Oh! kweli makafiri hawafaulu.
83. Hivyo nyumba ya Akhera tutawafanyia wale wasiotaka kujitukuza katika ardhi wala (kufanya) ufisadi, na mwisho (mwema) ni kwa wacha Mungu.
84. Atakayefanya wema atapata bora kuliko huo, na atakayefanya ubaya, basi hawatalipwa wale wafanyao ubaya ila yale waliyokuwa wakiyafanya.
85. Hakika yule aliyekulazimisha (kufuata) Qur'an lazima atakurudisha mahala pa kurejea. Sema Mola wangu ndiye amjuaye sana ajaye na muongozo na yule aliyomo katika upotovu ulio dhahiri.
86. Nawe hukuwa unatumai kuwa utapelekewa Kitabu lakini ni rehema ya Mola wako, basi usiwe msaidizi wa makafiri.
87. Wala wasikuzuie katika Aya za Mwenyeezi Mungu baada ya kufunuliwa kwako, na uwaite (watu) kwa Mola wako, wala usiwe miongoni mwa washirikina.
88. Wala usimuombe pamoja na Mwenyeezi Mungu mungu mwingine, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, kila kitu kitaangamia isipokuwa yeye, hukumu iko kwake, na kwake mtarejeshwa.