24 SUURATUN NUUR

Sura hii imeteremshwa Madina, ina Aya 64

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ni sura tumeiteremsha, na tumeilazimisha, na tumeteremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.

2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, basi mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia. Wala isiwashikeni kwa ajili yao huruma katika hukumu ya Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi mnamwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini.

3. Mwanamume mzinifu haoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina, na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina, na hayo yameharamishwa kwa waumini.

4. Na wale wanaowasingizia wanawake waaminifu kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni mijeledi themanini na msiwakubalie ushahidi wao kabisa na hao ndio mafasiki.

5. Isipokuwa wale wenye kutubu baada ya hayo na wakasahihisha, basi bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.

6. Na wale wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudulia mara nne kwa kiapo cha Mwenyeezi Mungu, kwamba: Bila shaka yeye ni katika wasema kweli.

7. Na mara ya tano (aape) kwamba: Laana ya Mwenyeezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.

8. Na (mkewe) itamuondokea adhabu kwa kutoa ushahidi mara nne kwa kiapo cha Mwenyeezi Mungu, kwamba: Huyu (mume) ni miongoni mwa waongo.

9. Na mara ya tano (aape) kwamba: Ghadhabu ya Mwenyeezi Mungu iwe juu yake kama (mumewe) ni miongoni mwa wakweli.

10. Na lau isingelikuwa fadhili ya Mwenyeezi Mungu juu yenu na rehema yake (mngetaabika) na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mpokeaji wa toba, Mwenye hekima.

11. Hakika wale walioleta uongo ni kundi miongoni mwenu. Msiufikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu, kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi, na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa.[1]

12. Mbona mlipousikia, wanaume waumini na wanawake waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhahiri?

13. Mbona hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyokuwa hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Mwenyeezi Mungu ndio waongo.

14. Na kama isingelikuwa juu yenu fadhili ya Mwenyeezi Mungu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.

15. Mlipoupokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mliufikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyeezi Mungu ni kubwa.

16. Na mbona mlipousikia hamkusema: Haitupasi kuzungumza haya, utakatifu ni wako, huu ni uongo mkubwa.

17. Mwenyeezi Mungu anakunasihini, msirudie kabisa mfano wa haya, ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.

18. Na Mwenyeezi Mungu anakubainishieni Aya (zake) na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.

19. Kwa hakika wale wanaopenda uenee uchafu kwa walioamini, watapata adhabu yenye kuumiza katika dunia na Akhera, na Mwenyeezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

20. Na isingelikuwa fadhili ya Mwenyeezi Mungu juu yenu na rehema yake na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu (yangetokea machafuko makubwa).

21. Enyi mlioamini! msifuate nyayo za shetani, na atakayefuata nyayo za shetani, basi hakika yeye huamrisha mambo ya aibu na maovu, na lau kuwa si fadhili za Mwenyeezi Mungu na rehema zake asingelitakasika miongoni mwenu hata mmoja, lakini Mwenyeezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

22. Na wasiape wale wenye utajiri na wenye wasaa (kujizuia) kuwapa walio jamaa na masikini na waliohama katika njia ya Mwenyeezi Mungu, na wasamehe na waachilie, Je, nyinyi hampendi Mwenyeezi Mungu awasamehe? Na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

23. Bila shaka wale wanaowasingizia wanawake wanaojiheshimu, wasiojua (maovu) waumini, wamelaniwa katika dunia na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.

24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao, kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

25. Siku hiyo Mwenyeezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kuwa Mwenyeezi Mungu ndiye Haki iliyo wazi.

26. Wanawake wabaya ni kwa wanaume wabaya, na wanaume wabaya ni kwa wanawake wabaya, na wanawake wema ni kwa wanaume wema na wanaume wema ni kwa wanawake wema, hao wameepushwa na hayo wanayoyasema, wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.

27. Enyi mlioamini! Msiingie nyumba ambazo si nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, na muwatolee salamu waliomo humo, hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.

28. Na kama hamtamkuta humo yeyote, basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini, basi rudini, ni takaso kwenu, na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyatenda.

29. Si vibaya kwenu kuingia majumba yasiyokaliwa mlimo na manufaa yenu na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyadhihirisha na mnayoyaficha.

30. Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyeezi Mungu anazo khabari za yale wanayoyafanya.

31. Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, na wasionyeshe uzuri wao ila kwa' waume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au wanawake wenzao, au wale waliomilikiwa na mikono yao au wafuasi  wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua siri za wanawake. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni nyote kwa Mwenyeezi Mungu enyi wenye kuamini ili mpate kufaulu.[2]

32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wawezao kuowa na kusimamia haki zake katika watumwa wenu na wajakazi wenu, wakiwa mafakiri Mwenyeezi Mungu atawatajirisha katika fadhili zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.[3]

33. Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea mpaka Mwenyeezi Mungu awatajirishe kwa fadhili zake. Na wale wanaotaka kuandikiwa katika wale waliomilikiwa na mikono yenu, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyeezi Mungu aliyokupeni wala msiwashurutishe vijana wenu wa kike kufanya ukahaba kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ili hali wao wanataka kujiheshimu. Na takayewalazimisha, basi hakika Mwenycezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu

34. Na bila shaka tumekuteremshieni Aya zinazoeleza wazi wazi na mifano kutokana na waliotangulia kabla yenu, na mawaidha kwa wacha Mungu.

35. Mwenyeezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi, mfano wa nuru yake ni kama shubaka ndani yake mna taa. Taa ile imo katika tungi, tungi lile ni kama nyota ing'aayo inayowashwa katika mti uliobarikiwa wa mzaituni, si wa mashariki wala magharibi yanakaribia mafuta yake kung'aa ingawa moto haujayagusa, nuru juu ya nuru, Mwenyeezi Mungu humuongoza kwenye nuru yake amtakaye, na Mwenyeezi Mungu hupiga mifano kwa watu, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

36. Katika Nyumba ambazo Mwenyeezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, humtukuza humo asubuhi najioni.[4]

37. Watu ambao haiwashughulishi biashara wala kuuza kunikumbuka Mwenyeezi Mungu, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, wakiogopa siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.

38. Ili Mwenyeezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyafanya, na kuwazidishia katika fadhili zake, na Mwenyeezi Mungu humruzuku amtakaye pasipo hesabu.

39. Na wale waliokufuru vitendo vyao ni kama mazigazi jangwani mwenye kiu huyadhani ni maji hata ayafikiapo hapati chochote, na humkuta Mwenyeezi Mungu hapo, naye humpa hesabu yake sawa sawa, na Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.

40. Au ni kama giza katika bahari yenye maji mengi, inayofunikwa na mawimbi, juu ya mawimbi najuu yake kuna mawingu, giza juu ya giza, anapoutoa mkono wake anakaribia asiuone, na ambaye Mwenyeezi Mungu hakumjaalia nuru, basi huyo hana nuru.

41. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu vinamtukuza vilivyomo mbinguni na ardhini, na ndege kwa kukunjua mbawa zao? kila mmoja amekwisha jua swala yake na namna ya kumtakasa, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yale wanayoyafanya.

42. Na ni wa Mwenyeezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyeezi Mungu tu ndiko marejeo.

43 Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu anayaendesha mawingu, kisha huyagandisha pamoja, kisha huyarundika, na unaona mvua ikitoka katikati yake, naye huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamfikishia amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye, hukaribia mwanga wa umeme wake kupofua macho.

44. Mwenyeezi Mungu hubadilisha usiku na mchana, bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa wenye busara.

45. Na Mwenyeezi Mungu amemuumba kila mnyama kwa maji, wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine wao huenda kwa miguu miwili na wengine wao huenda kwa (miguu) minne, Mwenyeezi Mungu huumba atakayo hakika Mwenyeezi Mungu anao uwezo juu ya kila kitu.

46. Kwa hakika tumeteremsha Aya zinazo bainisha, na Mwenyeezi Mungu humuongoza anayetaka kwenye njia iliyo nyooka.

47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyeezi Mungu na Mtume, na tumetii, kisha hugeuka kundi moja kati yao baada ya hayo, wala hao si wenye kuamini.

48. Na wanapoitwa kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kundi moja miongoni mwao linajitenga.

49. Na kama ikiwa haki ni yao, wanamfikia kwa kutii.

50. Je, wana maradhi katika nyoyo zao, au wanashaka, au wanaogopa kuwa atawadhulumu Mwenyeezi Mungu na Mtume wake? Bali hao ndio madhalimu.

51. Hakika kauli yaWaumini wanapoitwa kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, husema: Tunasikia na tunakubali, na hao ndio wenye kufaulu.

52. Na anayemtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na kumnyenyekea Mwenyeezi Mungu na kumuogopa basi hao ndio watakaofuzu.

53. Na wanaapa kwa Mwenyeezi Mungu ukomo wa kiapo chao, kwamba:

ukiwaamrisha bila shaka wataondoka, sema: Msiape, utiifu unajulikana, hakika Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.

54. Sema: Mtiini Mwenyeezi Mungu na mtiini Mtume, na kama mkikataa, basi aliyolazimishwa yeye ni juu yake, na ni juu yenu mliyolazimishwa nyinyi na kama mkimtii mtaongoka, si vingine juu ya Mtume ila kufikisha (ujumbe wake) wazi wazi.

55. Mwenyeezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, bila shaka atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale wa kabla yao, na lazima atawaimarishia dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wataniabudu, hawatanishirikisha na chochote, na afakayekufuru baada ya hayo, basi hao ndio wenye kuvunja amri.

56. Na simamisheni swala na toeni zaka na mtiini Mtume ili mrehemewe.

57. Msiwadhanie wale waliokufuru kuwa watamshinda (Mwenyeezi Mungu) katika ardhi, na makazi yao ni Moto na marudio (yao) bila shaka ni mabaya.

59. Enyi mlioamini! Wakuombeni ruhusa wale iliyowamiliki mikono yenu, na wale wasiofikia baleghe miongoni mwenu mara tatu: Kabla ya swala ya alfajirii na mnapovua nguo zenu adhuhuri na baada ya swala ya isha, hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya juu yenu wala juu yao baada ya nyakati hizo, mnazungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyo kuelezeni Aya (zake) na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

59. Na watoto watakapo baleghe miongoni mwenu, basi waombe ruhusa kama walivyoomba ruhusa wale wa kabla yao. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyokubainishieni Aya zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

60. Na wanawake wakongwe ambao hawatumaini kuolewa basi si vibaya kwao kufunua nguo zao, bila kuonyesha mapambo. Na kama wakijizuilia (kufunua hizo nguo) ni bora kwao, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

61. Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kilema, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu, kama mkila katika nyumba zenu au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za ndugu zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za a'mi zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za wale mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya juu yenu kama mkila pamoja au mbali mbali. Na mnapoingia katika majumba basi mtoleane salamu, ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyeezi Mungu yenye baraka njema. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyokubainishieni Aya ili mpate kufahamu.

62.  Waumini ni wale tu waliomwamini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, pia wanapokuwa pamoja naye kwa jambo linalohusiana na wote, hawaondoki mpaka wamuombe ruhusa, kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa hao ndio wanaomuamini Mwenyeezi  Mungu na Mtume wake. Na watakapokuomba ruhusa kwa ajili ya baadhi ya kazi zao, basi mruhusu umtakaye miongoni mwao, na uwaombee msamaha kwa Mwenyeezi Mungu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

63. Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyeezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale waondokao kwa utoro wakijificha. Basi wajihadhari wale wanaokaidi amri yake, isije ikawapata balaa au ikawafikia adhabu yenye kuumiza.

64. Sikilizeni! kwa hakika ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Bila shaka anajua mliyo nayo, na siku watakaporudishwa kwake, basi atawaambia waliyoyafanya na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.


[1] Aya 11

TUKIO KUBWA JUU YA MWANA AISHA

Waandishi wa Tarekh wamepokea kuwa: Harith bin Abi Dhirar, kiongozi wa Bani Mustaliq, aliandaa jeshi kwa ajili ya kuuvamia mji wa Madina.

Zilipomfikia khabari hizi Mtume s.a.w akachukua tahadhari ya kulinda nafsi zao na mji wao. Akaweka kikosi tayari kwa kukabili uchokozi wowote kutoka kwa adui. llikuwa mwezi wa Shaaban mwaka wa sita Hijria, Mtume s.a.w akapambana na jeshi la Bani Mustaliq katika eneo la Muraysii.

Jeshi la Waislamu lilipata ushindi mkubwa, ambapo kwa Waislamu alipata shahada (aliuliwa) mtu mmoja tu, ambaye kwa bahati mbaya aliuliwa na Mwislamu mwenzake akidhaniwa ni adui. Kwa upande wa adui, walipigwa na majeshi ya Waislaamu na kutekwa mia mbili akiwamo bibi Juwairiyya binti Harithi bin Abi Dhirar (kiongozi wa Bani Mustaliq) bibi ambaye baadaye aliolewa na Mtume s.a.w kisha mateka hao waliachiliwa huru, na hapo Uislamu ukaenea katika koo ya Bani Mustaliq.

Sasa, Mwana Aisha (mkewe Mtume) anasimulia tukio la If-k kama hivi:

Anasema Aisha: Mtume s.a.w alikuwa akipiga kura kati ya wakeze kila alipotaka kusafiri. Yeyote anayeangukiwa na kura ndiye anayesafiri pamoja naye. Mtume s.a.w alipokwenda Muraysii kupambana na Bani Mustahq mimi nilifuatana naye (baada ya kuangukiwa na kura).

Jeshi la Mtume lilipokuwa likirudi, mimi nilikuwa nimepanda ngamia wangu nikiwa ndani ya Hawdaj (khema dogo linalowekwajuu ya ngamia) Tulipofika mahala mimi nilishuka nikamwacha ngamia njiani, nikaenda faragha kujisaidia, Niliporudi barabarani, nikagundua kuwa kidani hakipo kifuani! Nikarudi haraka kule nilikokuwa, nikakitafuta sikukipata! Huku nyuma, ukapita msafara wakamchukua yule ngamia wangu wakidhani mimi nimo ndani ya Hawdaj.

Mimi nikaendelea kukitafuta kidani changu na baadae nikakipata, nikarudi aliko ngamia wangu, sikumkuta, kwa kuwa usiku ulikuwa mwingi, nikajilaza mahala nikapitiwa na usingizi. Katika majiraya alfajiri Swafwan bin Mua'ttal As'Sulamy akapita, alipokaribia nilipo, akaona kuna binadamu, akanisogelea akanifahamu akasema: Inna lillahi wainna ilayhi raajiu'n. Mimi nikaamka na mara moja nikafunika uso wangu! Akamuweka sawa ngamia wake, akaniambia nipande, nami nikapanda, akanipeleka mpaka Madina. Watu wakazusha uongo dhidi yangu na Swafwan bin Mua'ttal, na aliyejitwika uongo huo ni Abdallah bin Ubayya bin Saluul. Mambo yalipozidi, Mtume s.a.w akaniruhusu niende kwa wazazi wangu.

Nilipomuuliza mama yangu: Watu wanasema nim? Mama akajibu: Mwanangu tulia, mimi nikazidi kulia usiku kucha! Siku moja Mtume akamwita Ali bin Abi Talib na Usama bin Zayd. Hapo ni baada ya mwezi mzima kupita bila ya kushuka wahyi, Mtume s.a.w akawashauri, afanye nini? Usama akasema:

Ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu! wao ni watu wako, na hatuna lolote tulijualo kwao isipokuwa jema tu. Ali yeye akasema: Wanawake ni wengi, na kama utamuuliza kijakazi atakuthibitishia. Mtume akamwita Barira, anasema Aisha: Ali akamsimamia Barira akampiga sana na huku akimwambia: Mhakikishie Mtume. Aisha anasema: akajibu Barira: Wallahi sina lolote nilijualo mimi juu ya Aisha isipokuwa jema tu. Mtume s.a.w akapanda minbari akawaambia Waislamu: Enyi Waislamu! Nani analeta uchochezi kwa watu wa nyumba yangu? Wallahi mimi sijui lolote kwa watu wangu isipokuwa jema tu, wamemzulia mtu jambo ambalo mimi silijui kwake isipokuwa ni la wema tu.

Mwana Aisha anasema: Nilimuona Mtume akitabasamu akisema: Furahi ewe Aisha! Mwenyeezi Mungu amekutakasa, Aisha anasema: Akaniambia mama yangu: Msimamie Mtume nikajibu: Wallahi simsimamii, na wala simshukuru isipokuwa Mwenyeezi Mungu tu. Mwenyeezi Mungu aliteremsha Aya kumi za kumtakasa Mwana Aisha kwa uongo aliosingiziwa.

Taz: Tarekhut Tabari: J.2  Uk. 265-268

Tarekh Ibn Athir: J.2  Uk. 132-135

MusnadAhmad: J.6 Uk. 221-223

Tafsir Ayaatil Ahkaam: J.2 Uk. 119-124

Fat-hul Baari:  J.8 Uk. 360-309

Sharh Sahih Muslim:  J.17 Uk.03-112

UPEMBUZI YAKINIFU:

Upembuzi wetu katika tukio hili utaangalia mambo matano:

(a) Wahyi ulikatika mwezi mzima?

(b) Ali alimshauri Mtume kumwacha Aisha?

(c) Ali alimpiga sana Barira?

(d) Aisha alikataa kumsimamia Mtume?

(e) Aisha alifanya uchafu?

(A) WAHYI ULIKATIKA MWEZI MZIMA?

Je tukio la If-k halikuwa muhimu mbele ya Mwenyeezi Mungu? Kwanini kuzuiwa Wahyi mwezi nizima, katika jambo kubwa namna hii? chukua mfano wa matukio mawili, ambayo ukiyaangalia utayaona ni kama hili, uone msimamo wa Qur'an kisha ujiulize, ilikuwaje katika tukio la Mwana Aisha ukazuiwa Wahyi kwa muda wa mwezi mzima? kwa maslahi, au kwa izara gani?

Matukio mawili hayo tunayaleta hapa uyasome kwa makini kisha ulinganishe

matukio hayo na hili la Mwana Aisha:

a) Kisa cha Hilal bin Umayya alipomtukana mkewe, Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya pale pale: "Na wale wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Mwenyeezi Mungu, kwamba:

Bila shaka yeye ni mmoja wa wanaosema kweli." 24:6.

Taz: Tafsirul Qurtubi: J.12 Uk. 183 Addurrul Manthur: J.5  Uk. 44

b) Kisa cha Kawlah bint Tha'alaba, alipoambiwa na mumewe: "Wewe kwangu mimi ni kama mgongo wa mama yangu" Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya pale pale: Mwenyeezi Mungu amekwisha sikia usemi wa mwanamke yule aliyejadiliana nawe kwa sababu ya mumewe, na akashtaki mbele ya Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu anayasikia mazungumzo yenu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. Wale miongoni mwenu wawaitao wake zao mama, wao si mama zao, hawakuwa mama zao isipokuwa wale waliowazaa. Na kwa hakika wao wanasema maneno mabaya na ya uongo na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye Msamaha, Mwenye maghfira. Na wale wawaitao wake zao mama, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema (wakataka kuwarejea wake zao) basi wampe mtumwa uhuru kabla ya kugusana, hayo ndiyo mnayoagizwa, na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyatenda.” 58:1-3.

Taz: Tafsirul Qurtubi: J.17 Uk. 270-271

Addurrul Manthur: J.6  Uk. 265

(B) ALI ALIMSHAURI MTUME KUMWACHA AISHA?

Ali bin Abi Talib ni, Wasii na Khalifa wa Mtume s.a.w na ni mmoja wa Ahlul kisaa. Ikiwa, kama asemavyo Aisha itathibiti, kuwa Mtume s.a.w alipomtaka ushauri akajibu: "Wanawake ni wengi" basi, Imam Ali (a.s) atakuwa amempa Mtume ushauri wenye hekima na uadilifu ndani yake. Hapa ninataka kukumbusha neno la Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w aliposema juu va Imam Ali (a.s) kuwa: "Ali yu pamoja na Qur'an, na Qur'an i pamoja na Ali, havitaachana (Ali na Qur'an) mpaka vitakaponifikia katika Hawdh."

Taz: Almustadrak: J..3  Uk. 134

 Tarekhul Khulafai: Uk. 162

 Yanabiul Mawaddah: Uk. 339

Sasa, tuangalie Mwenyeezi Mungu amesema nini juu ya MwanaAisha: "Kama Mtasaidiana (Aisha na Hafsa) dhidi yake (Mtume kumuudhi, Mwenyeezi Mungu atakuwa pamoja naye dhidi yenu kuwalaani) kwa sababu, Mwenyeezi Mungu ni kipenzi chake, na Jibril na Waislamu wema, na zaidi ya hayo, Malaika (wote pia) watasaidia. Akikupeni talaka (Mtume) Mola wake atampa badala yenu, wake wengine walio bora kuliko nyinyi." 66:4.

C) ALI ALIMPIGA SANA BARIRA?

Mwana Aisha anasema: "Ali akamsimamia Barira akampiga sana."

MAJIBU: Tarekh inaonyesha kuwa: "Barira hakuwapo katika tukio hilo.

Taz: Zadul Maa'dy:  J.3  Uk. 268

Ashia'tul baitin Nabawy: J.2  Uk. 107

D) AISHA ALIKATAA KUMSIMAMIA MTUME?

Mwana Aisha anasema: "Akaniambia mama yangu, msimamie Mtume, nikajibu: Wallahi simsimamii, na wala simshukuru isipokuwa Mwenyeezi Mungu tu."

MAJIBU:

Qadhia iliyopo hapa, si Aisha kukataa kumsimamia Mtume, bali Aisha amekataa amri ya mama yake hili ndilo jipya kwa Waislamu.

Kwa sababu: Jambo kama kumkosea adabu Mtume, au kuwa na mashaka ya utume wake, hayo mara kadhaa yametokea kwa bibi huyu juu ya Mtume s.a.w.

Ta.z: Ahaadithu Ummil Muuminiin Aisha ukurasa 27-57

E) AISHA ALIFANYA UCHAFU?

Amesema Mtume s.a.w:

"Ewe Aisha! Kwamba, imenifikia (khabari) kuhusu wewe mambo fulani fulani, basi ikiwa hukuyatenda, Mwenyeezi Mungu atakutakasa. Na kama umefanya kosa lolote, basi muombe msamaha Mwenyeezi Mungu na urejee kwake."

Taz: Fat'hul Baary:  J.8  Uk. 308

Sharh Sahih Muslim:  J.17 Uk. 111

Naam, Mwenyeezi Mungu ameteremsha Aya kumi (11-20) katika suratun Nuur za kumtakasa Mwana Aisha kwa uongo aliozuliwa.

Kwa hali yoyote, lisilokuwa na shaka katika qadhia hii ni kwamba: Wake za Mtume wote ni wema kwa upande wa sharaf (heshima) lakini kwa upande wa itikadi (ukafiri mathalan) hilo linawezekana: "Mwenyeezi Mungu amepiga mfano wa waliokufuru, kwa mkewe Nuhu na mkewe Luti, hawa wawili walikuwa chini ya waja wema wawili miongoni mwa waja wetu. Basi wakawafanyia khiyana, (waume zao) hawakuwasaidia chochote mbele ya Mwenyeezi Mungu, na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoia nawenye kuingia." 66:10.

[2] Aya 31

 VAZI LA MWANAMKE WA KIISLAM

Iliposemwa: "Isipokuwa unaodhihirika" Maana yake ni: Uso, mikono na miguu.

Taz: Al miizan fyitafsiril Qur'an:  J.15 Uk. 121

Majmaul Bayan fyitafsiril Our'an: J. 4 Uk. 138

Alburhan fyitafsiril Qur'an:  J.3  Uk. 130

Tafsirus Saafi: J.3  Uk. 430

"Waangushe shungi zao juu ya vifua vyao." Na wala haikusemwa: "Juu ya nyuso zao". Mwenyeezi Mungu (s.w) amewaamrisha wanawake waumini kuangusha shungi juu ya vifua, hii ndiyo NASSI ya kuwajibisha kufunika kifua, na hii ni NASSI pia ya kuruhusu kuacha uso wazi Mwenyeezi Mungu anasema: "Baada ya hawa si halali kwako (kuoa) wanawake (wengine) wala si (halali) kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza. 33:52.

Iliposemwa: "Uzuri wao ukikupendeza" Je, macho yako yatavutiwa na nini kwake, ikiwa mwanamke huyo ameviringishwa maguo uso mzima. Amesema Mtume s.a.w kuwa: "Mtu yeyote atakayemuona mwanamke akampendeza, basi aende kwa mkewe, kwani mwanamke (huyo) anayo kama yale aliyonayo (mkewe).”

Taz: Fatawa Muaswira:  J.2  Uk. 321

SahihMuslim: J.2  Uk. 1021

Aliulizwa Imam Ja'afar As-Swaadiq (a.s) "Maeneo gani ambayo mwanamume ni halali kuyaona kwa mwanamke ambaye si maharimu? Akajibu: Ni uso, mikono na miguu."

Taz: Al-Waafy: J.22 Uk. 818-821

Imepokewa kwa Qays bin Shimas, anasema: "Alikuja kwa Mtume s.a.w Mwanamke fulani aitwae Mama Khallaad akiwa amevaa niqaab (amefunika uso) akamuulizia mwanawe ambae aliuliwa: Mmoja wa maswahaba akamwambia: Umekuja kumuuliza mwanao na hali umevaa niqaab?!

Taz: Awnul Maabud: J.7  Uk.119

Fatawa Muasira: J.2  Uk. 325

Maswahaba walishangaa kuona mwanamke amevaa niqaab!! Kama kuvaa niqaab nijambo lililoagizwa na Uislaamu, bila shaka maswahaba wangelijua hilo, kwa hiyo, maswahaba wasingeshangaa kuona mwanamke wa kiislamu aliyevaa niqaab.

Jambo ambalo ni muhimu kulikariri hapa ni kwamba: Mwenyeezi Mungu (s.w) amewaamrisha wanawake waumini kufunika mwili mzima isipokuwa uso, mikono na miguu.

[3] Aya32

Tamko la Kiarabu tulilolifasiri: 'Wawezao kuowa na kusimamia haki zake" ni: "AS-SAALIHIIN" na tamko hili maana yake ni: "Watu wenye matendo mema”.

Lakini, AS-SAALIH hapa si, kwa matendo mema tu, bali awezae kuowa na kusimamia haki za ndoa.

Taz: Almizan fyi tafsiril Qur'an: J.15 Uk. 122

Tafsirus Saafi: 1.3 Uk. 4.32

Tafsirul Maraghy: J.18     Uk. 103

[4] Aya 36

Imepokewa kwa Anas bin Malik anasema: Aliposoma Mtume Aya "Fyi buyuutin adhinallahu antur fa'a" yaani, 'Katika nyumba ambazo Mwenyeezi Mungu ameamrisha zitukuzwe."

Mtu mmoja akamsimamia akasema: Ni nyumba gani hizi ewe mtume wa Mwenyeezi Mungu? Mtume akajibu: Ni nyumba za Mitume, mara Abubakr akamsimamia akasema: Ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu! nyumba hii ni miongoni mwa hizo? akaonyesha nyumba ya Ali na Fatima (a.s) Mtume akajibu: Ndiyo, ni miongoni mwa nyumba zenye kutukuzwa.

Taz: Alburhan fyitafsiri Qur'an: J.3  Uk. 138

Majmaul bayan fyitafsiril Qur'an: J.4  Uk. 144

Almizan fyitafsiril Our'an:  J.15  Uk. 153

Taisirus saafi: J.3  Uk. 437

Addurrul Manthur: I.5  Uk. 91

Ruuhul Maany: J.18  Uk. 255