Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Imewakaribia watu hesabu yao nao wamo katika mghafala, wanapuuza.
2. Hayawafikii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao ila huyasikiliza na hali wanafanya mchezo.
3. Nyoyo zao zimeghafilika, na wananong'onezana kwa siri wale waliodhulumu. Ni nani huyu isipokuwa ni binadamu tu kama nyinyi, je, mnafika penye uchawi na hali nyinyi mnaona?
4. Alisema: Mola wangu huyajua yanayosemwa mbinguni na ardhini, naye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
5. Lakini wanasema; (hizo ni) Ndoto zilizovurugika, bali ameyabuni mwenyewe, kwa vile yeye ni mshairi, basi atuletee Muujiza kama walivyotumwa (Mitume) wa kwanza.
6. Haukuamini kabla yao mji wowote tuliuangamiza je, wao wataamini?
7. Na hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowaletea Wahyi, basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.
8. Wala hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kukaa milele.
9. Kisha tukawasadikishia ahadi na tukawaokoa pamoja na wale tuliowataka na tukawaangamiza wanaopita kiasi.
10. Bila shaka tumekuteremshieni Kitabu ambacho mna mawaidha kwenu, je, hamfahamu?
11. Na miji mingapi tuliiharibu iliyokuwa ikidhulumu na tukawaumba baadae watu wengine?
12. Basi walipohisi adhabu yetu mara walianza kuikimbia.
13. Msikimbie, na rudini katika yale mliyojistareheshea na katika maskani zenu ili mkaulizwe.
14. Wakasema: ole wetu! hakika tulikuwa madhalimu.
15. Na kukaendelea kulia kwao (huko) mpaka tukawafanya kama
waliofyekwa; wakazimika.
16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake kwa mchezo.
17. Kama tungelitaka kufanya mchezo, hakika tungeufanya Sisi wenyewe, hatukuwa wenye kufanya (mchezo).
18. Bali tunaitupa haki juu ya uwongo ikauvunja na mara (uongo) ukatoweka, na ole wenu kwa ajili ya mnayonena.
19. Na ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, na walio mbele yake hawajivuni kwa kumuabudu wala hawachoki.
20. Wanamtukuza usiku na mchana hawafanyi uvivu.
21. Au wamepata waungu katika ardhi wafufuao?
22. Lau kama wangelikuwako humo (mbinguni na ardhini) waungu wengine isipokuwa Mwenyeezi Mungu. Lazima zingeharibika. Na ametakasika Mwenyeezi Mungu, Mola wa arshi, yu mbali na yale wanayoyasifu.
23. Haulizwi anayoyafanya na wao wataulizwa.
24. Au wameshika badala yake miungu? Sema leteni dalili zenu, huu ni ukuinbusho wa wale walio pamoja nami na ukumbusho wa wale wa kabla yangu, lakini wengi wao hawajui ukweli, kwa hiyo wanapuuza.
25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna aabudiwaye ila Mimi tu basi niabuduni.
26. Na wanasema: Mwingi wa rehema amejifanyia mtoto, ametakasika Mwenyeezi Mungu bali (Malaika) ni waja walio tukuzwa.
27. Hawamtangulii kwa neno, nao hufanya kwa amri yake.
28. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao, na hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia, nao kwa kumuogopa yeye wananyenyekea.
29. Na atakayesema miongoni mwao: Hakika mimi ni mungu badala yake, basi huyo tutamlipa Jahannam hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.
30. Je, hawakuona wale waliokufuru kwamba mbingu na ardhi vilikua vimeambatana kisha tukaviambua, na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai basi je, hawaamini?
3 1. Na tukaweka katika ardhi milima ili isiwayumbishe, na tukaweka humo bara bara wazi wazi ili wapate kuongoka.
32. Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyohifadhiwa, nao wanazipuuza dalili zake.
33. Na yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote vinaogelea katika anga.
34. Nasi, hatukumuumba mwanadamu yeyote wa kabla yako aishi milele basi kama ukifa wao wataishi milele?
35. Kila nafsi itaonja mauti, na tunakujaribuni kwa shari na kheri kuwa mtihani na kwetu mtarejeshwa.
36. Na wanapokuona wale waliokufuru hawakufanyii chochote ila mzaha (wakisema) Je, huyu ndiye anayewataja waungu wenu? Na hao ndio wakataao mawaidha ya Mwingi wa rehema.
37. Mwanadamu ameumbwa na haraka, nitakuonyesheni Miujiza yangu, kwa hiyo msinihimize.
38. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini kama mnasema kweli.
39. Lau wangejua wale waliokufuru wakati ambao hawatauzuia Moto katika nyuso zao wala katika migongo yao wala hawatasaidiwa.
40. Bali utawafikia kwa ghafla na utawahangaisha, kisha hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula.
41. Na bila shaka walifanyiwa kejeli Mitume kabla yako, kwa hiyo yakawazinga wale waliofanya kejeli miongoni mwao yale waliyokuwa wakiyafanyia kejeli.
42. Sema: Nani anakulindeni usiku na mchana na Mwenyeezi Mungu? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao.
43. Je, wanao miungu wanaowalinda badala yetu? Hawawezi kujisaidia wenyewe wala hawatahifadhiwa nasi.
44. Bali tuliwastarehesha hawa (makafiri) na baba zao mpaka umri wao ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni kuwa tunaifikia ardhi tukiipunguza mipaka yake? Basi je, wao ni wenye kushinda?
45. Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi tu, na viziwi hawasikii mwito wanapo onywa.
46. Na kama ingeliwagusa dharuba (moja) ya adhabu ya Mola wako, bila shaka wangelisema: ole wetu! hakika tulikuwa madhalimu.
47. Nasi tutaweka mizani ya uadilifu siku ya Kiyama, na nafsi yoyote haitadhulumiwa hata kidogo, na kama kukiwa na uzito wa chembe ya khardali tutaileta, nasi tunatosha kuwa wenye kuhesabu.
48. Na kwa hakika tuliwapa Musa na Harun kipambanuzi na mwanga na mawaidha, kwa wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).
49. Ambao wanamuogopa Mola wao hata faraghani nao (pia) hukiogopa Kiyama.
50. Na haya ni makumbusho yaliyobarikiwa tuliyoyateremsha, je nyinyi mtayakataa?
51. Na hakika tulimpa Ibrahimu muongozo wake zamani na tulikuwa tukimjua.
52. Alipomwambia Baba yake na watu wake: Ni nini masanamu haya mnayotegemea?
53. Wakasema: Tuliwakuta baba zetu wakiyaabudu.
54. Akasema: Bila shaka nyinyi na baba zenu mlikuwa katika upotovu dhahiri.
55. Wakasema: Je, umetufikia kwa haki au umo miongoni mwa wachezaji?
56. Akasema: Bali Mola wenu ndiye Mola wa mbingu na ardhi ambaye aliziumba, nami juu ya hayo ni miongoni mwa wenye kushuhudia.
57. Na Wallahi lazima nitayafanyia vitimbi masanamu yenu baada ya kunipa mgongo.
58. Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao, ili wao walirudie.
59. Wakasema: Nani amefanya hivi kwa miungu yetu? Hakika huyo ni miongoni mwa madhalimu.
60. Wakasema: Tulimsikia kijana mmoja akiwataja anaitwa Ibrahimu.
61. Wakasema: Basi mleteni mbele ya macho ya watu, ili wamshuhudie.
62. Wakasema: Je, wewe umewafanya hivi waungu wetu ewe Ibrahimu?
6.3. Akasema: Bali ametanya mkubwa wao huyu kwa hiyo waulizeni kama wanaweza kutamka.
64. Bali wakajirudi na nafsi zao na wakasema: Hakika nyinyi ni madhalimu.
65. Kisha wakarejea kwenye upotovu wao (wakasema:) hakika wamekwisha jua kuwa hawa hawasemi.
66. Akasema: Je, mnaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu yasiyokufaeni chochote wala kukudhuruni?
67. Aibu yenu na hivyo mnavyoviabudu badala ya Mwenyeezi Mungu je, hamfikiri.
68. Wakasema: Mchomeni na muiokoe miungu yenu ikiwa nyinyi ni wenye kutenda.
69. Tukasema: Ewe moto! uwe baridi na salama juu ya Ibrahimu.
70. Na wakamtakia ubaya lakini tukawafanya kuwa wenye kupata khasara.
71. Na tulimuokoa yeye na Luti katika ardhi tuliyoibarikia kwa ajili ya walimwengu wote.
72. Naye (Ibrahimu) tukampa Isihaka na Yaakub mjukuu, na wote tukawafanya kuwa wema.
73. Na tukawafanya kuwa Maimam wanaoongoza kwa amri yetu, na tukawapelekea Wahyi kuzifanya kheri, na kusimamisha swala na kutoa zaka na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
74. Na Luti tukampa hukumu na elimu na tukamuokoa katika mji uliokuwa ukifanya maovu, hakika wao walikuvva watu wabaya wavunjao amri.
75. Na tukamwingiza katika rehema zetu, kwani yeye alikuwa miongoni mwa watanyao mema.
76. Na Nuhu alipoita zamani, nasi tukamwitikia, na tukamuokoa yeye na watu wake katika shida kubwa.
77. Na tukamsaidia yeye juu ya watu waliozikadhibisha Aya zetu, hakika wao walikuwa watu wabaya, basi tukawagharikisha wote.
78. Na Daudi na Suleimani, walipokata hukumu juu ya shamba, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku nasi kwa hukumu yao tulikuwa mashahidi.
79. Hivyo tukamfahamisha Suleiman, na kila mmoja tukampa hukumu na elimu, na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase (Mwenyeezi Mungu) na Sisi tulikuwa ni wenye kufanya.
80. Na tukamfundisha ( Daudi) matengenezo ya mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika mapigano yenu, je, mtakuwa wenye kushukuru.
81. Na kwa Suleiman (tukautiisha) upepo wa nguvu uendao kwa amri yake kwenye ardhi ambayo tumeibarikia nasi ndio tunaokijua kila kitu.
82. Na katika mashetani (walikuwako) wenye kumpigia mbizi na kufanya kazi nyingine, nasi tulikuwa walinzi wao.
83. Na Ayubu, alipomwita Mola wake ya kwamba imenigusa dhara nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.
84. Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara aliyokuwa nayo na tukampa watu wake na mfano wa pamoja nao ni rehema kutoka kwetu, na ukumbusho kwa wafanya ibada.
85. Na Ismail na Idrisa na Dhulkifli wote walikuwa miongoni mwa wanaosubiri.
86. Na tukawaingiza katika rehema zetu, hakika wao walikuwa katika watu wema.
87. Na Dhun Nun (Yunus) alipoondoka hali amechukia, na akadhani kuwa hatutakuwa na uwezo juu yake basi aliita katika giza kwamba: Hakuna aabudiwaye isipokuwa wewe tu, umetakasika, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.
88. Basi tukampokelea na tukamuokoa katika huzuni, na hivyo ndivyo tunavyowaokoa wenye kuamini.
89. Na Zakaria alipomwita Mola wake: Mola wangu! usiniache peke yangu na wewe ndiye mbora wa wanaorithi.
90. Basi tukampokelea na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe, hakika wao walikuwa wepesi kufanya wema na wakituomba kwa shauku na khofu, nao walikuwa wakitunyenyekea.
91. Na (Mwanamke) yule aliyejilinda tupu yake, na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa Muujiza kwa walimwengu.
92. Kwa hakika huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu, kwa hiyo niabuduni.
93. Nao wakalivunja jambo lao baina yao, wote watarudia kwetu.
94. Na atakayefanya vitendo vizuri hali ya kuwa Muumini basi haitakataliwa juhudi yake, na hakika Sisi tutamwandikia.
95. Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.
96. Hata watakapofunguliwa Yaajuj naMaaju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.
97. Na itafika ile ahadi ya kweli, ndipo yatakodoka macho ya wale waliokufuru (wakisema) Ole wetu! bila shaka tulikuwa katika mghafala na (jambo) hili tulikuwa madhalimu.
98. Hakika nyinyi ni wale mnaoabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.
99. Lau hawa wangelikuwa miungu wasingeliingia humo (Jahannam) na wote watakaa humo milele.
100. Wamo humo watapiga kelele, nao humo hawatasikia.
101. Hakika wale ambao wema wetu ulitangulia kufika kwao, hao ndio watakaowekwa mbali nayo.
102. Hawatausikia mvumo wake, nao watakaa milele katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.
103. Hakitawahuzunisha kitisho kikubwa, na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia) hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.
104. Siku tutakayoikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za maandiko, kama tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena, ni ahadi iliyo juu yetu, bila shaka sisi ni wenye kufanya.
105. Na hakika tuliandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa: Ardhi hii) watairithi waja wangu walio wema.
106. Hakika katika haya mna ujumbe kwa watu wafanyao ibada.
107. Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.
108. Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu, Je, nyinyi ni wenye kusilimu?
109. Na kama wakikataa, basi waambie; nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali yale mliyoahidiwa.
110. Hakika yeye anajua kauli iliyo dhahiri na anajua mnayoyaficha.
111. Wala sijui pengine huu ni mtihani kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
112. Akasema: Molawangu! hukumu kwa haki, na Molawetu ndiye Mwenye rehema, aombwaye msaada juu ya hayo mnayoyasema.