SUURA IBRAHIM

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 52.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

1. Alif Lam Ra. (Hiki ni) Kitabu tumekiteremsha kwako ili uwatoe watu katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe katika njia ya yule Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.

2. Mwenyeezi Mungu ambaye ni vyake peke yake vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Na adhabu itawathibitikia makafiri adhabu iliyo kali.

3. Wale wanaopenda maisha ya dunia kuliko Akhera, na kuzuilia watu njia ya Mwenyeezi Mungu, na wanataka kuipotosha, hao wamo katika upotovu ulio mbali (na haki).

4. Na hatukumpeleka Mtume yeyote isipokuwa kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia, kisha Mwenyeezi Mungu humpoteza anayetaka na humuongoza anayetaka, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

5. Na bila shaka tulimpeleka Musa pamoja na Miujiza yetu, tukamwambia watoe watu wako katika giza kuwapeleka kwenye nuru, na uwakumbushe siku za Mwenyeezi Mungu. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

6. Na (kumbuka) aliposema Musa kwa watu wake, kumbukeni neema ya Mwenyeezi Mungu iliyo juu yenu, alipokuokoeni kwa watu wa Firaun. waliokupeni adhabu mbaya, na wakawachinja watoto wenu wanaume wakawaacha hai watoto wenu wanawake, Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unaotoka kwa Mola wenu.

7. Na (kumbukeni) alipotangaza Mola wenu, kama mkishukuru bila shaka nitakuzidishieni, na kama mkikufuru, hakika adhabu yangu ni kali sana.

8. Na Musa akasema: Kama mtakufuru nyinyi na waliomo ardhini wote, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Mwenye kusifiwa.

9. Je, hazikukufikeni khabari za wale wa kabla yenu? watu wa Nuhu naAdi na Thamudi na wale wa baada yao ambao hakuna awajuaye ila Mwenyeezi Mungu. Waliwafikia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, na wakaserna hakika sisi tunayakataa mliyotumwa  nayo, na sisi tunayo shaka ihangaishayo kwa hayo mnayotuitia.

10. Mitume wao wakasema: Je, mnamfanyia Mwenyeezi Mungu shaka, Muumba wa mbingu na ardhi? yeye anakuiteni akusameheni dhambi zenu na akupeni muhula mpaka muda uliowekwa. Wakasema, Hamkuwa nyinyi ila ni watu kama sisi mnataka kutuzuilia waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu, basi tuleteeni hoja iliyo wazi.

11. Mitume wao wakawaambia; Sisi hatukuwa ila ni watu kama nyinyi, lakini Mwenyeezi Mungu humfanyia ihsani anayetaka katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kukuleteeni hoja (hizo) isipokuwa kwa ruhusa ya Mwenyeezi Mungu. Najuu ya Mwenyeezi Mungu wategemee wenye kuamini.

12. Na tuna nini tusimtegemee Mwenyeezi Mungu na hali ametuonyesha njia zetu? Na lazima tutayavumilia mnayotuudhi, basi kwa Mwenyeezi Mungu wategemee wenye kutegemea.

13. Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume wao: Lazima tutakutoeni katika nchi yetu au bila shaka mtarudi katika mila yetu. Basi Mola wao akawaletea Wahyi (kuwa) Lazima tutawaangamiza madhalimu.

14. Na kwa hakika tutakukalisheni katika nchi baada yao, hiyo ni kwa yule aliyeogopa cheo changu na akaogopa onyo (langu).

15. Na wakaomba ushindi na akashindwa kila jabari adui wa haki.

16. Mbele yake iko Jahannam na atanyweshwa maji yenye usaha.

17. Atayanywa kidogo kidogo wala hataweza kuyameza, na mauti yatamfikia kutoka kila mahala, naye hatakufa, na zaidi ya hayo iko adhabu kali.

18. Mfano wa wale waliomkufuru Mola wao vitendo vyao ni kama majivu yanayopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya kimbunga. Hawawezi kupata chochote katika waliyoyachuma, huo ndio upotovu wa mbali.

19. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki akitaka atakuondoeni na kuleta viumbe wapya.

20. Na hilo kwa Mwenyeezi Mungu si gumu.

21. Na wote watahudhuria kwa Mwenyeezi Mungu ndipo wanyonge watasema kuwaambia wale waliojivuna. Hakika sisi tulikuwa tukikufuateni nyinyi, basi je, nyinyi mnaweza kutuondolea chochote katika adhabu ya Mwenyeezi Mungu? watasema: Angelituongoza Mwnyeezi Mungu bila shaka tungelikuongozeni (lakini sasa) ni mamoja kwetu tusipo subiri au tukisubiri, hatuna pakukimbilia.

22, Na shetani atasema itakapokatwa hukumu. Hakika Mwenyeezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli, nami nilikuahidini, lakini sikukutimizieni. Wala sikuwa na mamlaka juu yenu isipokuwa nilikuiteni nanyi mkaniitika. Basi msinilaumu bali jilaumuni wenyewe, siwezi kukusaidieni, wala nyinyi hamuwezi kunisaidia. Hakika mimi nilikataa kunishirikisha kwenu toka zamani, hakika madhalimu watakuwa na adhabu yenye kuumiza.

23. Na wataingizwa wale walioamini na kufanya vitendo vizuri katika mabustani yapitayo mito chini yake, watakaa humo milele kwa idhini ya Mola wao. Maamkio yao humo yatakuwa: Salaamun.

24. Je, hukuona jinsi Mwenyeezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri (ambao) mzizi wake ni imara na (kila) tawi lake liko juu (sana).

25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake. Na Mwenyeezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.

26. Na mfano wa neno baya ni kama mti mbaya ambao umeng'olewa ardhini hauna imara.

27. Mwenyeezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera na Mwenyeezi Mungu huwapoteza madhalimu, na Mwenyeezi Mungu hufanya apendavyo.

28. Je, hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyeezi Mungu kwa kufru na wakawafikisha watu wao katika nyumba ya maangamizo.

29. (Ambayo ni) Jahannam, wataiingia, na ni mahala pabaya pakukaa.

30. Na wakamfanyia Mwenyeezi Mungu washirika ili kupoteza (watu) katika njia yake. Sema: Jifurahisheni (kidogo) kisha hakika marejeo yenu ni kwenye Moto.

31. Waambie waja wangu walioamini wasimamishe swala na watoe katika vile tulivyo wapa, kwa siri na kwa dhahiri, kabla haijafika siku isiyokuwa na biashara wala urafiki.

32. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na akateremsha maji kutoka mawinguni, na kwa hayo akaotesha matunda kuwa riziki kwa ajili yenu, na akakutiishieni majahazi ili yapite katika bahari kwa amri yake, na akakutiishieni mito.

33. Na akakutiishieni jua na mwezi, vifanyavyo kazi mfululizo, na akakutiishieni usiku na mchana.

34. Na akakupeni kila mlichomuomba na kama mkihesabu neema za Mwenyeezi Mungu, hamtaweza kuzihesabu, hakika mwanadamu ni dhalimu mkubwa asiye shukrani.

35. Na kumbuka aliposema Ibrahimu Mola wangu! ujaalie mji huu uwe wa amani na uniepushe mimi na wanangu tusiabudu masanamu.

36. Mola wangu! Hakika (masanamu) hawa wamepoteza watu wengi, basi aliyenifuata ni wangu mimi na aliyeniasi basi wewe hakika ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

37. Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya kizazi changu katika bonde lisilokuwa na mimea, katika Nyumba yako Takatifu. Mola wetu! ili wasimamishe swala, basi ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.

38. Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyadhihirisha. Na hakuna chochote kinachofichikana kwa Mwenyeezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.

39. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu aliyenipa juu ya uzee (wangu) Ismail na Is'haka, hakika Mola wangu ni Mwenye kusikia sana maombi.

40. Mola wangu! nijaalie niwe msimamishaji swala na kizazi changu (pia) Mola wetu! na upokee maombi yangu.

41. Mola wetu! unisamehe mimi na wazazi wangu na walioamini, siku ya kusimama hesabu.

42. Wala usidhani Mwenyeezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika yeye anawaakhirisha mpaka siku ambayo macho (yao) yatakodoka.

43. Wanakwenda mbio vichwa juu, na macho yao hayapepesi na nyoyo zao tupu.

44. Na uwaonye watu siku ambayo itawafikia adhabu waseme waliodhulumu. Mola wetu! tuakhirishe muda kidogo tutaitikia wito wako na tutawafuata Mitume (Waambie): Je, hamkuwa mmeapa zamani kuwa nyinyi hamtaondolewa?

45. Na mmekaa katika makao ya wale waliodhulumu nafsi zao, na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo wafanya, na tumekuelezeni mifano (yote).

46. Na kwa hakika wamekwisha fanya vitimbi vyao na vitimbi vyao viko kwa Mwenyeezi Mungu, wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.

47. Basi usimdhanie Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kuadhibu.

48. Siku ardhi itabadilishwa kuwa ardhi nyingine, na mbingu (pia) nao watahudhuria mbele ya Mwenyeezi Mungu, Mmoja Mwenye nguvu.

49. Na utawaona wakosefu siku hiyo wamefungwa katika minyororo.

50. Kanzu zao zitakuwa na lami, na Moto utazifunika nyuso zao.

51. Ili Mwenyeezi Mungu ailipe kila nafsi yale iliyoyachuma, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.

52.Hili ni Tangazo liwafikie watu (wote) liwaonye, na wapate kujua yeye ni Mwenyeezi Mungu Mmoja tu, na ili wenye akili wakumbuke.