1. (Hili ni) tangazo la kujitoa katika dhima, litokalo kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.
2. Basi tembeeni katika nchi miezi minne, najueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyeezi Mungu, na kwamba Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye kuwahizi makafiri.
3. Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, kwa watu siku ya Hija kubwa kwamba Mwenyeezi Mungu yu mbali na washirikina na (pia) Mtume wake (yu mbali nao) Basi kama mkitubu ndiyo kheri kwenu, na kama mkikataa basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyeezi Mungu. Na wapashe khabari waliokufuru kwa adhabu iumizayo.
4. Isipokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao, hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wanaomuogopa.
5. Na miezi mitukufu itakapopita basi waueni washirikina popote muwakutapo, na wakamateni na wazungukeni, na wakalieni katika kila njia.
Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi waachilieni, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Na kama mmoja wa washirikina akikuomba ulinzi, basi mlinde mpaka asikie maneno ya Mwenyeezi Mungu, kisha mfikishe mahala pake pa amani hayo ni kwa sababu ya kuwa wao ni watu wasiojua.
7. Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyeezi Mungu na mbele ya Mtume wake isipokuwa wale mlioahidiana nao mbele ya Msikiti Mtukufu, basi madamu wanakunyokeeni, nanyi pia wanyokeeni hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wanaomuogopa.
8. Vipi, wakikushindeni hawatazami kwenu udugu wala ahadi. Wanakufurahisheni kwa vinywa vyao hali nyoyo zao zinakataa, na wengi wao ni waasi.
9. Wanaziuza Aya za Mwenyeezi Mungu kwa thamani ndogo na wanazuilia watu njia yake (Mwenyeezi Mungu) hakika ni mabaya waliyo kuwa wakifanya.
10. Hawatazami kwa muumini udugu wala ahadi, na hao ndio warukao mipaka.
11. Na kama wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi ni ndugu zenu katika dini. Na tunazieleza Aya kwa watu wanaojua.
12. Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi waueni viongozi wa ukafiri kwani viapo vyao havina maana ili wapate kujizuia.
13. Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakafunga nia ya kumfukuza Mtume, nao ndio waliokuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyeezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope, ikiwa nyinyi mmeamini.
14. Piganeni nao, Mwenyeezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awahizi na akunusuruni juu yao, na wavipoze vifua vya Waumini.
15. Na aondoe ghadhabu ya nyoyo zao, na Mwenyeezi Mungu humkubalia toba ya amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima.
16. Je, mnadhani kuwa mtaachwa na hali Mwenyeezi Mungu hakuwabainisha wale waliopigania dini miongoni mwenu wala hawakumfanya rafiki wa moyo isipokuwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na Waumini? na Mwenyeezi Mungu anazo habari za mnayofanya.
17. Washirikina hawawezi kuimarisha Misikiti ya Mwenyeezi Mungu hali wanajishuhudia kwa ukafiri. Hao ndio vitendo vyao vimeharibika, na watakaa katika Moto milele.
18. Anayeimarisha Misikiti ya Mwenyeezi Mungu ni yule tu anayemwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na kusimamisha swala na kutoa zaka na hawamuogopi yeyote ila Mwenyeezi Mungu, basi hao huenda wakawa miongoni mwa walio ongoka.
19. Je, mnafanya kuanywesha mahujaji na kuuamirisha Msikiti Mtukufu ni sawa na (kazi ya) yule aliyemwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwishi na wakapigania dini ya Mwenyeezi Mungu? Hawawi sawa mele ya Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu mashalimu.
20. Wale walio amini na wakahama na wakapigania dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zao na kwa nafsi zao wana cheo kikubwa mbele ya Mwenyeezi Mungu na hao ndio watakao tengenekewa.
21. Mola wao anawapa khabari njema za rehema zitokazo kwake, na radhi na Bustani ambazo humo watapata neema zitakazodumu.
22. Watakaa humo milele, hakika Mwenyeezi Mungu kwake kuna malipo makubwa.
23. Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa marafiki ikiwa wanapenda ukafiri kuliko Uislaam. na miongoni mwenu atakaye wafanya rafiki, basi hao ndio madhalimu.
24. Sema: Kama baba zenu na watoto wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa -zenu na mali mliyoyachuma na biashara mnazo ogopa kuharibikiwa, na majumba mnayoyapenda ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na kupigania dini yake, basi ngojeni mpaka Mwenyeezi Mungu alete amri yake, na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu maasi.
25. Bila shaka Mwenyeezi Mungu amekusaidieni katika mapigano mengi na siku ya hunayni, 'ambapo wingi wenu ulipokufurahisheni, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkakimbia mkirudi nyuma.
26. Kisha Mwenyeezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale waliokufuru, na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
27. Kisha baada ya hayo Mwenyeezi Mungu atawasamehe awatakao, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
28. Enyi mlioamini hakika washirikina ni najisi kwa hiyo wasiukaribie Msikiti Mtukufu baada ya mwaka wao huu.Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyeezi Mungu atakutajirisheni kwa fadhila zake akipenda. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima.
29. Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyeezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi alivyovihararnisha Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa wale waliopewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.
30. Na Mayahudi wanasema: Uzeiri ni mwana wa Mwenyeezi Mungu na Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mwenyeezi Mungu, hayo ndiyo wasemayo kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani Mwenyeezi Mungu awaangamize, wanageuzwa namna gani!
31. Wamewafanya makasisi wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyeezi Mungu na Masihi mwana wa Mariam, hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mwenyeezi Mungu Mmoja, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, ametakasika na yale wanayo mshirikisha nayo.
32. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyeezi Mungu kwa vinywa vyao, lakini Mwenyeezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wanachukia.
33. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa muongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote, ingawa washirikina watachukia.
34. Enyi mlio amini! hakika wengi katika makasisi na watawa wanakula mali ya watu kwa batili na kuwazuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu. Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyeezi Mungu, basi wape habari za adhabu iumizayo.
35. Siku (mali yao) itakapotiwa joto ndani ya Moto wa Jahannam, na kwa hayo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, haya ndiyo mliyojilimbikizia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya.
36. Hakika idadi ya miezi mbele ya Mwenyeezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika elimu ya Mwenyeezi Mungu tangu siku alipoiumba mbingu na ardhi, kati ya hiyo imo mine iliyo mitukufu, hiyo ndiyo hesabu iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu katika hiyo. Na nyote piganeni na washirikina kama wao wote wanavyopigana nanyi, najueni kwamba Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wanaomuogopa.
37. Bila shaka kuakhirisha (miezi mitukufu) ni kuzidi katika kufru k\va hayo hupotezwawalewaliokufuru. Wanauhalalisha (mwezi mtukufu) mwaka mmoja na kuuharamisha mwaka mwingine ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile aliyoiharamisha Mwenyeezi Mungu, hivyo huhalalisha alivyoviharamisha Mwenyeezi Mungu wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao, na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu makafiri.
38. Enyi inlioamini! mmekuwaje mnapoambiwa: Ncndeni (kupigana) katika njia ya Mwenyeezi Mungu mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmekuwa radhi na misha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kwa Akhera ni kidogo tu.
39. Mkikosa kwenda atakuadhibuni kwa adhabu iumizayo, na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru chochote, na Mwenyeezi Mungn ni Muweza juu ya kila kitu.
40. Kama hamtamsaidia, basi Mwenyeezi Mungu amekwisha msaidia (Mtume wake) walipomfukuza wale waliokufuru, naye ni wa katika wawili walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: Usihuzunike, hakika Mwenyeezi Mungu yupo pamoja nasi. Mwenyeezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona, na akafanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyeezi Mungu ndiyo la juu na Mwenyeezi Mungu ndiye anayeshinda Mwenye hekima.
41. Nendeni (vitani) mkiwa wepesi na mkiwa wazito, na piganeni katika dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, hayo ni bora kwenu ikiwa nyinyi mnajua.
42. Kama ingelikuwa faida iliyo karibu na safari fupi, lazima wangeli kufuata, lakini safari ya taabu imekuwa ndefu kwao. Nao wataapa kwa Mwenyeczi Mungu, kama tungeliweza bila shaka tungelitoka pamoja nanyi. Wanaangamiza nafsi zao, na Mwenyeezi Mungu anajua kwa hakika wao ni waongo.
43. Mwenyeezi Mungu amekusamehe, kwanini umewapa ruhusa? (ungengoja) mpaka wanaosema kweli wakupambanukie, na uwajue waongo.
44. Hawatakuomba ruhusa wale wanaomwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, kuwa hawatapigania dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, na Mwenyeezi Mungu anawajua wanaomcha.
45. Hakika wanakuomba ruhusa wale tu wasiomwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya mwisho, na nyoyo zao zina shaka, kwa hiyo wanasitasita katika shaka yao.
46. Na kama wangelitaka kutoka bila shaka wangelijiandalia maandalio, lakini Mwenyeezi Mungu kachukia kutoka kwao. Na kwa hiyo akawazuia na ikasemwa, kaeni pamoja na wakaao.
47. Kama wangelitoka pamoja nanyi wasingelikuzidishieni ila machafuko, na wangekwenda huku na huko baina yenu kukutakieni fitna. Na miongoni mwenu wako wanaowasikiliza, na Mwenyeezi Mungu anawajua madhalimu.
48. Bila shaka zamani walitaka fitna, na wakakupindulia mambo mpaka ikafika haki na kudhihirika amri ya Mwenyeezi Mungu na hali wamechukia.
49. Na miongoni mwao yuko anayesema, niruhusu, wala usinitie katika fitna. Hakika wameanguka katika fitna na hakika Jahannam ndiyo iwazungukayo makafiri.
50. Kama ukikufika wema unawachukiza na kama ukikufika msiba, husema: Hakika tuliangalia zamani mambo yetu, na hugeuka kwenda zao nao wanafurahi.
51. Sema: Halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyeezi Mungu, yeye ni Mola wetu, na Waumini wamtegemee Mwenyeezi Mungu tu.
52. Sema: Nyinyi hamtutazami ila (kupata) moja katika mema mawili. Na sisi tunawatazamieni kwamba Mwenyeezi Mungu akufikishieni adhabu itukayo kwake au kwa mikono yetu. Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.
53. Sema: Toeni (mali yenu) kwa kupenda au kutopenda, haitakubaliwa kwenu, kwani nyinyi ni watu waasi.
54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa sababu walimkataa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, wala hawafiki (kwenye) sala ila kwa vivu, wala hawatoi ila huwa wamechukia.
55. Basi yasikufurahishe mali yao wala watoto wao, hakika Mwenyeezi Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo katika maisha ya dunia, na roho zao zitoke hali ya kuwa makafiri.
56. Na wanaapa kwa (jina) la Mwenyeezi Mungu kwamba wao ni pamoia nanyi, hali wao si pamoja nanyi, bali wao ni watu wanao ogopa.
57. Kama wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahala pa kuingia, lazima wangekimbilia huko haraka.
58. Na miongoni mwao yuko anayekusengenya katika (kugawa kwako) sadaka. Wanapopewa katika hiyo huridhika, na wasipopewa katika hiyo, hapo huwa wanakasirika.
59. Na kama wangeyaridhia yale aliyowapa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na wakasema: Anatutoshea Mwenyeezi Mungu, atatupa Mwenyeezi Mungu katika fadhila zake, na Mtume wake (pia) hakika sisi tunaelekea kwa Mwenyeezi Mungu.
60. Hakika sadaka ni kwa (watu hawa) tu. Mafakiri na masikini, na wanaozitumikia, na wanaotiwa nguvu nyoyo zao, na katika kuwapa uhuru watumwa, na wenye deni, na katika njia ya Mwenyeezi Mungu, na msafiri. Ni faradhi kutoka kwa Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekirna.
61. Na. miongoni mwao wako wanaomuudhi nabii na wanasema: yeye ni sikio: Sema sikio la kheri kwenu, anamwamini Mwenyeezi Mungu na anawaamini waumini, na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyeezi Mungu watakuwa na adhabu iumizayo.
62. Wanakuapieni Mwenyeezi Mungu ili kukuridhisheni, hali Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ana haki zaidi ya kuridhishwa, ikiwa wao ni wenye kuamini.
63. Je, hawajui kwamba anayeshindana na Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, basi yeye atapata Moto wa Jahannam kukaa humo milele, hiyo ndiyo hizaya kubwa.
64. Wanafiki wanaogopa kuteremshiwa sura itakayowatajia (unafiki wao) uliomo katika nyoyo zao. Sema fanyeni mzaha, hakika Mwenyeezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.
65. Na kama ukiwauliza, lazima watasema: Sisi tulikuwa tukidhihaki na kucheza tu. Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyeezi Mungu Aya zake na Mtume wake?
66. Msitoe udhuru, hakika mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu, kama tukilisamehe kundi (moja) miongoni mwenu tutaliadhibu kundi (jingine) kwa sababu wao walikuwa waovu.
67. Wanaume wanafiki na wanawake wanafiki wote ni hali moja, huamrisha yaliyo mabaya na huyakataza yaliyo mazuri, na kuizuilia mikono yao, wamemsahau Mwenyeezi Mungu basi yeye pia amewasahau, hakika wanafiki ndio wavunjao amri.
68. Mwenyeezi Mungu amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri, Moto wa Jahannam kukaa humo milele. Huo unawatosha na Mwenyeezi Mungu amewalaani, nao wana adhabu ya kudumu.
69. Sawa na wale waliokuwa kabla yenu, walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko nyinyi na wenye mali nyingi na watoto. Basi waliifurahia sehemu yao na nyinyi mnaifurahia sehemu yenu kama walivyofurahia sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu, na mkazama katika maovu kama walivyozama wao. Hao ndio vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera, na hao ndio watakaopata khasara.
70. Je, hazikuwafikia khabari za wale waliokuwa kabla yao watu wa Nuhu na A'di na Thamud, na watu wa Ibrahimu na watu wa Madyan, na (watu wa) miji iliyopinduliwa? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi, basi Mwenyeezi Mungu hakuwa Mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
7l. Na Waumini Wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Huamrisha mema na hukataza maovu na hushika swala na hutoa zaka na humtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. hao ndio Mwenyeezi Mungu atawarehemu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
72. Mwenyeezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake Bustani zipitazo mito chini yake kukaa humo milele, na makazi mazuri katika Bustani zenye kudumu, na radhi ya Mwenyeezi Mungu ndiyo kubwa zaidi, huko ndiko kufuzu kukubwa.
73. Ewe Nabii! pigana na makafiri na wanafiki na uwe mgumu kwao, na makazi yao ni Jahannam, hayo ni marejeo mabaya.
74. Wanaapa kwa (jina) la Mwenyeezi Mungu (kwamba) hawakusema, na hakika wamekwisha sema neno la kufru na wakakufuru baada ya Uislam wao, na wakaazimia wasiyoweza kuyafikia. Na hawakuona kosa ila ya kuwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhili zake. Basi kama wakifanya toba, itakuwa kheri kwao, na kama wakikataa Mwenyeezi Mungu atawaadhibu kwa adhabu yenye kuumiza katika dunia na Akhera, na wala hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru.
75. Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyeezi Mungu. Akitupa katika fadhili zake lazima tutatoa sadaka na bila shaka tutakuwa miongoni mwa watendao mema.
76. Lakini alipowapa katika fadhili zake, wakazifanyia ubakhili nawakageuka na huku wakipuuza.
77. Kwa hiyo akawalipa unafiki nyoyoni mwao mpaka siku ya kukutana naye (Mwenyeezi Mungu) kwa sababu ya kumkhalifu Mwenyeezi Mungu ahadi waliyo mwahidi, na kwa sababu walikuwa wanasema uongo.
7 8. Je, hawajui kwamba Mwenyeezi Mungu anajua siri zao na minong'ono yao, na kwamba Mwenyeezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu?
79. Wale wanaowatia aibu Waumini wanaotoa sadaka na wale wasiopata (cha kutoa) ila juhudi yao, basi wanawafanyia mzaha, Mwenyeezi Mungu atawalipa mzaha (wao) nao watapata adhabu yenye kuumiza.
80. Uwaombee msamaha au usiwaombee msamaha hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyeezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu wavunjao amri.
81.Walifurahi walioachwa nyuma kwa sababu ya kubakia kwao nyuma na kumuacha Mturne wa Mwenyeezi Mungu na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyeezi Mungu na wakasema: Msiende (vitani) katika joto. Sema: Moto wa Jahannam unajoto zaidi laiti wangefahamu.
82. Basi wacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
83. Basi Mwenyeezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni mwao, na wakakutaka idhini ya kutoka (kwenda vitani) basi sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami abadan, wala hamtapigana na maadui pamoja nami. Hakika nyinyi mlipenda kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na wabakiao nyuma.
84. Wala usimsalie mmoja wao akifa, wala usisimame kaburini pake. Hakika wao wamemkataa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na wakafa hali ni wenye kuvunja amri.
85. Wala zisikushitue mali zao na watoto wao hakika Mwenyeezi Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo tu katika dunia, na roho zao zitoke hali wao ni makafiri.
86. Na inapoteremshwa sura (isemayo): Muaminini Mwenycezi Mungu na ipiganieni dini pamoja na Mtume wake, wenye wasaa miongoni mwao wanakuomba ruhusa, na husema: Tuache tuwe pamoja na watakaokaa.
87. Wameridhia kuwa pamoja na wanaobakia nyuma, na nyoyo zao zikapigwa muhuri, kwa hiyo hawafahamu.
88. Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye waliipigania (dini) kwa mali zao na nafsi zao, na hao ndio watakaopata kheri, na hao ndio wenye kufaulu.
89. Mwenyeezi Mungu amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, kukaa humo milele, huko ndiko kufuzu kukubwa.
90. Na walikuja wenye udhuru katika mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale waliosema uongo mbele ya Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Itawapata wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.
91. Si kosa juu ya waliodhaifu wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutoa (kubaki nyuma) wanapomsafia nia nzuri Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Hakuna njia (ya kuwalaumu) wanaofanya mema, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamahe, Mwenye kurehemu.
92. Wala (si kosa) juu ya wale waliokufikia ili uwapandishe (juu ya wanyama) ukasema: Sina cha kukupandisheni juu yake, wakarudi hali macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa kupata masurufu.
93. Iko njia yakuwalaumu wale tu wanaokuomba ruhusa hali wao ni matajiri, wamependa kuwa pamoja na wanaobaki nyuma, na Mwenyeezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, kwa hiyo hawajui.
94. Watakutoleeni udhuru mtakaporudi kwao, sema: Msitoe udhuru, hatukuaminini, hakika Mwenyeezi Mungu amekwisha tueleza khabari zenu, na Mwenyeezi Mungu ataviona vitendo vyenu, na Mturne wake (pia) kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri, naye atakuambieni yale mlivokuwa mkiyatenda.
95 Watakuapieni Mwenyeezi Mungu mtakaporudi kwao ili mjitenge nao. Basi jitengeni nao, kwani wao ni najisi, na makazi yao ni Jahannam ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
96. Wanakuapieni ili muwe radhi nao, na kama mkiwaridhia, basi hakika Mwenycezi Mungu hatakuwa radhi na watu wavunjao amri.
97. Mabedui wamezidi sana katika kufru na unafiki, na wameelekea zaidi wasijue mipaka ya yale aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu juu ya Mtume wake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
98. Na katika mabedui yuko anayefikri kuwa anayoyatoa ni gharama ya bure, na anakungojeleeni misiba. Msiba mbaya uko juu yao na Mwenyeezi Mungu ndiye asikiaye, ajuaye.
99. Na katika mabedui yuko anayemwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na anaitakidi kuwa anayoyatoa ndiyo (sababu za) kumkaribia Mwenyeezi Mungu, na za (kupatia) maombezi kwa Mtume, sikilizeni hakika hyo ni ukaribu kwa ajili yao. Mwenyeezi Mungu atawaingiza katika rehema yake, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
100. Na wale waliotangulia wakawa wa kwanza katika Muhajiri na Ansari, na wale waliowafuata kwa mwendo mzuri, Mwenyeezi Mungu amewaridhia, nao (pia) wamemridhia, na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, kukaa humo milele, huko ndiko kufuzu kukubwa.
101. Na katika mabedui wanaokaa pembezoni mwenu kuna wanafiki, na katika wenyeji wa Madina (pia) wamebobea katika unafiki, huwajui, sisi tunawajua tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.
102. Na wengine waliokiri dhambi zao wakachanganya vitendo vizuri na vingine vibaya, huenda Mwenyeezi Mungu akapokea toba zao, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
103. Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwa hizo (sadaka zao) na uwaombee. Hakika kuomba kwako ni utulivu kwao na Mwenyeezi Mungu ndiye Asikiaye, Ajuaye.
104. Je, hawajui kwamba Mwenyeezi Mungu Yeye anapokea toba ya waja wake na kuzipokea sadaka, na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kukubali toba, Mwenye kurehemu.
105. Na waambie: Tendeni Mwenyeezi Mungu atayaona matendo yenu na Mtume wake na Waumini. na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahir, naye atakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.
106. Na (wako) wengine wanaongojea kwa amri ya Mwenyeezi Mungu ama awadhibu au awasamehe, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
107. Na wale (wanafiki) waliojenga msikiti wa (kuleta) udhia na kufru, na kuwafarikisha Waumini, na kuufanya mahala pa kuvizia kwa waliompiga vita Mweenyeezi Mungu na Mtume wake zamani. Na bila shaka wataapa. : Hatukukusudia ila wema, na Mwenyeezi Mungu anashuhudia kwamba wao ni waongo.
108. Usisimame humo kabisa, hakika Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa kumcha Mwenyeezi Mungu tangu siku ya kwanza unastahili zaidi wewe usimame humo. Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa, na Mwenyeezi Mungu anawapenda wanaojitakasa.
109. Je, aliyeweka msingi wa jengo lake kwa kumuogopa Mwenyeezi Mungu na radhi (yake) ni mbora au aliyeweka msingi wa jengo lake juu ya ukingo wa shimo linalomomonyoka udongo wake, ukaanguka pamoja naye katika Moto wa Jahannam? na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
110. Jengo lao walilolijenga litakuwa sababu ya kutia wasi wasi nyoyoni mwao siku zote, isipokuwa nyoyo zao zikatike vipande na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
111. Hakika Mwenyeezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao ili wapate Pepo wanapigana katika njia ya Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo wanaua na wanauawa. Ni ahadi iliyolazimu juu yake katika Taurati na Injili na Qur'an na ni nani aitekelezaye zaidi ahadi yake kuliko Mwenyeezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye, na huko ndiko kufaulu kukubwa.
112. (Hao ndio) wanaotubu, wanaoabudu, wanaotukuza, wanaofunga swaumu, wanaorukuu, wanaosujudu, wanaoamrisha yaliyo mema, wanaokataza yaliyo mabaya na wanaohifadhi mipaka ya Mwenyeezi Mungu, na wape khabari njema Wauniini.
1 13. Haiwi kwa Mtume na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina ijapokuwa ni jamaa, baada ya kuwabainikia kuwa wao ni watu wa (Moto wa) Jahannam.
114. Wala haikuwa Ibrahimu kumuombea msamaha baba yake ila kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipombainikia kwamba yeye ni aduiya Mwenyeezi Mungu alijiepusha naye kwa hakika Ibrahimu alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyeezi Mungu mvumilivu.
115. Na haiwi kwa Mwenyeezi Mungu kuwapoteza watu baada ya kuwa amewaongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika Mwenyeezi Mungu anajua kila kitu.
1 16. Hakika Mwenyeezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi, huhuisha na kufisha. Nanyi hamna Mlinzi wala Msaidizi isipokuwa Mwenyeezi Mungu.
117. Bila shaka Mwenyeezi Mungu amekwisha pokea toba ya Mtume na Muhajiri na Ansari waliomfuata yeye katika saa ya dhiki, wakati ambao nyoyo za kundi moja miongoni mwao zilikuwa karibu kugeuka, kisha akawaelekea. Kwani yeye ni Mpole kwao, Mwenye kurehemu.
118. Na (pia akawaelekea) wale watatu walioachwa nyuma, hata ardhi ikawa finvu juu yao licha ya wasaa wake, na nafsi zao zikadhikika juu yao, na wakadhani kuwa hapana pa kumkimbilia Mwenyeezi Mungu ila kuelekea kwake, kisha akawaelekea ili wapate kutubu, hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Apokeaye toba, Mwenye kurehemu.
119. Enyi mlioamini! mcheni Mwenyeezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli.
120. Haikuwa kwa watu wa Madina na Mabedui wakaao pembeni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyeezi Mungu wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake. Hayo ni kwa sababu haiwafikii kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyeezi Mungu, wala hawakanyagi njia iwachukizayo makafiri, wala hawapati (taabu) yoyote kwa adui, ila huandikiwa kitendo chema, Hakika Mwenyeezi Mungu haharibu malipo ya watendao wema.
121. Wala hawatoi kinachotolewa, kidogo wala kikubwa, wala hawalipiti bonde ila wanaandikiwa, ili Mwenyeezi Mungu awalipe mema ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
122. Wala haiwezekani kwa Waumini kutoka wote, lakini kwa nini halitoki kundi katika kila taifa miongoni mwao kujielimisha vema dini na kuwaonya watu wao watakapowarudia, ili wapate kujihadhari.
123. Enyi mlioamini! piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri na wakute ugumu kwenu, na jueni ya kwamba Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wanaomuogopa.
124. Na inapoteremshwa sura yoyote, basi wako miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu hii imemzidishia imani? basi ama wale walioamini inawazidishia imani, nao wanafurahi.
125. Ama wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao, basi inawazidishia ubaya juu ya ubaya wao, nao wanakufa hali makafiri.
126. Je, hawaoni kwamba wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu wala hawakumbuki.
127. Na inapoteremshwa sura wanatazamana wao kwa wao: je, yuko yeyote anayekuoneni? kisha huondoka. Mwenyeezi Mungu amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu.
128. Bila shaka amekufikieni Mtume kutoka miongoni mwenu, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, kwa Waumini ni Mpole, Mwenye kurehemu.
129. Lakini kama wakikataa, basi waambie: Mwenyeezi Mungu ndiye anitoshaye, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, kwake yeye tu nimetegemea, naye ndiye Mola wa Arshi kuu.