SUURATUL ANFAL

Sura hii imeteremshwa Madina, Aya 75.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Wanakuuliza juu ya mali iliyotekwa. Waambie: Mali iliyotekwa ni ya Mwenyeezi Mungu na Mtume. Basi muogopeni Mwenyeezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.

2. Hakika wenye kuamini ni wale tu ambao anapotajwa Mwenyeezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani, na wakamtegemea Mola wao tu.

3. Ambao wanasimamisha swala na wanatoa katika yale tuliyowapa.

4. Hao ndio wenye kuamini kweli kweli, wao wana vyeo kwa Mola wao na msamaha na riziki bora.

5. Kama alivyokutoa Mola wako katika nyumba yako kwa haki, na hakika kundi moja la walio amini halipendi (utoke).

6. Wakabishana nawe katika haki baada ya kubainika (haki ile) kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti na hali wanaona.

7. Na (Kumbukeni) Mwenyeezi Mungu alipokuahidini moja katika mataifa mawili ya kwamba ni lenu, nanyi mkapenda mpate lile lisilo na nguvu, liwe lenu na Mwenyeezi Mungu anapenda ahakikishe haki kwa maneno yake na aikate mizizi ya makafiri.

8. Ili kuthibitisha haki na kuondoa batili hata kama wakichukia wabaya.

9. (Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni: Kwa hakika Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu moja watakao fuatana mfululizo.

10. Na Mwenyeezi Mungu hakufanya haya ila iwe habari ya furaha na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna ushindi ila utokao kwa Mwenyeezi Mungu tu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

11. (Kumbukeni) alipokuleteeni usingizi uliokuwa (alama ya) salama itokayo kwake, na akakuteremshieni maji mawinguni ili kukutakaseni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa shetani na kuzipa nguvu nyoyo zenu na kuitia imara miguu (yenu).

12. (Kumbukeni) Molawako alipowafunulia Malaika. Hakika mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini, nitatia woga katika nyoyo za makafiri, basi wapigeni juu ya shingo na wakateni kila ncha za vidole (vyao).

13. Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

14. Ndiyo hivyo, basi ionjeni, na bila shaka makafiri wana adhabu ya Moto.

15. Enyi mlioamini! mnapokutana vitani na wale waliokufuru basi msiwageuzie migongo.

16. Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo isipokuwa amegeuka kwa kushambulia au kageuka kwa kuungana na jeshi, basi hakika yeye amerudi na ghadhabu ya Mwenyeezi Mungu, na mahala pake ni Jahannam, ni mahala pabaya pa kurudia.

17. Basi nyinyi hamkuwaua lakini Mwenyeezi Mungu ndiye aliyewaua, na hukutupa wakati ulipotupa, lakini Mwenyeezi Mungu ndiye aliyetupa, ili awape hidaya nzuri wale walioamini itokayo kwake, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

18. Ndiyo hayo, na hakika Mwenyeezi Mungu ndiye adhoofishaye hila za makafiri.

19. Kama mnataka hukumu, basi hukumu imekwisha kufikieni, na kama mkijizuia, basi itakuwa bora kwenu, na kama mtarudia (kupigana nasi) sisi pia tutarudia na jeshi lenu halitakufaeni chochote hata likiwa na watu wengi, na kwa hakika Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wenye kuamini.

20. Enyi mlioamini! mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye na hali mnasikia.

21. Wala msiwe kama wale wasemao: Tumesikia, na kumbe hawasikii

22. Hakika wanyama wabaya zaidi mbele ya Mwenyeezi Mungu ni viziwi (na) mabubu ambao hawafahamu.

23. Na kama Mwenyeezi Mungu angelijua wema wowote kwao, bila shaka angewasikilizisha na kama angeliwasikilizisha hakika wangeligeuka wakipuuza.

24. Enyi mlio amini! mwitikieni Mwenyeezi Mungu na Mtume anapokuiteni kwa yale yatakayokupeni uzima. Najueni kwamba Mwenyeezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba kwake yeye mtakusanywa.

25. Na iogopeni dhabu ambayo haitawapata peke yao wale waliodhulumu nafsi zao miongoni mwenu, na jueni kuwa Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

26. Na (Kumbukeni) mlipokuwa wachache mkionekana wanyonge katika nchi mnaogopa watu wasikunyakueni, lakini akakupeni makao na akakutieni nguvu kwa msaada wake na akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru.

27. Enyi mlioamini! msimfanyie khiyana Mwenyeezi Mungu na Mtume na msikhini amana zenu na hali mnajua.

28. Najueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni mtihani, na kwamba kwa Mwenyeezi Mungu yako malipo makuu.

29. Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyeezi Mungu atawapeni kipambanuzi na atawafutieni makosa yenu na kuwasameheni, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.

30. Na (kumbuka) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe na wakafanya hila na Mwenyeezi Mungu akafanya hila (pia) na Mwenyeezi Mungu ni Mbora wa wafanyao hila.

31. Na wanaposomewa Aya zetu husema: Tumekwishasikia, tungependa bila shaka tungesema kama haya si chochote haya ila ni hadithi tu za watu wa kale.

32. Na (Kumbuka) waliposema (makafiri) Ee Mwenyeezi Mungu! Kama hii ni haki itokayo kwako, basi tupige kwa mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu nyingine iumizayo.

33. Na Mwenyeezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao wala Mwcnyeezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.

34. Na wana udhuru gani ili Mwenyeezi Mungu asiwaadhibu hali wanazuilia (watu) Msikiti Mtakatifu nao hawakuwa walinzi wake? Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wacha Mungu tu, lakini wengi wao hawajui.

35. Na haikuwa ibada yao katika nyumba (Alkaaba) ila mbinja na makofi, basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyo kuwa mkikufuru.

36. Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu, basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam.

37. Ili Mwenyeezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri, na kuwaweka wabaya juu ya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahannam, hao ndio waliokhasirika.

38. Waambie wale waliokufuru; Kama watakoma watasamehewa yaliyopita, na kama wakirudia, basi umekwisha pita mfano wa watu wa kwanza.

39. Na piganeni nao mpaka yasiweko mateso, na dini iwe kabisa kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyeezi Mungu anayaona wanayoyatenda.

40. Na kama wakigeuka, basi jueni kwamba Mwenyeezi Mungu ndiye Mola wenu, na Mola Mwema na msaidizi Mwema.

41. Na jueni kwamba chochote mlichokiteka, basi sehemu yake ya tano ni ya Mwenyeezi Mungu na Mtume na jamaa (zake Mtume) na yatima na masikini na msafiri, ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyeezi Mungu na yale tuliyoyateremsha kwa Mja wetu siku ya kipambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili na Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

42. (Kumbukeni) mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao walikuwa kando ya bonde lililo mbali, na msafara ulipokuwa chini yenu, na kama mngelipatana katika miadi bila shaka mngelikhitilafiana. Lakini ili Mwenyeezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lenye kutendeka ili yule aangamiaye aangamie kwa dalili dhahiri na asalimike wa kusalimika kwa dalili dhahiri. Na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

43. (Kumbuka) Mwenyeezi Mungu alipokuonyesha katika usingizi wako (kwamba wao) ni wachache, na kama angelikuonyesha kwamba wao ni wengi mngelivunjika nguvu na mngelizozana katika jambo hilo, lakini Mwenyeezi Mungu kakuvueni. Bila shaka yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

44. Na (Kumbukeni) alipokuonyesheni machoni mwenu mlipokutana (kwamba wao) ni wachache na akawafanyeni kuwa wachache machoni mwao, ili Mwenyeezi Mungu alitimize jambo aliloamuru litendeke, na mambo yote hurejeshwa kwa Mwenyeezi Mungu.

45. Enyi mlioamini! mnapokutana na jeshi, basi kuweni imara na mumkumbuke Mwenyeezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.

46. Na mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wala msigombane, msije mkavunjika mioyo na kupoteza nguvu zenu, na vumilieni, bila shaka Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wenye kuvumilia.

47. Wala msiwe kama wale waliotoka katika majumba yao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu ameyazunguka yote wanayoyafanya.

48. Na (Kumbukeni) shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo kuna wa kukushindeni katika watu, na hakika mimi ni Mlinzi wenu. Lakini  yalipoonana majeshi mawili, (shetani) akarudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, hakika mimi naona msiyoyaona bila shaka mimi ninamuogopa mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

49. (Kumbukeni) waliposema wanafiki na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao: watu hawa dini yao imewadanganya, na mwenye kutegemea kwa Mwenyeezi mungu, basi kwa hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

50. Na kama ungeliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao na kuwaambia: onjeni adhabu ya Moto.

51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyofanywa na mikono yenu. Na hakika Mwenyeezi Mungu si Mwenye kuwadhulumu waja (wake).

52. Ni kama hali ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao, walizikataa Aya za Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo Mwenyeezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya makosa yao, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.

53. Hayo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu habadilishi kabisa neema aliyowaneemesha watu mpaka wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao, na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

54. Ni kama hali ya watu wa Firaun na wale waliokuwa kabla yao, walizikadhibisha Aya za Mola wao, kwa hiyo tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukawazamisha watu wa Firaun, na wote walikuwa madhalimu.

55. Hakika wanyama walio wabaya zaidi mbele ya Mwenyeezi Mungu ni wale waliokufuru, nao hawaaamini.

56. Ambao umewaahidi miongoni mwao, kisha wakavunja ahadi yao kila mara nao hawaogopi.

57. Basi ukiwakuta vitani uwakimbize walio nyuma yao ili wapate kufahamu.

58. Na kama ukiogopa khiyana kwa watu, basi watupie (ahadi yao) kwa usawa, hakika Mwenyeezi Mungu hawapendi wafanyao khiyana.

59. Wala wale waliokufuru wasifikiri kuwa wao ametangulia, kwa hakika wao hawatamshinda (Mwenyeezi Mungu).

60. Na waandalieni nguvu muwezavyo, na kwa farasi waliofungwa (kwa maandalizi hayo) muogopeshe maadui wa Mwenyeezi Mungu na maadui zenu, na wengine wasiokuwa wao, msiowajua, Mwenyeezi Mungu anawajua. Na chochote mtakachokitoa katika njia ya Mwenyeezi Mungu mtarudishiwa kamili na nyinyi hamtadhulumiwa.

61. Na kama wakielekea (hao maadui) kwenye amani nawe pia ielekee na mtegemee Mwcnyeezi Mungu, hakika yeye ndiye Asikiaye, Ajuaye.

62. Na kama wakitaka kukuhadaa, basi Mwenyeezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndiye aliyekusaidia kwa ushindi wake na kwa waumini.

63. Na akaziunga nyoyo zao hata kama ungelitoa yote yaliyomo ardhini usingeliweza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyeezi Mungu ndiye aliyewaunganisha, hakika yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

64. Ewe Nabii! Mwenyeezi Mungu anakutosha wewe na yule aliyekufuata katika waumini.

65. Ewe Nabii! wahimize walioamini waende vitani, kama wakiwa miongoni mwenu ishirini wanaosubiri, watawashinda mia mbili. Na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, kwa sababu wao ni watu wasiofahamu.

66. Sasa Mwenyeezi Mungu amekukhafifishieni na anajua kwamba kuna udhaifu kati yenu kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.

67. Haimpasi Nabii kuwa na mateka mpaka apigane na kushinda katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, hali Mwenyeezi Mungu anataka Akhera na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

68. Isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyeezi Mungu, bila shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

69. Basi kuleni katika vile mlivyoteka (vitani) ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyeezi Mungu hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

70. Ewe Nabii! waambie wale mateka walio mikononi mwenu! kama Mwenyeezi Mungu akiona wema wowote nyoyoni mwenu, atawapeni vizuri kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atakusameheni, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

71. Na kama wanataka kukufanyia khiyana, basi walikwisha mfanyia Mwenyeezi Mungu khiyana zamani, lakini akakupa ushindi juu yao, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

72. Hakika wale walioamini na wakahama, na wakapigania dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, na wale waliowapa (Muhajiri) mahala pa kukaa na wakainusuru (dini ya Mwenyeezi Mungu) hao ndio marafiki wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhama, nyinyi hamna haki ya kurithiana nao hata kidogo mpaka wahame (katika nchi ya kikafiri). Na kama wakiomba msaada kwenu katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano kati yenu na wao na Mwenyeezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

73. Na wale waliokufuru ni marafiki wao kwa wao, msipofanya hivi (basi) itakuwako chokochoko katika nchi na machafuko makubwa.

74. Na wale walioamini na kuhama na wakapigania dini ya Mwenyeezi Mungu na wale waliowapa (Muhajiri) mahala pa kukaa na wakainusuru (dini ya Mwenyeezi Mungu) hao ndio waumini wa kweli, watapata msamaha na riziki tukufu.

75. Na wale watakao amini baadaye na wakahama na wakapigana Jihadi pamoja na nyinyi, basi hao ni miongoni rnwenu na ndugu wa nasaba, wana haki zaidi wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.