SUURATUL AN'AAM

Sura hii imeteremshwa Makka Aya 165

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

1. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi, na akafanya giza na nuru, kisha wale waliokufuru wanamsawazisha Mola wao.

2.Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo kisha akaweka muda, na muda maalumu uko kwake, kisha nyinyi mnafanya shaka.

3. Na yeye ndiye Mwenyeezi Mungu katika mbingu na katika ardhi, anajua ndani yenu na nje yenu na anajua yale mnayoyachuma.

4. Na haiwafikii hoja yoyote katika hoja za Mola wao ila wanaikataa.

5. Na wameikadhibisha haki ilipowafikia, kwa hivi zitawafikia khabari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

6. Je, hawaoni umma ngapi tulizoziangamiza kabla yao? tuliwamakinisha katika nchi tusivyokumakinisheni (nyinyi) na -tukawapelekea mvua iendeleayo, na tukaifanya mito ipite chini yao. Na tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukaumba baada yao umma nyingine.

7. Na kama tungelikuteremshia maandishi katika karatasi na wakayagusa kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema: Haya si chochote ila ni uchawi dhahiri.

8. Na husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika. Na kama tungeliteremsha Malaika bila shaka ingelihukumiwa amri, kisha wasingelipewa nafasi.

9. Na kama (Mtume) tungelimfanya Malaika bila shaka tungelimfanya kama binadamu, na tungeliwatatanisha yale wanayoyatatanisha.

10. Na hakika walifanyiwa mzaha Mitume wa kabla yako, na yakawazunguka wale waliofanya mzaha miongoni mwao yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

11. Waambie: Safirini katika nchi, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wakadhibishaji.

12. Waulize: Ni vya nani vilivyomo mbinguni na ardhini? sema: Ni vya Mwenyeezi Mungu. yeye amejilazimisha (kuwafanyia rehema), hakika atakukusanyeni siku za Kiyama isiyo na shaka ndani yake, wale waliojitia khasarani, basi wao hawataamini.

13. Na ni vyake (Mwenyeezi Mungu) vinavyokaa katika usiku na mchana, naye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

14. Sema: je, nifanye kiongozi asiyekuwa Mwenyeezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi naye hulisha wala halishwi? Sema: Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza katika wenye kusilimu, nawe usiwe miongoni mwa wanaomshirikisha.

15. Sema; Hakika mimi naogopa adhabu ya siku kubwa ikiwa nitamuasi Mola wangu.

16. Atakayeepushwa nayo (adhabu) siku hiyo (ya Kiyama) bila shaka amemrehemu (Mwenyezi Mungu) na huko ndiko kufaulu dhahiri.

17. Na kama Mwenyeezi Mungu akikugusisha taabu, basi hakuna yeyote awezaye kuiondoa ila yeye, na kama akikugusisha kheri, basi yeye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

18. Na yeye ni Mwenye kushinda juu ya waja wake, na yeye ndiye Mwenye hekima, Mwenye khabari (zote).

19. Waulize: Kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa zaidi? sema: Mwenyeezi Mungu ndiye shahidi baina yangu na bainayenu. Na Qur'an hii imefunuliwa kwangu ili kwayo niwaonyeni na kwayeyote imfikiae. Je nyinyi mnashuhudia kwamba wako waungu wengine pamoja na Mwenyeezi Mungu? Sema: Mimi sishuhudii. Sema: Yeye ni Mwenyeezi Mungu Mmoja tu, na hakika mimi ni mbali na hayo mnayoyashirikisha.

20. Wale tuliowapa Kitabu wanamfahamu (Mtume Muhammad) kama wanavyowafahamu watoto wao, wale wanaojitia khasarani, basi wao hawaamini.

21. Na nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye uongo Mwenyeezi Mungu au azikadhibishaye Aya zake? hakika madhalimu hawafaulu.

22. Na (kumbukeni) siku ambayo tutawakusanya wote pamoja, kisha tutawaambia wale walioshirikisha: Wako wapi washirika wenu mliokuwa mnadai?

23. Kisha hautakuwa udhuru wao isipokuwa watasema: Wallahi, Mola wetu, hatukua washirikina.

24. Angalia jinsi wanavyosema uongo juu ya nafsi zao, na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.

25. Na wako miongoni rnwao wanaokusikiliza, na tumezitia pazia nyoyo zao wasije kuyafahamu, na mnauziwi masikioni mwao, na wakiziona kila hoja hawaziamini. Hata wanapokujia kukujadili, wale waliokufuru husema: Hizi si chochote ila ni hadithi tu za watu wa kale.

26. Nao wanakataza (watu kuyafuata) haya na (wao) wanajiweka mbali nayo, na hawaangamizi ila nafsi zao hali hawatambui.

27. Na ungeona watakaposimamishwa Motoni, waseme: Laiti tungerudishwa wala hatutakadhibisha Aya za Mola wetu na tutakuwa katika wanaoamini.

28. Bali yamewadhihirikia waliyokuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangelirudishwa bila shaka wangeyarudia yale waliyokatazwa, na bila shaka wao ni waongo.

29. Na walisema: Hakuna kingine ila maisha yetu ya dunia tu, wala sisi hatutafufuliwa,

30. Na ungeona watakaposimamishwa mbele ya Mola wao! Akasema: Je, si kweli haya? Watajibu: Naam, kwa hakiya Mola wetu atawaambia: Basi ionjeni adhabu kwa sababu mlikuwa mkikataa.

31. Bila shaka wamekwisha pata khasara wale waliokadhibisha kukutana na Mwenyeezi Mungu hata itakapowafikia saa ile kwa ghafla watasema: Oo! Majuto yetu! kwa yale tuliyoyapuuza, nao watabeba mizigo ya (madhambi) yao miogongoni mwao, angalieni ni mabaya (sana) wanayoyabeba.

32. Na maisha ya dunia si kitu ila mchezo tu na upuuzi. Na bila shaka nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wale wamchao (Mwenyeezi Mungu) basi hamtii akilini?

33.Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Basi wao hawakukadhibishi lakini madhalimu wanakanusha hoja za Mwenyeezi Mungu.

34. Na hakika wamekadhibishwa Mitume kabla yako, wakavumilia, kwa kule kukadhibishwa na kuudhiwa mpaka ukawafikia ushindi wetu. Na hakuna abadilishaye maneno ya Mwenyeezi Mungu, na bila shaka zimekufikia baadhi ya khabari za Mitume.

35. Na ikiwa kujitenga kwao ni makubwa kwako, basi kama unaweza kutafuta njia (ya chini kwa chini) katika ardhi, au ngazi mbinguni na kuwaletea hoja. Na kama Mwenyeezi Mungu angependa bila shaka angeliwakusanya kwenye muongozo basi usiwe miongoni mwa wasiojua.

36. Hakika wanaokubali ni wale tu wanaosikia. Na wafu (wasiotaka kusikia) Mwenyeezi Mungu atawafufua kisha watarejeshwa kwake.

37. Na husema: Kwa nini hakuteremshiwa Muujiza kutoka kwa Mola wake? Waambie: Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo wa kuteremsha Muujiza lakini wengi wao hawajui.

38. Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake mbili, ila ni uma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote, kisha watakusanywa kwa Mola wao.

39. Na wale waliokadhibisha hoja zetu, ni viziwi na mabubu waliomo gizani. Mwenyeezi Mungu humwachia kupotea amtakae, na humweka katika njia iliyonyooka amtakae.

40. Sema: Mnaonaje, kama ikiwafikieni adhabu ya Mwenyeezi Mungu au kiwafikieni Kiyama je, mtamwita asiyekuwa Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi, ni wakweli?

41. Bali yeye ndiye mtamwita, naye atakuondoleeni mnayo muomba akipenda, na mtasahau mnao washirikisha.

42. Na kwa hakika tulipeleka (Mitume) kwa nyumati zilizokuwa kabla yako, kisha tukazitia katika dhiki na mashaka ili zipate kunyenyekea.

43. Basi mbona hawakunyenyekea ilipowafikia adhabu yenu? lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu, na shetani akawapambia waliyokuwa wakiyafanya.

44.Basi waliposahau yale waliyokumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu mpaka walipofurahia yale waliyopewa tukawakamata ghafla na mara wakawa wenye kukata tamaa.

45. Ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu na kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu Mola wa walimwengu.

46. Sema: Mnaonaje, kama Mwenyeezi Mungu akikuondoleeni kusikia kwenu na kuona kwenu, na akazipiga muhuri nyoyo zenu ni nani mungu mwingine isipokuwa Mwenyeezi Mungu awezaye kukuleteeni tena? Tazama jinsi tunavyozieleza Aya, kisha wao wanapuuza.

47. Sema: Mnaonaje, kama ikikufikieni kwa ghafla adhabu ya Mwenyeezi Mungu au (ikakufikieni) kwa dhahiri, nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu.

48. Na hatutumi Mitume ila huwa watoaji khabari njema na waonyaji. Na wenye kuamini na kufanya wema haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

49. Na wale waliokadhibisha Aya zetu itawapata adhabu kwa sababu ya kule kuasi kwao.

50. Sema: Mimi siwaambii ninazo khazina za Mwenyeezi Mungu, wala najua mambo yaliyofichikana, wala siwaambieni mimi ni Malaika sifuati ila yale yanayofunuliwa kwangu. Sema: Je, kipofu na mwenye macho huwa sawa? basi je, hamfikiri?

51. Na uwaonye kwa (Qur'an) wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao, (hali kuwa) hawana Kiongozi yeyote asiyekuwa yeye, wala muombezi ili wapate kumcha Mungu.

52. Wala usiwafukuze wale wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hesabu yao hata kidogo, wala hesabu yako si juu yao hata kidogo, na kuwafukuza, basi utakuwa miongoni mwa madhalimu.

53. Na namna hii tumewafanyia mtihani baadhi yao kwa wengine ili waseme: Je, hao ndio Mwenyeezi Mungu amewafanyia hisani miongoni mwetu? Je, Mwenyeezi Mungu hawajui wanaoshukuru?

54. Na wanapokufikia wale wanaoamini Aya zetu, basi waambie: Amani iwe juu yenu, Mola wenu amejilazimisha rehema, kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akafanya wema, basi yeye ndiye Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehernu.

55. Na namna hii tunazieleza Aya ili njia ya waovu ibainike.

56. Sema: Hakika nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu. Sema sifuati matamanio yenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walio ongoka.

57. Sema: Mimi ninayo dalili ya wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha sina mnayoyataka kwa haraka, hapana hukumu ila kwa Mwenyeezi Mungu, anaelezea yaliyo kweli, naye ni Mbora wa kuhukumu.

58. Sema: Kama ningelikuwa nayo mnayoyahimiza, bila shaka ingelikwisha katwa shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyeezi Mungu anawajua sana madhalimu.

59. Na ziko kwake funguo za (mambo) yaliyofichikana, hakuna azijuaye ila yeye tu, Na anajua yaliyomo barani na baharini, na halianguki jani ila analijua, wala punje katika giza la ardhi, wala kilichorutubika wala kilichoyabisika, ila yamo katika Kitabu kidhihirishacho.

60. Na ndiye anayekufisheni wakati wa usiku na anayafahamu mnayoyatenda wakati wa mchana, kisha yeye hukufufueni humo ili muda uliowekwa umalizike. Kisha kwake ndio marudio yenu, akwambieni yale mliyokuwa mkiyafanya.

61. Naye ndiye Mwenye kushinda, (aliye) juu yawajawake, na hukuleteeni (Malaika) wanaohifadhi (matendo yenu). Hata mmoja wenu anapofikiwa na mauti, wajumbe wetu humfisha nao hawalegei.

62. Kisha wanarudishwa kwa Mwenyeezi Mungu Mola wao wa haki. Sikilizeni! Hukumu ni yake, naye ni Mwepesi sana wa wanaohesabu.

63. Waulize: Ni nani anayekuokoeni katika taabu za bara na bahari? ninamuomba kwa unyenyekvu, na kwa siri. Kama akituokoa katika (shida) hii, bila shaka tutakua miongoni mwa wanaoshukuru.

64. Sema: Mwenyeezi Mungu hukuokoeni katika hayo na katika kila mashaka, kisha nyinyi mnamshirikiha!!

65. Sema: Yeye ndiye awezaye kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu au kukuvurugeni muwe makundi makundi, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao, tazama jinsi tunavyoeleza Aya ili wapate kufahamu.

66. Na watu wako wameikadhibisha (Qur'an) hali hiyo ni haki. Sema: Mimi si mlinzi juu yenu.

67. Kila khabari ina wakati maalum, na hivi karibuni mtajua.

68. Na unapowaona wale wanaozungumza Aya zetu, (kwa kuzikadhibisha) basi jitenge nao mpaka wazungumze maneno mengine na kama shetani akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu madhalimu.

69. Wala si juu ya wale wanaomcha (Mwenyeezi Mungu) Hesabu yao (madhalimu) hata kidogo, lakini ni (juu yao kuwapa) mawaidha ili wapate kujiepusha.

70. Na waache wale walioifanyia dini yao mchezo na upuuzi, na yamewadanganya maisha ya dunia, na wakumbushe kwa (Qur'an) isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma, haina mlinzi wala muombezi yeyote isipokuwa Mwenyeezi Mungu. Na hata ikitoa fidia ya kila namna haitapokelewa kwake. Hao ndio walioangamizwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto na adhabu iumizayo kwa sababu walikuwa wakikataa.

71. Sema: Je, tumuombe asiyekuwa Mwenyeezi Mungu ambaye hatupi faida wala hawezi kutudhuru, na turudishwe nyuma baada ya Mwenyeezi Mungu kutuongoza, sawa na yule ambaye mashetani yamempoteza akiwayawaya katika ardhi? Anao marafiki wanao mwita kwenye muongozo hasa ni muongozo wa Mwenyeezi Mungu na tumeamrishwa tumnyenyekee Mola wa walimwengu wote.

72. Na tumeambiwa simamisheni swala na mcheni yeye, naye ndiye ambaye mtakusanywa kwake.

73. Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki, na siku anayosema: Kuwa, basi huwa. Kauli yake ni haki, na ufalme ni wake siku itakapopulizwa parapanda, Mjuzi wa yaliyofichikana na yanayo onekana, naye ndiye Mwenye hekima, Mwenye khabari.

74. Na (kumbukeni) Ibrahim alipomwambia babayake Azara, Je, unawafanya masanamu kuwa waungu? hakika ninakuona wewe na watu wako katika upotovu dhahiri.

75. Na hivyo tukamuonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini.

76. Na usiku ulipomwingilia akaona nyota, akasema: Hii ni Mola wangu. Lakini ilipotua, akasema: Siwapendi wanao tua.

77. Na alipouona mwezi unang'aa, akasema: Huu ni Mola wangu. Lakini ulipotua, akasema: Asiponiongoza Mola wangu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu wapotovu.

78. Na alipoliona jua linang'aa akasema: Hili ni Mola wangu, hili kubwa kabisa, Lakini lilipotua, akasema: Enyi watu wangu! mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha.

79. Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi, hali yakuwa nimewacha dini za upotovu, mimi si miongoni mwa washirikina.

80. Na watu wake wakajadiliana naye, akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyeezi Mungu na hali ameniongoza? wala siogopi wale mnaowashirikisha naye, isipokuwa Mola wangu akipenda jambo kuwa, basi litakuwa, Mola wangu anao wasaa wa elimu ya kila kitu, basi je, hamzindukani?

81. Na nitawaogopaje hao mnaowashirikisha, hali nyinyi hamuogopi kumshirikisha Mwenyeezi Mungu na kile ambacho hakukiteremshia dalili kwenu? Basi kundi gani katika mawili linastahiki zaidi kupata amani, ikiwa nyinyi mnajua?

82. Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na dhulma, hao ndio watakaopata amani, nao ndio walioongoka.

83. Na hiyo ndiyo hoja yetu tuliyompa Ibrahim juu ya watu wake, tunamnyanyua katika vyeo yule tumtakaye, hakika Mola wako ndiye Mwenye hekima, Ajuaye.

84. Na tukampa (Ibrahim mtoto anayeitwa) Is'haka na Yaakub, wote tukawaongoza, na Nuhu tulimuongoza zamani na katika kizazi chake, Daudi na Suleiman na Ayubu na Yusuf na Musa na Harun, Na hivyo ndivyo tuwalipavyo wafanya mema.

85. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyasa, wote walikuwa miongoni mwa watu wema.

86. Na Ismail na Al Yasaa na Yunus na Luti, Na wote tukawafadhilisha juu ya walimwengu.

87. Na (tukawaongoza) baadhi ya baba zao (baaadhi ya) vizazi vyao na (baadhi ya) ndugu zao, na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.

88. Huo ni muongozo wa Mwenyeezi Mungu kwa huo humuongoza amtakaye katika waja wake, na kama wangemshirikisha bila shaka yangeliwaharibikia yale waliyokuwa wakiyatenda.

89. Hao ndio tuliowapa Kitabu na hukumu na Utume, kama hawa wakiyakataa hayo, basi tumekwisha yawekea watu wasioyakataa.

90. Hao ndio ambao Mwenyeezi Mungu amewaongoza, basi fuata muongozo wao, Sema: sikuombeni malipo juu ya haya, hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa watu.

91. Na (Mayahudi) hawakumheshimu Mwenyeezi Mungu kama inavyotakiwa kumheshimu, waliposema: Mwenyeezi Mungu hakuteremsha chochote juu ya binadainu. Sema: Ni nani aliyekiteremsha Kitabu alicholeta Musa? chenye nuru na muongozo kwa watu, mlichokifanya juzuu juzuu, mkadhihirisha sehemu yake na yaliyo mengi mkayaficha. Na mkafundishwa msiyoyajua nyinyi wala baba zenu. Sema: Mwenyeezi Mungu (ndiye aliyekiteremsha) kisha waache wacheze katika porojo lao.

92. Na hiki ni Kitabu tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kuhakikisha yaliyotangulia na ili uwaonye (watu wa) mama wa miji (Makka) na walio pembezoni mwake. Na wale walioamini Akhera hukisadiki, nao huziangalia vizuri swala zao.

93. Na nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliae uwongo Mwenyeezi Mungu au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi, na hali hakuletewa chochote na yule asemaye: Nitateremsha (ufunuo) kama ule aliouteremsha Mwenyeezi Mungu. Na kama ungewaona madhalimu watakapokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono yao (na kuwaambia) zitoeni roho zenu, leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkisema juu ya Mwenyeezi Mungu pasipo haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi Aya zake.

94. Na (siku ya Kiyama tutakwambieni) bila shaka mmetujia mmoja mmoja kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza, na mmeyaacha nyuma tuliyokupeni, na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai kuwa ni washirika (wa Mwenyeezi Mungu) kwenu. Bila shaka yamekatika (mahusiano yaliyokuwa) baina yenu, na yamekupoteeni mliyokuwa mkidai.

95. Hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mchipushaji wa mbegu na kokwa, hutoa mzima katika maiti, na mtoaji wa maiti katika mzima huyo ndiye Mwenyeezi Mungu, basi mnageuzwa wapi?

96. Ndiye anayepambazua mwangaza asubuhi na ameufanya usiku kuwa mapumziko, najua na mwezi kwa kuhesabu. Hayo ndiyo matengenezo ya Mwenye nguvu, Mjuzi.

97. Na Yeye ndiye aliyekuumbieni nyota ili muongoke kwazo katika giza la bara na bahari, hakika tumezichambua dalili kwa watu wanaojua.

98. Na Yeye ndiye aliyekuumbeni katika nafsi moja, na pako mahala pakukaa na mahala pa kuwekea, hakika tumezichambua dalili kwa watu wanaofahamu.

99. Na Yeye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mawinguni, na kwayo tunaotesha mimea ya kila kitu, na tunachipusha (majani ya) kijani katika (mimea) hiyo, tukatoa ndani yake punje zilizopangana. Na katika mitende tunatokeza katika makole yake vishada vyenye kuinama, na bustani za zabibu na mizaituni na makomamanga, yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapopamba na kuiva kwake, hakika katika hayo ziko dalili kwa watu wanaoamini.

100. Na wakamfanyia Mwenyeezi Mungu majinni kuwa washirika, hali amewaumba na wanamsingizia kuwa ana watoto wa kiume na wa kike pasipo kujua. Ameepukana na upungufu, nayu juu kuliko yale wanayomsifu nayo.

101. Muumbaji wa mbingu na ardhi, inawezekanaje awe na mtoto hali hana mke, na ameumba kila kitu naye ni Mjuzi wa vitu vyote?

102. Huyo ndiye Mwenyeezi Mungu, Mola wenu, hakuna aabudiwaye ila yeye tu. Muumba wa kila kitu, basi mwabuduni naye ni Mlinzi wa kila kitu.

103. Maono hayamfikii, bali yeye anayafikia maono, naye ni Mwenye kujua (ya ndani) Mwenye khabari.

104. Hakika zimekufikieni hoja kubwa kutoka kwa Mola wenu, basi anayeona ni kwa faida yake mwenyewe, na anayepofuka, basi ni khasara yake mwenyewe, nami si mlinzi wenu.

105. Na hivi ndivyo tunazikariri Aya (wapate kufahamu) na wanasema: Umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanaojua.

106. Fuata uliyofunuliwa kutoka kwa Mola wako. Hakuna aabudiwaye ila yeye tu, najitenge na washirikina.

107. Na kama Mwenyeezi Mungu angependa wasingelishirikisha, na hatukukufanya uwe Mlinzi juu yao, wala wewe si wakili juu yao.

108. Wala msiwatukane wale ambao wanawaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyeezi Mungu kwa jeuri bila kujua. Hivyo tumewapambia kila watu vitendo vyao kisha marejeo yao kwa Mola wao, na atawaambia waliyokuwa wakiyatenda.

109. Na (makafiri) waliapa kwa Mwenyeezi Mungu kwa viapo vyao vyenye nguvu, kama utawafikia Muujiza watauamini. Sema: Hakika Miujiza iko kwa Mwenyeezi Mungu tu, na ni kitu gani kilichokutambulisheni, ya kuwa itakapofika hawataamini.

110. Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao kwa kuwa hawakuiamini mara ya kwanza, na tutawaacha katika maasi yao wakitangatanga.

111. Na kama tungewateremshia Malaika, na wafu wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, wasingeliamini isipokuwa atakapo Mwenyeezi Mungu, Lakini wengi wao wamo ujingani.

112. Na namna hiyo tumemfanyia kila Nabii maadui, mashetani katika watu na majinni. Baadhi yao wanawafunulia wengine maneno ya kupambapamba ili kuwadanganya. Na kama Mola wako angelipenda wasingelifanya hilo basi waache na wanayoyazua.

113. Na ili zielekee kwa hayo (maneno yao) nyoyo za wale wasioamini Akhera na wayaridhie na ili wayachume wanayoyachuma.

114. Je, nimtafute hakimu asiyekuwa Mwenyeezi Mungu hali yeye ndiye aliyekuteremshieni Kitabu kielezacho wazi wazi? Na wale tuliowapa Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako kwa haki, basi usiwe miongoni mwa watiao shaka.

115. Na limetimia neno la Molawako kwa kweli na uadilifu, hakuna awezaye kuyabadilisha maneno yake, na yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

116. Na kama ukiwatii wengi katika (hawa) waliomo ulimwengu watakupoteza na njia ya Mwenyeezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu, hawana ila (ni wenye kusema) uongo tu.

117. Hakika Mola wako ndiye anayewajua sana wanaopotea njia yake, na ndiye anayewajua sana wanao ongoka.

118. Basi kuleni katika wale waliosomewa jina la Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi mnaziamini Aya zake.

119. Na kwa nini msile (wanyama) wale waliosomewa jina la Mwenyeezi Mungu na hali amekubainishieni alivyowaharamishieni, isipokuwa vile mnavyolazimishwa. Na hakika wengi wanapoteza (wengine) kwa matamanio yao bila elimu, bila shaka Mola wako ndiye awajuaye sana warukao mipaka.

120. Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana, hakika wale wanaochuma dhambi watalipa yale waliyokuwa wakiyachuma.

121.Wala msile katika wale wasiosomewa jina la Mwenyeezi Mungu, kwa sababu huo hakika ni uasi. Na kwa hakika mashetani wanaowafunulia marafiki zao kubishana nanyi na ikiwa mtawatii hakika nyinyi mtakuwa washirikina.

122. Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru, kwa (nuru) hiyo hutembea katika watu anaweza kuwa sawa na yule ambaye hali yake ni kuwa gizani asiyeweza kutoka humo? Hivyo ndivyo wamepambiwa makafiri waliyokuwa wakiyafanya.

123. Na hivyo tukajaaalia katika kila mji wakuu wa wakosefu wake, ili wafanye vitimbi humo, wala hawafanyi hila isipokuwa nafsi zao, lakini hawatambui.

124. Na inapowafikia hoja, husema: Hatuwezi kuamini mpaka tupewe kama yale waliyopewa Mitume wa Mwenyeezi Mungu. Mwenycezi Mungu ndiye ajuaye zaidi atakapoweka ujumbe wake. Hivi karibuni utawafikia waovu udhalili kutoka kwa Mwenyeezi Mungu na adhabu kali kwa sababu ya hila walizokuwa wakifanya.

125. Basi yule ambaye Mwenyeezi Mungu anataka kumuongoza humfungulia kifua chake Uislaamu, na yule ambaye Mwenyeezi Mungu anataka kumhukumu kupotea hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana kama kwamba anapanda mbinguni. Hivi ndivyo Mwenyeezi Mungu huweka uchafu juu ya wale wasioamini.

126. Na hii (dini ya Uislam) ndiyo njia ya Mola wako iliyonyooka, bila shaka tumezipambanua Aya kwa watu wenye kukumbuka.

127. (Watu wema) watapata nyumba ya salama kwa Mola wao, naye ni Kiongozi wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

128. Na (wakumbushe) siku atakapowakusanya wote (awaambie) Enyi makundi ya majinni! hakika mmechukua wafuasi wengi katika wanadamu. Na marafiki wao katika wanadamu watasema; Mola wetu! tulinufaishana sisi na wao, na tumefikia muda wetu uliotuwekea. Atasema: Moto ndio makazi yenu, mtakaa humo milele ila apende Mwenyeezi Mungu, hakika Mola wako ndiye Mwenye hekima, Ajuaye.

129. Na hivyo tukawatawalisha baadhi ya madhalimu juu ya wengine kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

130. Enyi makundi ya majinni na wanadamu! Je, hawakuwafikieni Mitume miongoni mwenu kukusomeeni Aya zangu na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya maisha ya dunia, nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri,

131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako hakuwa wa kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyeji wake wameghafilika.

132. Na wote wana vyeo sawa na yale waliyoyatenda, na Mola wako si Mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.

133. Na Mola wako ndiye Mkwasi, Mwenye rehema. Kama akitaka atakuondoeni na kuweka wengine awatakao baada yenu kama vile alivyokuumbeni katika uzazi wa watu wengine.

134. Hakika mnayoahidiwa yatafika, wala hamtaweza kuyashinda.

135. Sema: Enyiwatu wangu! fanyeni katika makaoyenu, mimi (pia) nafanya. Hivi karibuni mtajua ni nani atakuwa na makao (mema) mwishoni, kwa sababu madhalimu hawafaulu.

136. Na wamemfanyia Mwenyeezi Mungu sehemu katika mimea aliyoiumba na katika wanyama, na husema: Hii ni ya Mwenyeezi Mungu kwa madai yenu, na hii ni ya waungu wetu. Basi vilivvokuwa vya waungu wao havifiki kwa Mwenyeezi Mungu, na vilivyokuwa vya Mwenyeezi Mungu, basi hivyo hufika kwa waungu wao. Ni mabaya wanayo yahukumu.

137. Na hivyo washirika wao wamewapambia washirikina wengi kuwaua watoto wao, ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Nakama Mwenyeezi Mungu angependa wasingelifanya hayo, basi waache na hayo wanayoyatunga.

138. Na husema: Wanyama hawa na mimea hii vimekatazwa, hawatavila ila wale tupendao kwa madai yao, na wanyama ambao migongo yao imeharamishwa (kupandwa) na wanyama ambao hawalitaji jina la Mwenyeezi Mungu juu yao, wanamzulia uongo. Atawalipa kwa yale waliyokuwa wakiyazua.

139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa hasa ni kwa ajili ya wanaume wetu, na wameharamishwa kwa wake wetu, na ikiwa nyamafu basi wanashirikiana. Atawalipa maelezo yao, kwani yeye ni Mwenye hekima, Ajuaye.

140. Bila shaka wamekhasirika wale ambao wamewaua watoto wao kwa upumbavu pasipo kujua, na wakaharamisha alivyo waruzuku Mwenyeezi Mungu kwa kumtungia uongo Mwenyeezi Mungu. Bila shaka wamepotea wala hawakuwa wenye kuongoka.

141. Naye ndiye aliyeziumba Bustani zilizoegemezwa na zisizoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbalimbali na mizaituni na makomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapopamba, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake, wala msitumie kwa fujo, hakika yeye hawapendi watumiao kwa fujo.

142. Na wako katika wanyama wabebao mixigo na (kutoa) matandiko. Kuleni katika vile alivyokuruzukuni Mwenyeezi Mungu, wala msifuate nyayo za shetani, hakika yeye ni adui yenu dhahiri.

143. Wako (namna) nane, wawili katika kondoo, na wawili katika mbuzi, waambie: Je, ameharamisha madume mawili (ya kondoo na mbuzi) au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? nambieni kwa elimu ikiwa nyinyi mnasema kweli.

144. Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? Au, nyinyi mlikuwako Mwenyeezi Mungu alipokuusieni haya? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule aliyemzulia Mwenyeezi Mungu uongo ili kuwapoteza watu bila ya elimu? Hakika Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

145. Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa Wahyi mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hivyo ni uchafu, au kisicho cha dini, kilichochinjwa kwa jina la asiyekuwa Mwenyeezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura pasipo kupenda wala kuruka mipaka, basi hakika Mola wako ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

146. Na kwa wale walio Mayahudi tuliharamisha kila chenye kucha, na katika ng'ombe na kondoo tukawaharamishia mafuta yao isipokuwa va'le iliyobeba migongo yao au (iliyobeba) matumbo au yale yaliyogandamana na mifupa. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya uasi wao, na sisi ndio wa kweli.

147. Kama wakikukadhibisha, basi waambie! Molawenu ni Mwenye rehema nyingi na adhabu yake haizuiliwi kwa watu waovu.

148. Wanaomshirikisha Mwenyeezi Mungu watasema: Angelipenda Mwenyeezi Mungu tusingelimshirikisha sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha kitu chochote. Hivyo ndivyo walivyokanusha waliokuwa kabla yao mpaka wakaonja adhabu yetu, sema: Je, mnayo elimu? basi mtutolee hiyo, nyinyi hamfuati ila dhana tu, wala hamsemi ila uongo tu.

149. Sema: Basi Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye hoja ikomeshayo, na kama angelipenda angewaongozeni nyote.

150. Sema; Leteni mashahidi wenu wanaoweza kushuhudia kuwa Mecnyeezi Mungu ameharamisha (mnyama) huyu. Basi wakitoa ushahidi (wa uongo) wewe usishuhudie pamoja nao, wala usifuate matamanio ya wale waliokadhibisha Aya zetu na wasioamini Akhera, nao wanawafanya (masanamu) sawa na Mola wao.

151. Waambie: Njooni nikusomeeeni aliyokuharamishieni Mola wenu, kwamba msimshirikishe na chochote, na fanyeni wema kwa wazazi wenu, wala msiue watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tutakupeni riziki na wao, wala msikaribie mambo maovu, yaliyo dhahiri na yaliyo siri, wala msimuue mtu ambaye Mwenyeezi Mungu ameharainisha (kuuawa) ila kwa haki. Hayo amewausieni ili mzingatie.

152. Wala msikaribie mali ya yatima, isipokuwa kwa njia bora, mpaka afike baleghe yake. Na kamilisheni kipimo na mizani kwa uadilifu, hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uweza wake. Na msemapo, basi semeni kwa insafu ingawa ni jamaa, na tekelezeni ahadi ya Mwenyeezi Mungu, hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka.

153. Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni, wala msifuate njia mbali mbali zikakutengeni mbali na njia yake. Hayo amekuusieni ili mpate kujilinda.

154. Kisha tulimpa Musa Kitabu kwa kutimiza (neema) juu ya yule aliyefanya wema, na maelezo ya kila kitu, na muongozo na rehema ili wapate kuamini mkutano wa Mola wao.

155. Na hii Qur-an ni Kitabu tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, basi kifuateni na muwe wacha Mungu ili mrehemewe.

156. Msije mkasema: Hakika Kitabu kiliteremshwa juu ya makundi mawili kabla yetu, nasi tulikuwa hatuna khabari ya yale waliyoyasoma.

157. Au mkasema: Lau tungeliteremshiwa Kitabu bila shaka tungelikuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu, na muongozo na rehema. Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezikadhibisha Aya za Mwenyeezi Mungu na akajitenga nazo? Tutawalipa wale wanaojitenga na Aya zetu adhabu mbaya kwa sababu walikuwa wakijitenga.

158. Hawangoji ila wawafikie Malaika au Mola wako afike, au zifike baadhi ya dalili za Mola wako, siku zitakapofika baadhi ya Ishara za Mola wako, (hapo) kuamini hakutomfaa mtu kitu ikiwa hakuamini zamani, na hakuchuma kheri katika Uislaam wake. Sema Ngojeni, sisi pia tunangoja.

159. Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna uhusiano nao wowote. Bila shaka shauri lao ni kwa Mwenyeezi Mungu, kisha atawaambia yale waliyokuwa wakitenda.

160. Afanyaye kitendo kizuri, atalipwa mfano wake mara kumi, na afanyae kitendo kibaya, basi hatalipwa ila sawa nacho, nao hawatadhulumiwa.

161. Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza kwenye njia iliyonyooka dini iliyo sawa kabisa, ndiyo mila ya Ibrahim muongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

162. Sema: Hakika swala yangu na ibada zangu na uzima wangu na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, Mola wa ulimwengu wote.

163. Hana mshirika, na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Mwenyeezi Mungu).

164. Sema: Je, nishike Mola mwingine asiyekuwa Mwenyeezi Mungu. hali yeye ndiye Mola wa kila kitu? wala nafsi yoyote haichumi (ubaya) ila juu yake, wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Kisha marudio yenu ni kwa Mola wenu, naye atawaambieni yale mliyokuwa mkikhitilafiana.

165. Naye ndiye aliyekufanyeni makhalifa katika ardhi, na amewanyanyua badhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo aliyokupeni. Hakika Mola wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.