Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Enyi watu! mcheni Mola wenu ambaye amewaumba kutokana na nafsi moja, na akaumba kutokana na (nafsi) hiyo wa pili wake, na akaeneza kwa wawili hao wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyeezi Mungu ambaye mnaomba kwaye (na kuangalia) jamaa wa karibu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mlinzi juu yenu.
2. Na wapeni yatima mali zao, wala msibadilishe mazuri kwa mabaya, wala msile mali yao pamoja na mali yenu, hakika hiyo ni dhulma kubwa.
3. Na kama mkiogopa kwamba hamuwezi kufanya uadilifu katika mayatima, basi oweni mnaowapenda katika wanawake, wawili wawili au watatu watatu au wanne wanne. Na mkiogopa kuwa hamuwezi kufanya uadilifu basi (oeni) mmoja au waliomilikiwa na mikono yenu, hii ni karibu zaidi na kutofanya dhulma.
4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni hadiya, lakini wakikupeni chochote kwa radhi ya nafsi katika hayo, basi kileni kiwashuke kwa raha.
5. Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyeezi Mungu amewajaalia ili kuwapelekea maisha, na walisheni katika hayo na muwavishe, na muwaambie maneno mazuri.
6. Na wajaribuni yatima mpaka wafikilie (umri wa) kuoa, basi kama mkiwaona wana akili njema, wapeni mali yao, wala msiyale kwa fujo na kwa haraka kwamba watakuwa wakubwa. Na aliyekuwa tajiri, basi ajiepushe, na atakayekuwa fakiri, basi ale kwa kadiri ya ada. Na mtakapowapa mali yao, basi muwawekee mashahidi, na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa ni Mwenye kuwahasibu.
7. Wanaume wana fungu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa waliowakaribia, na wanawake wana fungu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa walio wakaribia, ikiwakidogo au kingi, (hili ni) fungu lililofaradhiwa.
8. Na watakapohudhuria wakati wa kugawanya jamaa na yatima na masikini, basi wapeni katika hayo, na waambieni maneno mazuri.
9. Na (warithi) waogope kama wangeacha nyuma yao watoto wanyonge wangewakhofia basi wamuogope Mwenyeezi Mungu na waseme maneno ya kweli.
10. Hakika wale ambao wanakula mali ya yatima kwa dhulma, bila shaka wanakula Moto matumboni mwao, na wataingia Motoni.
11. Mwenyeezi Mungu anawausia kwa watoto wenu, mwanamume apate sawa na fungu la wanawake wawili, na wakiwa ni wanawake (watupu) zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili ya alichokiacha, na akiwa (binti) ni mmoja basi apewe nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja katika wao apate sudusya alichokiacha ikiwa (huyo maiti) ana mtoto. Ikiwa hanamtoto, na wazazi wake wawili ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja na kama (maiti) anao ndugu basi mamayake atapata sudus, baadaya (kutoa) aliyoyausia (marehemu) au (kulipa) deni. Baba zenu nawatoto wenu, hamjui ni nani katika wao aliye karibu zaidi wa manufaa yenu (Hiyo) ni Sharia itokayo kwa Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
12. Na nyinyi mtapata nusu ya walichoacha wake zenu, kama wao hawana mtoto, na ikiwa wana mtoto, nyinyi mtapata robo ya walichokiacha, baada ya (kutoa) wasia waliousia au (kulipa) deni nao (wake zenu) watapata robo ya mlichokiacha ikiwa hamna mtoto. Mkiwa na mtoto, basi watapata thumni ya mlichokiacha, baada ya (kutoa) wasia mtakaousia au (kulipa) deni. Na kama mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja katika wao atapata fungu la sita, na wakiwa zaidi kuliko hao basi watashirikiana katika fungu la tatu baada ya (kutoa) wasia utakaousiwa na (kulipa) deni pasipo kuleta madhara, (huu) ni wasia utokao kwa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.
13. Hiyo ni mipaka ya Mwenyeezi Mungu, na anayemtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake atamtia katika Pepo ipitayo mito chini yake watakaa milele humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa.
14. Na anayemuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na kuiruka mipaka yake atamtia katika Moto humo atakaa milele, na atapata adhabu ya kudhalilisha.
l5. Na wale wafanyao uchafu miongoni mwa wanawake wenu, basi washuhudishieni mashahidi wanne miongoni mwenu. Watakaposhuhudia, basi muwazuie majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyeezi Mungu awafanyie njia (nyingine).
16. Na wale wanao ufanya (huo uchafu) katika nyinyi, basi waadhibuni, na kama wakitubia na kujisahihisha basi waacheni. Hakika Mwenveezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
17. Hakika toba inayopokelewa na Mwenyeezi Mungu ni ya wale tu wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka, basi hao ndio Mwenyeezi Mungu huipokea toba yao, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima,
18. Na si toba ya wale ambao hufanya maovu mpaka mauti imemfikia mmoja wao, husema: Hakika mimi nimetubia sasa, wala ya wale ambao wanakufa hali ya kuwa wao ni makafiri, hao tumewaandalia adhabu iumizayo.
19. Enyi mlioamini! si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu, wala msiwazuie (kuolewa) ili mpate kuwanyang'anya baadhi ya vile mlivyowapa, ila watakapofanya uchafu huo wazi. Na kaeni nao kwa wema na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkachukia kitu na Mwenyeezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
20. Na kama mkitaka kubadilisha mke mahala pa mke, basi msichukue chochote katika hicho (mlichowapa). Je, mtakichukua kwa dhulma na makosa yaliyo wazi?
21. Na mtakichukuaje na hali mmeingiliana nyinyi kwa nyinyi, na (wao) wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?
22. Wala msioe wanawake walio olewa na baba zenu, ila yaliyokwisha pita, hakika hilo ni uchafu na ni jambo lenye kuchukiza na ni njia mbaya.
23. Mmeharamishiwa (kuoa) mama zenu na binti zenu na dada zenu na binti za
ndugu na binti za dada na mama zenu waliowanyonyesheni na dada zenu wa kunyonya
na mama za wake zenu na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu,
waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia. Lakini kama hamjawaingilia, basi si
vibaya kwenu (kuwaoa) na wake wa wana wenu
waliotoka katika migongo yenu, na kukusanya madada wawili (wakati mmoja)
isipokuwa yale yaliyokwisha pita. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe,
Mwenye kurehemu.
24. Na (pia mmeharamishiwa) wanawake wenye waume, isipokuwa wale walio milikiwa na mikono yenu, (ndiyo) Sharia ya Mwenyeezi Mungu juu yenu. Na mmehalalishiwa wasiokuwa hao, kwamba mtafute kwa mali yenu kwa kuoa bila ya kufanya zinaa. Ambao mmestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari yao yaliyolazimu, wala si vibaya kwenu katika yale mliyokubaliana baada ya (kutoa) mahari, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
25. Na miongoni mwenu asiyeweza kupata mali ya kuoa wanawake waungwana wa Kiislaamu, basi (aoe) katika wajakazi wenu wa Kiislaamu mliowamiliki na Mwenyeezi Mungu anajua sana imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na baadhi, basi waoweni kwa idhini ya watu wao na muwape mahari yao kwa Sharia, wanawake wema, si wazinifu, wala wenye kujifanyia mahawara. Na watakapoolewa, basi watakapofanya uchafu itawapasa nusu ya adhabu iwapasayo wanawake waungwana. Hayo ni kwa aliyechelea mashaka katika nyinyi, na mtakaposubiri ni bora zaidi kwenu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
26. Mwenyeezi Mungu anataka kuwabainishieni na kuwaongozeni kwenye mwendo wa wale waliowatangulieni na awakubalie (toba yenu) na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
27. Na Mwenyeezi Mungu anataka kuwarejesha (katika twaa yake) na wake wanaofuata matamanio (yao) hutaka ya kwamba ingeuke mgeuko mkubwa.
28. Mwenyeezi Mungu anataka kuwapunguzieni, na ameumbwa mwanadamu hali ya kuwa ni dhaifu.
29. Enyi mlioamini! msiliane mali yenu bainayenu kwa batili ila itakapokuwa ni (mali ya ) biashara kwa kuridhiana kati yenu. Wala msijiue, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye rehema kwenu.
30. Na mwenye kufanya hili kwa uadui na dhulma basi tutamtia Motoni, na hilo ni jepesi kwa Mwenyeezi Mungu.
31. Kama mkijiepusha na maovu makubwa mnayokatazwa, tutawafutieni makosa yenu, na tutawaingizeni mahala patukufu.
32. Wala nisitamani vile ambavyo Mwenyeezi Mungu amewafadhili baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walichokichuma, na
wanawake wanafungu katika walichokichuma. Na muombeni Mwenyeezi Mungu katika fadhila yake, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
33. Na kila mmoja tumemuwekea warithi wa yale waliyoyaacha wazazi wawili na jamaa (zake) na wale mnaofungamana nao ahadi, basi wapeni fungu lao, hakika Mwenyeezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
34. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake kwa sababu Mwenyeezi Mungu amewafadhili baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali yao waliyoyatoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii wanaojilinda (hata) asipokuwapo (waume zao) yale aliyohifadhi Mwenyeezi Mungu. Nawanawake ambao mnaogopa uasi wao, basi waonyeni na waacheni peke yao katika vitanda, na wapigeni. Watakapowatii, basi msiwatafutie njia (ya kuwaudhi) hakika Mwenyeezi Mungu ni Mtukufu, Mkuu.
35. Na mtakapochelea kuwapo mfarakano baina yao,basi pelekeni mwamuzi katika watu wa mume na mwamuzi katika watu wa mke. Kama wote wawili wakitaka mapatano, Mwenyeezi Mungu atawawezesha, Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye khabari.
36. Na Mwabuduni Mwenyeezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa wa karibu, na mayatima na masikini na jirani wa karibu (katika koo) na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni, na msafiri, na waliomilikiwa na mikono yenu. Hakika Mwenyeezi Mungu hampendi mwenye kiburi, ajivunaye.
37. Ambao hufanya ubakhili na huwaamuru watu kufanya ubakhili na kuyaficha aliyowapa Mwenyeezi Mungu katika fadhili yake, na tumewaandalia makafiri adhabu venye kudhalilisha.
38. Na ambao hutoa mali yao kwa ajili ya kuonyesha watu, wala hawamwainini Mwenveezi Mungu wala siku ya Mwisho, na ambaye shetani ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya.
39. Na ingekuwa nini juu yao kama wangelimwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya mwisho na wakatoa katika alichowaruzuku Mwenyeezi Mungu? na Mwenyeezi Mungu anawajua sana.
40. Hakika Mwenyeezi Mungu hadhulumu (hata) uzani wa chembe, na kama likiwa ni tendo jema hulizidisha, na kutoa malipo makubwa kutoka kwake.
41. Basi itakuwaje tutakapoleta katika kila umati na tukakuleta wewe kuwa ni shahidijuu ya hawa?
42. Siku hiyo watatamani wale waliokufuru na wakamuasi Mtume lau kama ardhi isawazishwe juu yao, wala hawataweza kumficha Mwenyeezi Mungu neno lolote.
43. Enyi mlioamini! msikaribie swala hali ya kuwa mmelewa mpaka myajue mnayoyasema, wala mkiwa na janaba, isipokuwa mmo safarini, mpaka muoge. Na kama mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake, na msipopata maji, basi tayamamuni kwa mchanga safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kufuta madhambi.
44. Je, huwaoni wale waliopewa fungu katika kitabu, wananunua upotovu na kuwapendelea nyinyi mpotee njia?
45. Na Mwenyeezi Mungu anawajua sana maadui zenu, na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi, na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa ni Mwenye kunusuru!.
46. Miongoni mwa Mayahudi (wamo ambao) hubadilisha maneno kutoka mahala pake na wakasema: Tumesikia na tumeasi na sikia bila ya kusikilizwa, na (husema) Raainaa kwa kuligeuza kwa ndimi zao, na kuitukana dini. Na kama wao wangesema: Tumesikia na tumetii, na usikie na utuangalie ingekuwa ni kheri kwao na vizuri zaidi. Lakini Mwenyeezi Mungu amewalaani kwa kufru zao, basi hawaamini ila kidogo tu.
47. Enyi ambao mliopewa Kitabu! yaminini tuliyoyateremsha yenye kusadikisha mliyonayo kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au tukawalaani kama vile tulivyowalaani watu wa Jumamosi. Na kwa hakika amri ya Mwenyeezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kufanywa.
48. Hakika Mwenyeezi Mungu hasamehi kushirikishwa naye, na husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyeezi Mungu, bila shaka amezusha dhambi kubwa.
49. Je, huwaoni wale wajitakasao nafsi zao? Bali Mwenyeezi Mungu humtakasa amtakae, wala hawatadhulumiwa hata kidogo.
50. Tazama namna wanavyotunga uongo juu ya Mwenyeezi Mungu, na linatosha hilo kuwa ni dhambi iliyo wazi.
51. Je, huwaoni wale waliopewa fungu katika Kitabu, wanaamini sanamu na shetani, na wakiwasema wale waliokufuru kuwa; Hao wameongoka zaidi katika njia kuliko walioamini.
52. Hao ndio Mwenyeezi Mungu amewalaani, na ambaye amelaaniwa na Mwenyeezi Mungu basi hutampatia mwenye kumnusuru.
53. Au wanayo sehemu ya ufalme? basi hapo wasingeliwapa watu hata kolwa.
54. Au wanawahusudu watu kwa yale aliyowapa Mwenyeezi Mungu katika fadhili yake? basi bila shaka tuliwapa watoto wa Ibrahimu Kitabu na hekima, na tukawapa ufalme mkubwa.
55. Basi yuko miongoni mwao anayemwamini, na yuko miongoni mwao anayejiepusha naye, na Jahannam yatosha kwa kuunguza.
56. Hakika wale waliozikataa Aya zetu, karibuni tutawaingiza Motoni kila zitakapoiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyingine ili wapate onja adhabu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
57. Na wale walioamini na kufanya vitendo vizuri karibuni tutawaingiza katika Mabustani yapitayo mito chini yake, watakaa humo milele, humo watakuwa na wake waliotakaswa, na tutawaingiza katika kivuli cha daima.
58. Hakika Mwenyeezi Mungu anawaamuruni kuwatekelezea amana zao wenyewe, na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
59. Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyeezi Mungu na mtiini Mtume na Wenye mamlaka katika nyinyi, na kama mkigombana katika jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume ikiwa mnamwamini Mwenyeczi Mungu na siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na ni lenye mwisho mzuri zaidi. 60. Je, hukuwaona wale wanaodai kuwa wao wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa shetani hali wameamrishwa kumkataa. na shetani anataka kuwapoteza upotovu wa mbali.
61. Na wanapoambiwa: Njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu na kwa Mtume, utawaona wanafiki wanajizuilia na kukupa mgongo.
62. Basi inakuwaje unapowafikia msiba kwa sababu ya yale yaliyotangulizwa na mikono yao, kisha wanakujia wakiapa kwa Mwenyeezi Mungu (wakisema). Hatukutaka ila wema na mapatano.
63. Hao ndio ambao Mwenyeezi Mungu anayajua yaliyomo nyoyoni mwao, basi waache, na uwape mawaiclha na uwaambie maneno yatakayoingia katika nafsi zao.
64. Na hatukumpeleka Mtume yeyote ila apate kutiiwa kwa amri ya Mwenyeezi Mungu. Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyeezi Mungu, na Mtume akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyeezi Mungu, Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
65. Naapa kwa Mola wako! hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu (wao) katika yale waliyokhitilafiana kati yao, kisha wasione dhiki nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyotoa na wanyenyekee kabisa.
66. Na kama tungewaamrisha; Jiueni, au tokeni katika miji yenu, wasingelifanya hayo isipokuwa wachache katika wao. Na lau kama wangelifanya yale waliyoagizwa, ingekuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi.
67. Na hapo tungewapa malipo makubwa yatokayo kwetu.
68. Na tungewaongoza njia iliyonyooka.
69. Na wenye kumtii Mwenyeezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyeezi Mungu, miongoni mwa Manabii, na Masiddiki, na Mashahidi na Watu wema. na hao ndio marafiki wema.
70. Hiyo ni fadhili itokayo kwa Mwenyeezi Mungu, na anatosha Mwenyeezi Mungu kuwa Mjuzi.
71. Enyi mlioamini shikeni hadhari yenu, na tokeni kundi moja moja au tokeni nyote pamoja.
72. Na hakika katika nyinyi yuko anayekawia, na ukiwapateni msiba, husema: Hakika Mwenyeezi Mungu amenineemesha nilipokuwa sikuhudhuria pamoja nao.
73. Na kama ikiwafikieni fadhila itokayo kwa Mwenyeezi Mungu, husema:
Kama kwamba hapakuwa na mapenzi baina yenu na baina yake, laiti ningekuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa.
74. Basi wapigane katika njia ya Mwenyeezi Mungu wale wanaouza maisha (yao) ya dunia kwa Akhera. Na anayepigana katika njia ya Mwenyeezi Mungu akauwawa au akashinda, basi hivi karibuni tutampa malipo makubwa.
75. Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyeezi Mungu na ya wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto ambao husema: Mola wetu! tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na utujaalie mlinzi kutoka kwako, na utujaalie msaidizi kutoka kwako.
76. Wale walioamini wanapigana katika njia ya Mwenyeezi mungu na wale waliokufuru wanapigana katika njia ya shetani, basi piganeni na marafiki za shetani, hakika hila za shetani ni dhaifu.
77. Je, huwaoni wa1e walioambiwa: Zuieni mikono yenu, na simamisheni swala na mtoe zaka walipolazimishwa kupigana, mara kundi moja katika wao wakawaopa watu kama kumuogopa Mungu au kwa khofu zaidi, na wakasema: Mola wetu! mbona umetulazimi sha kupigana? kwa nini hukutuakhirisha mpaka muda ulio karibu? Waambie: Starehe ya ulimwenguni ni kidogo, na Akhera ni hora kwa wenye kumcha Mwenyeezi Mungu wala hamta dhulumiwa hata kidogo.
78. Popote mtakapokuwa yatawafikia mauti, na ingawa muwe katika ngome zilizo na nguvu. Na likiwafikilia jema husema: Hili limetoka kwa Mwenyeezi Mungu. Na likiwafikilia ovu husema: Hili limetoka kwako. Waambie yote yametoka kwa Mwenyeezi Mungu, basi wana nini watu huwa hawawezi kufahamu maneno?
79. Wema uliokufikia umetoka kwa Mwenyeezi Mungu, na ubaya uliokufikia basi umetoka kwako mwenyewe. Tumekupeleka kwa watu kuwa ni Mtume, na atosha Mwenyeezi Mungu kuwa ni Mwenye kushuhudia.
80. Mwenye kumtii Mtume basi amemtii Mwenyeezi Mungu, na mwenye kukataa, basi hatukukupeleka kuwa ni mwenye kuwalinda.
81. Na wanasema: Tumetii, wanapotoka mbele yako kundi moja miongoni mwao linashauriana usiku kinyume cha yale uliyoyasema. Na Mwenyeezi Mungu huyaandika wanayoshauriana usiku basi waache, na mtegemee Mwenyeezi Mungu, na atosha Mwenyeezi Mungu kuwa Mlinzi.
82. Je, hawaizingatii Our'an? na kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenveezi Mungu, bila shaka wangekuta ndani yake khitilafu nyingi.
83. Na linapo wafikia jambo lolote la amani au khofu hulitangaza, (hivyo msifanye) na kama wangelipeleka kwa mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, bila shaka wangelijua wale wanaochunguza katika wao.Na kama isingelikuwa fadhila ya mwenyezi mungu juu yenu na rehma yake mmngefuata shetani isipokuwa wachache.
84. Basi pigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, hukukalifishwa ila nafsi yako. na uwahimize wenye kuamini, huenda Mwenyeezi Mungu akazuia mashambulio ya wale waliokufuru, na Mwenyezi Mungu ndie Mkali wa kushambulia na Mkali wa kuadhibu.
85. Mwenye kuunga mkono jambo zuri, hupata fungu katika hayo.Na mwenye kuunga mkono jambo baya, hupata hisa katika hayo. Na Mwenyeezi Mungu Mwenye uweza juu ya kila kitu.
86. Na mnaposalimiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au mrejeshe hayo hayo. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuhesabu kila jambo.
87. Mwenyeezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye tu. Kwa hakika atawakusanya siku ya Kiyama, halina shaka hilo na ni nani mkweli zaidi katika maneno kuliko Mwenyeezi Mungu?
88. Basi mna nini nyinyi mmekuwa makundi mawili katika khabari ya wanafiki, na hali Mwenyeezi Mungu amewapindua kwa yale waliyoyachuma? Je, mnataka kumuongoza ambaye Mwenyeezi Mungu amemhukumu kupotea? Na ambaye Mwenyeezi Mungu amemwacha katika upotovu, hutampatia njia (ya uongofu).
89. Wanapenda lau mngekufuru kama walivyokufuru mkawa sawa sawa (nao). Basi msiwafanye baadhi yao kuwa Viongozi mpaka wahame katika njia ya Mwenyeezi Mungu, na kama wakikataa, basi wakamateni na waueni popote mnapowapata wala msifanye Viongozi katika wao wala msaidizi.
90. Isipokuwa wale wanaopatana na watu ambao mna ahadi baina yenu na wao, au wakawajia hali ya kuwa wanaona dhiki nyoyo zao kupigana na nyinyi au kupigana na watu wao. Na Kama Mwenyeezi Mungu angependa angewasaliti nao wakapigana nanyi, basi watakapojitenga nanyi, wasipigane nanyi, na wakawapa amani, basi Mwenyeezi Mungu hakuwafanyieni njia juu yao (ya kuwapiga).
91. Mtawakuta wengine wanaotaka amani kwenu na amani kwa watu wao, kila wakirudishwa kwenye fitina hudidimizwa humo, basi wasipojitenga nanyi, wakijitolea kwa amani, na wakazuia mikono yao, basi wakamateni na muwauwe popote mnapowapata Na hao ndio ambao tumewafanyia hoja zilizo wazi juu yao.
92.Na haimpasi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa bahati mbaya. Na mwnye kumuuwa Muumini kwa bahati mbaya, hasi amwache huru mtumwa aliye amini, na atoe (pia)malipo kwa warithi wake ila watakapoifanya sadaka (wao wenyewe) na akiwa aliyeuawa ni mmoja wa watu walio maadui zenu, naye (mwenye kuuwa) ni muumini, basi amwache huru mtumwa alieamini. Na ambae hakupata basi afunge saumu miezi miwili inayofuatana ili kutubia kwa mwenyezi mungu, na mwenyeezi mungu ni mjuzi, mwenye hekima.
93. Na Mwenye kumuua Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atakaa milele, na Mwenyeezi Mungu amemghadhabikia na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.
94. Enyi mlioamini! mtakaposafiri katika njia ya Mwenyeezi Mungu basi pelelezeni, wala msimwambie mwenye kuwapa salamu: Wewe si muumini, mnataka mafao ya dunia, na kwa Mwenyezi Mungu kuna neema nyingi. Hivyo ndivyo mlivyokuwa zamani, na Mwenyeezi Mungu amewafanyieni hisani, basi chunguzeni, hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale mnayoyatenda.
95. Hawawi sawaWaumini wale wenye kukaa, isipokuwa wenye udhuru, na wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyeezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyeezi Mungu amewatukuza katika cheo wenye kupigana jihadi kwa mali yao na nafsi zao kuliko wenye kukaa. Na Mwenyeezi Mungu amewaahidi wote (kupata) wema, lakini Mwenyeezi Mungu amewatukuza kwa malipo makubwa wenye kupigana jihadi kuliko wenye kukaa.
Hakika nyinyi mnaogopwa zaidi katika nyoyo zao kuliko (wanavyomuogopa) Mwenyeezi Mungu. Haya ni kwa sababu wao ni watu wasiofahamu." 59:13
96. (Ni) vyeo vitokavyo kwake, na msamaha na rehema, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
97. Hakika wale ambao wametolewa roho na Malaika hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao (Malaika) watawaambia: Mlikuwa wapi? Watasema:
Tulikuwa wanyonge (huko) ardhini. (Malaika) watasema: Je, ardhi ya Mwenyeezi Mungu haikuwa na wasaa mkahamia humo? Basi hao makazi yao ni jahannam, nayo ni marudio mabaya.
98. Isipokuwa wale wanyonge katika wanaume, na wanawake, na watoto wasio na uwezo wa hila yoyote wala hawaoni njia (ya kuokoka).
99. Basi hao huenda Mwenyeezi Mungu akawasamehe, na hakika Mwenyeez! Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kufuta madhambi.
100. Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyeezi Mungu, atapata mahala pengi ardhini pa kukimbilia na wasaa, na anayetoka katika nyumba yake ili kuhamia kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti, basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
101. Na mnaposafiri katika ardhi, basi si vibaya kwenu kama mkifupisha swala, iwapo mkiogopa ya kwamba wale waliokufuru watakupeni taabu. Hakika makafiri ni maadui wenu walio wazi.
102. Na unapokuwa parnoja nao ukawaswalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao, na (watakapomaliza) kusujudu basi wawe nyuma yenu, na lije kundi jingine ambao hawajaswali kisha waswali pamoja nawe, na washike hadhari yao na silaha zao. Wanapendelea wale waliokufuru kama mtasahau silaha zenu na vifaa vyenu wapate kuwavamia mvamio mmoja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua, au rnkawa wagonjwa, kuziweka silaha zenu. Na shikeni hadhari yenu, hakika Mwenyeezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
103. Basi mtakapomaliza swala, basi mtajeni Mwenyeezi Mungu kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala kwa mbavu zenu. Na mtakapopata amani, basi simamisheni swala. Hakika swala kwa wenye kuamini ni faradhi iliyo na wakati maalurnu.
104. Wala msidhoofike katika kuwafuatia watu hao (makafiri) mkiwa mnaumia, basi na wao wanaumia kama muumiavyo (nyinyi). Na mnataraji kwa Mwenyeezi Mungu ambayo hawataraji wao. Na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
105. Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kama alivyokufahamisha Mwenyeezi Mungu, wala usiwe mtetezi wa wafanyao khiyana.
106. Na muombe msamaha Mwenyeezi Mungu hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
107. Wala usiwatetee wale wanaozikhini nafsi zao, hakika Mwenyeezi Mungu hampendi aliyekhaini, mwenye dhambi.
108. Wanajificha kwa watu wala hawamstahi Mwenyeezi Mungu, naye yu pamoja nao wanaposhauriana usiku kwa maneno asiyoyapenda na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema wayatendayo.
109. Nyinyi ndio ambao mliwatetea katika maisha ya dunia, basi ni nani atakayemjadili Mwenyeezi Mungu siku ya Kiyama kwa ajili yao, au ni nani atakayekuwa mlinzi juu yao?
110. Na mwenye kutenda ovu na akaidhulumu nafsi yake, kisha akaomba msamaha kwa Mwenyeezi Mungu, atamkuta Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
111. Na mwenye kuchuma dhambi, anajichumia mwenyewe, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
112. Na mwenye kuchuma kosa au dhambi, kisha akamsingizia nayo asiye na kosa, basi kwa hakika amebeba uongo na dhambi iliyo wazi.
113. Na kama si fadhila ya Mwenyeezi Mungu juu yako na rehema yake, bila shaka kundi moja katika hao lingekusudia kukupoteza, wala hawazipotezi ila nafsi zao wala hawatakudhuru chochote. Na Mwenyeezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hekima, na amekufundisha yale uliyokuwa huyajui, na hakika fadhila ya Mwenyeezi Mungu juu yako ni kubwa.
114. Hakuna kheri katika mengi wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa (mashauri ya ) mwenye kuamrisha (kutoa) sadaka au (kufanya) wema au kusuluhisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyeezi Mungu basi hivi karibuni tutampa malipo makubwa.
115. Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannam. Na (hayo) ni marejeo maovu.
116. Hakika Mwenyeezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, na husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye, na mwenye kumfanyia mshirika Mwenyeezi Mungu, basi amepotea upotevu wa mbali.
117. Hawawaombi badala yake ila (masanamu) ya kike, na hawamwambudu ila shetani aliyeasi.
118. (Ambaye) Mwenyeezi Mungu amemlaani. Na amesema (shetani) kwa hakika nitajifanyia katika waja wako fungu maalumu.
119. Na bila shaka nitawapoteza, na nitawatia tamaa, na nitawaamrisha, basi watayapasua masikio ya wanyama, na nitawaamrisha (tena) basi wataigeuza dini ya Mwenyeezi na mwenye kumfanya shetani kuwa kiongozi badala ya Mwenyeezi Mungu, basi amekhasiri khasara iliyo wazi.
120. (Shetani) anawaahidi na kuwatia tamaa, na shetani hawaahidi ila udanganyifu.
121. Hao makazi yao ni Jahannam, wala hawatapata pa kukimbilia.
122. Na wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, tutawatia katika Pepo zenye kupita mito chini yake, watakaa humo milele, (ni) ahadi ya Mwenyeezi Mungu iliyo kweli na ni nani msema kweli zaidi kuliko Mwenyeezi Mungu.
123. Si kwa matamanio yenu wala matamanio ya watu wa Kitabu, anayefanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatapata mlinzi wala msaidizi kwa ajili yake badala ya Mwenyeezi Mungu.
124. Na mwenye kufanya mema, mume au mke, hali yakuwa ni mwenye kuamini, basi hao wataingia Pepo wala hawatadhulumiwa hata kidogo.
125. Na ni nani mwenye dini nzuri kuliko yule ambaye ameuelekeza uso wake kwa Mwenyeezi Mungu, naye ni mwenye kutenda mema na anafuata mila ya Ibrahimu mwenye kushikamana na haki, na Mwenyeezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa rafiki.
126. Na ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kukijua kila kitu.
127. Na wanakuuliza yanayowahusu wanawake, waambie Mwenyeezi Mungu anawaambieni habari zao, na msomewavyo katika Kitabu juu ya wanawake yatima ambao hamuwapi walichoandikiwa, na mnapenda kuwaoa, na watoto wanyonge, na kuwasimamia yatima kwa uadilifu, na wema wowote mnaofanya, basi Mwenyeezi Mungu anaujua.
128. Na kama mke akiogopa kwa mume wake kutomjali au kumpa nyongo, basi si vibaya kwao kusikilizana kwa sulhu baina yao, na sulhu ni bora. Na nafsi zimewekewa tamaa (mbele yao) na mtakapotenda wema na mkajilinda (na kuwadhulumu wanawake) basi Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi kwa mnayoyatenda.
129. Na hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, japokuwa mtajitahidi. Basi msielekee (upande mmoja) kabisa kabisa mkamwacha (huyu mwingine) kama aliyetundikwa. Na mtakapotengeneza na mkajilinda (na dhulma) basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehernu.
130. Na kama wakitengana, Mwenyeezi Mungu atamstawisha kila mmoja wao kwa wasaa wake, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye hekima.
131. Na ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na kwa hakika tuliwaagiza waliopewa Kitabu kabla yenu, na nyinyi (pia) kwamba: Mcheni Mwenyeezi Mungu. Na kama mkikataa, basi ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyeezi Mungu ni Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
132. Na ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyombo ardhini, na anatosha Mwenyeezi Mungu kuwa mlinzi.
133. Akitaka atawaondoeni, enyi watu! na alete wengine, na Mwenyeezi Mungu ni Muweza wa hilo.
134. Anayetaka malipo ya dunia, basi yako kwa Mwenyeezi Mungu malipo ya dunia na ya Akhera, na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
135. Enyi mlioamini! kuweni wenye kusimamia uadilifu mtoe ushahidi kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au (juu ya) wazazi (wenu) na jamaa wa karibu. Awe tajiri au masikini Mwenyeezi Mungu anawastahikia zaidi wote wawili. Basi msifuate matamanio mkaacha kufanya uadilifu. Na kama mkipotoa (ukweli) au mkijitenga, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yale mnayoyatenda.
136. Enyi mlioamini! mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha zamani. Na mwenye kumkataa Mwenyeezi Mungu na Malaika wake na Vitabu vyake na Mitume wake na siku ya Mwisho basi bila shaka amepotea upotevu wa mbali.
137. Hakika wale walioamini kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakakufuru, kisha wakazidi kukufuru, Mwenyeezi Mungu hatawasamehe wala hatawaongoza njia.
138. Waambie wanafiki ya kwamba watapata adhabu iumizayo.
139. Ambao huwafanya makafiri kuwa viongozi badala ya wenye kuamini. Je, wanataka kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyeezi Mungu.
140. Na amekwisha wateremshia katika Kitabu ya kwamba mnaposikia Aya za Mwenyeezi Mungu zinakataliwa na kufanyiwa mzaha, basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine (mtakapokaa) nanyi mtakuwa kama wao. Hakika Mwenyeezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika jahannam.
141. Amhao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyeezi Mungu huwaambia: Je hatukuwa pamoja nanyi? na kama makafiri wangepata fungu (la ushindi) huwaambia: Je, hatukuwashindeni na kuwakinga na waumini? Basi Mwenyeezi Mungu atahukumu baina yenu siku ya Kiyama, na Mwenyeezi Mungu hatawajaalia makafiri njia ya kuwashinda wenye kuamini.
142. Hakika wanafiki wanataka kumdanganya Mwenyeezi Mungu, naye atawaadhibu kwa sababu ya udanganyifu wao. Na wanaposimama kuswali, husimama kwa uvivu, kujionyesha kwa watu, wala hawamtaji Mwenyeezi Mungu ila kidogo tu.
143. Wanayumbayumba huku na huku, huku hawako wala huku hawako. Na ambaye Mwenyeezi Mungu ainemwacha katika upotovu, basi huwezi kumpatia njia (ya uongofu).
144. Enyi mlioamini! msiwafanye makafiri kuwa viongozi badala ya Waumini. Je, mnataka kumfanyia Mwenyeezi Mungu hoja iliyo wazi juu yenu?
145. Hakika wanafiki watakuwa kalika tabaka ya chini kabisa (huko) Motoni, wala hutawapatia mwenve kuwanusuru.
146. Isipokuwa wale waliotubu na kujisahihisha na wakashikamana na Mwenyeezi Mungu, na wakamtakasia utii wao kwa Mwenyeezi Mungu, basi hao wako pamoja na wenye kuamini. Na Mwenyeezi Mungu atawapa wenye kuamini malipo makubwa.
147. Mwenyeezi Mungu hakuadhibuni kama mtashukuru na mtaamini, na Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani, Mjuzi.
148. Mwenyeezi Mungu hapendi kelele za maneno mabaya, ila kwa mwenye kudhulumiwa. Na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusikia, Mjuzi.
149. Mkidhihirisha wema au mkiuficha au mkiyasamehe maovu, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Muweza.
150. Hakika wale wanaomkataa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na wanataka kutenga baina ya Mwenyeezi Mungu na Mitume wake, na wakasema: Wengine tumewaamini na wengine tunawakataa, na wanataka kushika njia iliyo kati ya haya.
151. Hao ndio makafiri kweli, na tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
152. Na waliomwamini Mwenyeezi Mungu na Mitume wake wala hawakumfarakisha mmojawapo kati yao, hao atawapa malipo yao. Na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
153. Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshie Kitabu kutoka mbinguni. Hakika walimuomba Musa makubwa kuliko hayo wakasema: Tuonyeshe Mwenyeezi Mungu waziwazi, ikawashika ngurumo (ya radi) kwa sababu ya dhulma yao, kisha wakamfanya mwana ng'ombe (kuwa mungu) baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi. Tukasamehe hayo, na tukampa Musa nguvu zilizo dhahiri.
154. Na tukauinua mlima juu yao kwa ajili ya ahadi yao, na tukawaambia:
Ingieni mlangoni kwa unyenyekevu, na tukawaambia: Msiivunje siku ya Jumamosi na tukachukua kwao ahadi madhubuti.
155. Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao, na kuzikataa kwao dalili za Mwenyeezi Mungu, na kuua kwao Manabii bila ya haki, na kusema kwao Nyoyo zetu zina vizibo, bali Mwenyeezi Mungu amezipiga mihuri kwa sababu ya kufru zao, basi hawataamini ila wachache tu.
156. Na kwa kufru zao na kumsingizia kwao Mariam uongo mkubwa.
157. Na kusema kwao Hakika tumemuua Masihi Isa mwana wa Mariam, Mtume wa Mwenyeezi Mungu, wala hawakumuua wala hawakumsulubu, lakini alifananishwa kwao. Na hakika ambao wamekhitilafiana katika khabari yake wana shaka nayo, hawana ujuzi wowote ila kufuata dhana tu, wala hawakumuua kwa yakini.
158. Bali Mwenyeezi Mungu alimnyanyua kwake, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
159. Na hakuna yeyote katika watu wa Kitabu ila humwamini yeye (Isa) kabla ya kufa kwake, na siku ya Kiyama atakuwa (Isa) shahidi juu yao.
160. Basi kwa dhulma ya Mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa, na kwa sababu ya kuzuilia kwao (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu kwa wingi.
161. Na kwa kuchukua kwao riba na hali wamekatazwa, na kula kwao mali ya watu kwa batili, na tumewaandalia makafiri katika wao adhabu iumizavo.
162. Lakini waliobobea katika elimu miongoni mwao, na wenye kuamini, wanaamini yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako, na wenye kusimamisha swala na wenye kutoa zaka na wenye kumwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, hao ndio tutawapa malipo makubwa.
163. Hakika tumekuletea Wahyi kama tulivyompelekea Wahyi Nuhu na Manabii baada yake. Na tulimpelekea Wahyi Ibrahim na Ismaifi na Is’haka na Yaakub na Makabila na Isa na Ayub na Yunus na harun na Suleiman na Dawuud tukampa Zaburi.
164. Na (tukawapeleka) Mitume tuliokuhadithia zamani na Mitume (wengine) ambao hatukukuhadithia, na Mwenyeezi Mungu akasema na Musa kwa maneno.
165. Mitume, watoao habari nzuri na waonyao ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyeezi Mungu baada ya Mitume, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
166. Lakini Mwenyeezi Mungu anayashuhudia aliyokuteremshia, ameyateremsha kwa elimu yake, na Malaika (pia) wanashuhudia na anatosha Mwenyeezi Mungu kuwa Shahidi.
167. Hakika wale waliokufuru na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu bila shaka wamepotelea mbali sana.
168. Hakika wale waliokufuru na kudhulumu hakuwa Mwenyeezi Mungu awasamehe wala awaongoze njia.
169. Isipokuwa njia ya Jahannam, watakaa humo milele na hakika hilo kwa Mwenyeezi Mungu nijepesi.
170. Enyi watu! bila shaka amewafikieni Mtume kwa haki kutoka kwa Mola wenu, basi aminini, ni bora kwenu, na kama mtakataa, basi ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima.
171. Enyi watu wa Kitabu! msiruke mipaka ya dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyeezi Mungu ila lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Mariam ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu na ni neno lake tu alimpelekea Mariam, na ni roho itokayo kwake. Basi mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, wala msiseme watatu, wacheni (itikadi hiyo) ni bora kwenu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mmoja tu, ameepukana na kuwa na mtoto. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi,
172. Masihi hataona unyonge kuwa mtumwa wa Mwenyeezi Mungu wala Malaika waliokurubishwa, na atakayeona unyonge kumtii na akatakabari, basi atawakusanya wote kwake.
173. Ama wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, basi atawapa malipo yao na atawazidishia katika fadhila yake. Ama wale walioona unyonge na kufanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu yenye kuumiza, wala hawatapata kiongozi wala msaidizi yeyote badala ya Mwenyeezi Mungu.
174.Enyi watu! bila shaka imewafikieni dalili kutoka kwa Mola wenu, na tumewateremshia Nuru iliyo wazi.
175. Ama wale waliomwamini Mwenyeezi Mungu na wakashikamana naye, atawatia katika rehema itokayo kwake na fadhila (yake) na atawaongoza kwake kwa njia iliyonyooka.
176. Wanakuuliza; Waambie: Mwenyeezi Mungu anawapeni hukumu juu ya mkiwa, kama mtu amekufa wala hana mtoto, na anaye ndugu wa kike, basi ana nusu ya alichokiacha (marehemu) naye atamrithi (dada yake) ikiwa hana mtoto. Na kama wao ni (madada) wawili basi watapata thuluthi mbili katika alichokiacha. Na iwapo ni ndugu wa kiume na wakike, basi mwanamume atapata fungu la wanawake wawili. Mwenyeezi Mungu anawabainishieni ili msipotee, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.