Abdullah ibn Abbas (r.a.) amesema kuwa baada ya kumaliza Hajj ya mwisho (mwaka wa 10 Hijriyyah), Mtume Mtukufu s.a.w.w. alisimama mbele ya mlango wa Ka'aba Tukufu, akiwa ameshikilia komeo ya mlango, huku akiwauliza ma-Sahaba wake: "Je, nikuambieni dalili za siku ya QIYAMA?" Salman Farsi (r.a.) ambaye alikuwa karibu naye, alisema:"Ndiyo, Ewe Mtume wa Allah swt."
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema, "Hakika,miongoni mwa dalili za saa, ni kuwa (1) watu watapuuza sala, (2) watafuata matamanio yao wenyewe (3) wataelekeza kujipendelea wao wenyewe, watawaheshimu matajiri, (4) na watauza Dini yao kwa manufaa ya kidunia (5) wakati huo roho na moyo wa Muumin itayayuka (kwa huzuni) kama chumvi inavyoyayuka katika maji, kwa sababu ataona mambo yaliyoharamishwa na hataweza kuyabadili."
Salman akasema: "Haya yatatokea, ewe Mtume wa Allah swt?"
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema: "Ndiyo, naapa kwa Aliyonayo roho yangu mkononi mwake."
"Ewe Salman, (6) wakati huo watawala watakuwa wadhalimu (7) Mawaziri watakuwa waasi, (8) na wadhamini (wale waliopewa amana kwa kuaminiwa) watafanya hiana, (9) hakika wakati huo maovu yatakuwa mema na mema yatakuwa maovu, (10) wale wafanyao hiana wataaminiwa na waaminifu watafikiriwa kuwa si waaminifu;na mwongo atasadikiwa,na msema kweli atahesabiwa mwongo. (11) Wakati huo kutakuwapo na utawala wa wanawake, (12) Masuria watashauriwa, (13) na watoto watakaa juu ya mimbar, (14) udanganyifu utahesabiwa kuwa ni uerevu (15) na Zaka itakuwa ni kama kutozwa faini;na mateka ya vita (yaani mali ya ummah) yatakuwa kama ni mali ya mtu binafsi; na mtu atakuwa mjeuri kwa wazazi wake na atakuwa mwema kwa marafiki zake, (16) na wakati huo kutatokea na nyota zenye mikia (comets)."
Salman akasema: "Haya yatatokea, ewe Mtume wa Allah swt?"
Mtume Mtukufu s.a.w.w. akasema: "Ndiyo, naapa kwa Aliyonayo roho yangu mkononi mwake."
"Ewe Salman! (17) wakati huo mwanamke atakuwa mshiriki wa mumewe katika biashara, (18) na mvua itakuwa moto sana (19) na watu wema watabaki katika huzuni; na masikini hawata heshimiwa; na wakati huo masoko yatakaribiana, (20) Tena huyu atasema,"Mimi sikuuza chochote, na yule atasema, "Mimi sikupata faida yoyote." Kwa hivyo hutamkuta mtu yeyote asiyemlalamikia Allah swt.
"Ewe Salman! (21) tena itatokea iwapo watu watawazungumzia watawala wao, watawaua, na ikiwa watanyamaza kimya, watanyang'anywa mali yao, watanyimwa heshima zao, watamwaga damu yao na mioyo ya watu itajaa woga;kisha hutamwona mtu yeyote ila atakuwa mwoga,mwenye khofu, ametishika na ameshstushwa"
"Ewe Salman! (22) Bila shaka wakati huo mambo fulani yataletwa kutoka Mashariki (23) na mambo fulani yataletwa kutoka Magharibi, (24) Basi ole kwa watu walio dhaifu (wa imani) katika Ummah wangu kutokana na hayo; Ole ya Allah swt iwe kwa hayo. Wao hawatakuwa na huruma juu ya wadogo wao, wala hawatamsamehe yeyote aliyefanya kosa. Miili yao itakuwa ya wanadamu, lakini mioyo yao itakuwa ya mashetani."
"Ewe Salman! (25) Wakati huo wanaume watawaashiki wanaume, (26) na wanawake watawaashiki wanawake; (27) na watoto wa kiume watapambwa kama wanawake; (28) na wanaume watajifanya kama wanawake(29) na wanawake wataonekana kama wanaume; (30) na wanawake watapanda mipando (31) Hapo tena patakuwepo laana ya Allah swt juu ya wanawake wa Ummah wangu."
"Ewe Salman! (32) Bila shaka wakati huo Misikiti itapambwa (kwa dhahabu n.k.) kama inavyofanywa katika masinagogi na makanissa, (33) na Quran zitapambwa (kwa nakshi na rangi za kupendeza n.k.) (34) na minara (ya misikiti) itakuwa mirefu; na safu za watu wanaosimama katika sala zitazidi, lakini nyoyo zao zitachukiana na maneno yao yatatofautiana."
"Ewe Salman! (35) Wakati huo wanaume watatumia mapambo ya dhahabu; kisha watavaa hariri,na watatumia ngozi za chui."
"Ewe Salman! (36) Wakati huo riba itakuwako, (37) na watu wata-fanyia biashara kwa kusemana na rushwa (38) na dini itawekwa chini, na dunia itanyanyuliwa juu."
"Ewe Salman! (39) Wakati huo talaqa zitazidi (40) na mipaka ya Allah swt hayatasimamishwa (41) Lakini hayo hayatamdhuru Allah swt."
"Ewe Salman! (42) Wakati huo watatokea wanawake waimbaji, (43) na ala za muziki (44) na wabaya kabisa watawatawala Ummah wangu."
"Ewe Salman! (45) Wakati huo matajiri katika Ummah wangu watakwenda Kuhiji kwa matembezi, na walio wastani kwa biashara, na masikini kwa kujionyesha. (46) Hivyo basi wakati huo watakuwapo watu ambao watajifundisha Quran si kwa ajili ya Allah swt na wataifanya Quran kama ala ya muziki. (47) Na watakuwapo watu ambao watasoma dini si kwa ajili ya Allah swt (48) na idadi ya wanaharamu itazidi (49) watu wataiimba Quran, (50) na watu watavamiana kwa uroho wa kidunia."
"Ewe Salman! (51) Haya yatatokea wakati heshima zitakapo- ondoka,na madhambi yatatendwa (52) na watu waovu watakuwa na uwezo juu ya watu wema, (53) na uongo utaenea na mabishano (matusi) yatatokea (54) na umasikini utaenea, (55) na watu watajiona kwa mavazi yao (56) na itakuwepo mvua wakati si wake (57) na watu watacheza dama, kamari na Ala za muziki, (58) na hawatapenda kuhimizana mema wala kukatazana maovu (59) na kwa ajili hali itakavyokuwa hata itafikia wakati huo kuwa Muumin atakuwa na heshima ndogo kuliko hata mjakazi (60) na wanaosoma na wanaotumia wakati wao katika kumwabudu Allah swt watalaumiana. (61) Hao ndio watu watakaoitwa wachafu na wanajisi katika Ufalme wa mbinguni."
"Ewe Salman! (62) Wakati huo matajiri hawataogopa chochote isipokuwa mtu masikini; hadi kwamba masikini wataendelea kuomba kati ya ijumaa mbili, na hawatamwona mtu yeyote wa kutia chochote mikononi mwao."
"Ewe Salman! (63) Wakati huo itazungumzwa Ruwaibidhah."
Salman akauliza: "Ni nini Ruwaibidhah ? Ewe Mtume wa Allah swt, baba na mama yangu wawe fidia kwako."
Mtukufu Mtume s.a.w.w. akajibu: (64) "Watu fulani watazungumza kuhusu mambo ya watu ambayo hayakuwahi kuzungumzwa namna hii zamani. (65) Tena baada ya muda mchache machafuko yatatokea duniani, na kila nchi itafikiri kuwa machafuko yapo katika nchi yao tu."
(66) "Watabaki katika hali hiyo kwa muda ambao Allah swt atapenda wabaki; (67) kisha ardhi itatapika vipande vya moyo wake dhahabu, fedha na madini mengineyo; (Hapo Mtume s.a.w.w.) alinyosha kidole chake penye nguzo, na akasema:"Kama hizi (kwa ukubwa), lakini siku hiyo dhahabu wala fedha hazitamsaidia mtu yeyote. Na hii ndiyo maana ya maneno ya Allah swt 'Hakika dalili Zake zimekuja.'
Zipo habari zingine zilizoelezwa katika vitabu vinginevyo kwa kupitia Jabir Ibn Abdullah Ansari, ambavyo ninazitaja:
"Ewe Salman! Wakati huo (1) Wazee watajitumbukiza katika mambo ya ushirikina na uchawi, (2) ghiba ndiyo itakuwa mazungumzo yenye kupendeza, (3) mali iliyopatikana kwa njia za haramu, itachukuliwa kama ndiyo neema, (4) wazee hawatakuwa na mapenzi ya wadogo na vile vile wadogo hawatawajali wazee na kuwaheshimu (5) Islam itabakia kwa jina tu kwani wafuasi wake hawatakuwa wakifuata maadili na maamrisho yake, (6) Kimbunga kikubwa cha rangi nyekundu kitatokezea mbinguni na kutaanguka mawe kutoka mbinguni (7) nyuso zitakuwa za kuchukiza (8) kutakuwa na mitetemeko na kuporomoka kwa ardhi kila mara.
Hapo Sahaba walimwuliza Mtume s.a.w.w., "Ewe Mtume wa Allah swt, je lini yatakapotokea hayo yote?" (pamoja na nishani na dalili za hapo juu, baadhi zimeongezeka hapa chini)
Mtume s.a.w.w. aliwajibu: (1) "Watu watakuwa watumwa wa shahwa au matamanio yao, (2) watu watakuwa walevi wa kupindukia kwani matumizi ya ulevi utakithiri na utakuwa ukipatikana kwa udhahiri bila ya watu kuona aibu ya aina yoyote, (3) Wanaume watakuwa wakiwatii wake zao, (4) jirani atakuwa wakiwaudhi na kuwatesa majirani wenzake, (5) Wakubwa hawatakuwa watu wenye huruma, mioyo yao itakuwa imejaa kwa maonevu, (6) vijana hawatakuwa na heshima (7) watu watajenga majumba imara na marefu mno, (8) wafanyakazi watadhulumiwa haki zao, (9) ushahidi wa kiuongo utachukuliwa kuwa wa kawaida, (10) ndugu atakuwa akimwonea wivu ndugu yake halisi (11)watu watakaokuwa wakifanya biashara kwa ushirika, basi watakuwa daima wakifikiriana mbinu za kumdhulumu mwenzake, (12) mambo ya zinaa yatakuwa kama kawaida kwani yatatendeka na kusikika pia.(13) ile mioyo ya kutaka kusaidia watu wengine itakuwa imetoweka, (14) Maasi na dhuluma itaongezeka kupita kiasi, (15) matumbo ya watu itachukuliwa kuwa ndiyo miungu yao,kwani hawatajali kiwevyo, ilimradi wapate chochote kile, (16) wanawake watakuwa wakitawala akili za wanaume na watakuwa wakiwaendesha wanaume vile watakavyo wao, (17) kutatokea Maulamaa au wanazuoni waovu kabisa kwani watajionyesha kuwa ni wacha Mungu na wenye ilimu, ambapo kwa hakika watakuwa waroho wa mali ya dunia tu."
Hapo Mtume Mtukufu s.a.w.w.liwaonya: "Kumbukeni,wakati kama huo utakapokuja, basi Allah swt atatumbukiza watu katika balaa za aina nne, (1) kutawaliwa na watawala dhalimu (2) ukame na vitu vya matumizi ya kila siku kuwa bei ghali yaani kupanda kwa maisha, (3) dhuluma za watawala (4) kuabudu miungu."
Sahaba waliposikia hayo walishtushwa na kuuliza: "Ewe Mtume wa Allah swt! Je kweli kuwa Mwislamu atakuwa akiabudu miungu na masanamu?"
Mtume s.a.w.w. aliwajibu: "Naam! Kwao mapesa yatakuwa kama miungu kwani watakuwa wakiziabudu kupindukia kiasi."
Kwa hakika sisi tunayashuhudia haya yote yakitokea ambayo Mtume s.a.w.w. amekwisha bashiri karibu karne kumi na nne zilizokwishapita. Imam Ali a.s. katika khutba yake ijulikanayo kama Al-Bayan anaelezea ubashiri kwa undani zaidi. Wasomaji wenye kutaka kupata habari zaidi wanaweza kutazama (1) Yanabi-ul-Muwaddah (2) Basharat-ul-Islam, Sayyid Mustafa Ali-Sayyid Haider al-Kazami, chapa ya Baghdad.
.