HADITHI ZISEMAZO KUWA ATAONEKANA

Anasimulia Abu Huraira katika Hadithi aliyoipokea kuwa: (siku ya kiyama) "Mwenyeezi Mungu atawaijia (watu) akiwa na sura tofauti na ile wanayomjua, awaambie: Mimi ndiyo Mola wenu. (Watu) watajibu:

Mwenyeezi Mungu atuepushe nawe, sisi tutabaki hapa hapa mpaka Mola wetu (tunayemjua) atufikie, na akija sisi tutamjua. Mara Mwenyeezi Mungu atawafikia kwa sura yake ile wanayomjua atasema: Mimi ni Mola wenu. Nao watajibu: (kweli) wewe ndiye Mola wetu, na watamfuata".

Taz: Sahihi Bukhari J. 4 Uk. 92

Sahihi Muslim J. 1 Uk. 86

Tafsirul Khazin J. 7 Uk. 137

Abu Huraira anaendelea kusimulia: "Watu walimuuliza Mtume (s.a.w.) 'Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu! Hivi tutamuona Mola wetu siku ya kiyama?' Mtume (s.a.w.) akajibu: 'Hivi mnapata pingamizi gani kwa kutazama mwezi wa siku kumi na tatu?'

Wakajibu: 'Hatupati pingamizi yoyote.' Mtume (s.a.w.) akauliza tena: 'Mnapata kizuizi gani kutazama jua ambalo halina mawingu?' Wakajibu: 'Hakuna kuzuizi chochote.' Mtume (s.a.w.) akawaambia: 'Basi ndivyo matakavyomuona".

Suhaybu anasimulia kuwa: Amesema Mtume kuwa:

"Watu wa peponi watakapoingia Peponi, Mwenyeezi Mungu atawauliza: 'Mnataka niwaongeze kitu gani?'

Watasema: 'Oh, umekwisha ng'arisha nyuso zetu, umetuingiza peponi na umetuepusha mbali na moto.' (Hapo) Pazia litaondolewa, eeh, hawajapewa kitu kilicho bora zaidi kuliko kumuona Mola wao. Kisha Mtume (s.a.w.) akasoma aya: "Wale waliofanya wema watapata wema na zaid". 10:26 Iliposemwa: (katika Aya iliyotangulia), "WAZIYADAH" maana yake, KUMUONA MWENYEEZI MUNGU"

Taz: At'targhib Wat'tarhib J. 4 Uk. 551