Tunaamini kuwa: "Mwenyeezi Mungu haweki sheria yoyote isipokuwa ina maslahi ndani yake. Kwa mantiq hii, Mtume (s.a.w.) asingehitaji kurudi mara zote hizo kwa ajili ya kupunguziwa. Kwa sababu kufanya hivyo ni kutaka sheria isiyo na maslahi, kama ambavyo sababu zilizompelekea Nabii Musa kutaka zipunguzwe Sala hamsini ni kushindwa kuzitekeleza sala hizo. Kama kwamba Nabii Musa anaamini kuwa Sheria hii (ya Sala hamsim) inakwenda kunyume na maslahi, na hilo ni muhali (haliwezekani) kwa Mwenyeezi Mungu. Aidha, vipi Mwenyeezi Mungu hakujua kuwa: Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.) hauwezi hilo, bali Musa yeye alijue hilo?? Au tuseme, ni takhfif kwa jambo lisilowezekana, vipi, Mwenyeezi Mungu anatwambia wakati wote: "Mwenyeezi Mungu huwatakieni yaliyo mepesi wala hawatakieni yaliyo mazito". 2: 185.
"Wala hakuweka juu yenu dhiki katika dini" 22:78. Na vipi Nabii Ibrahim hakushitushwa na misafara ya nenda rudi ya Mtume Muhammad, asimuulize kuna nini! Maana kwa mujibu wa riwaya zinzosimulia tukio hili zinasema kuwa, Nabii Ibrahim (a.s.) alikuwa katika mbingu ya saba na Nabii Musa (a.s.) mbingu ya sita. Aidha, kwanini Mwenyeezi Mungu asimpe moja kwa moja Mtume wake Sala tano, kuliko usumbufu huu alioupata Mtume wa nenda rudi mpaka akaingiwa na aibu kubwa akashuka kwa shingo upande na sala zake tano!!?