MUSA NA SALA TANO

Imepokewa katika riwaya kuwa: Sala tano zimefaradhiwa wakati Mtume (s.a.w.) alipopelekwa katika msafara wa Miiraji huko juu Inasemwa kuwa, zilifaradhiwa sala hamsini kwa kila siku, na Mtume (s.a.w.) alipokuwa akirudi na agizo hilo, alipofika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa (a.s.) akamshauri Mtume Muhammad (s.a.w.) arudi kwa Mola wake amuombe ampunguzie Sala hizo. Mtume alirudi kwa Mola wake na akapunguziwa Sala kumi, aliposhuka katika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa akiwa na sala arobaini. Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake apunguziwe Sala hizo, Mtume akafanya hivyo, Mwenyeezi Muungu akapunguza Sala kumi. Mtume alipofika kwa Nabii Musa, akamrudisha kwa Mola wake akaombe takhfif; Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza sala kumi Mtume akashuka alipofika kwa Nabii Musa akiwa na sala ishirini, Nabii Musa akamtaka arudi kwa Mola wake akampunguzie, kwa sababu umma wake hawawezi hilo. Mtume (s.a.w.) alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala kumi, Mtume akashuka akiwa na sala kumi, alipokutana na Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake ili apunguziwe, Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala tano, Mtume (s.a.w.) aliposhuka kwa Nabii Musa (a.s.) akiwa na sala tano, alipotaka kumrudisha kwa Mola wake, Mtume (s.a.w.) alisema:- "Kwa hakika, nimerudi kwa Mola wangu mara tano, kuomba takhfif mpaka sasa naona aibu kubwa". Ndipo aliposhuka Mtume (s.a.w.) akiwa sala tano, ambazo wanapaswa Waislamu kuzisali kwa kila siku.