1. Hawakuwa walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake
miongoni mwa Mayahudi na Wakristo, na miongoni mwa washirikina, waache
kughafilika kwao na ujinga wao kuto ijua Haki mpaka iwajie hoja ya kukata.
2,3. Na hoja hiyo ni Mtume aliye tumwa kutokana na Mwenyezi Mungu
awasomee kurasa zilizo takasika na upotovu, ndani yake zimo hukumu zilizo
sawa zenye kutamka kwa haki na kwa yaliyo ndiyo.
4. Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu katika Mayahudi na Wakristo,
ila baada ya kuwajia hiyo hoja iliyo wazi yenye kuonyesha ya kwamba Muhammad
ndiye huyo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliye ahidiwa katika Vitabu vyao.
5. Na hawakulazimishwa jambo katika walio lazimishwa ila iwe ibada
yao kwa Mwenyezi Mungu ni kumsafia Yeye Dini, waache upotovu wasimame sawa
kwenye Haki, na wazihifadhi Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Mila Iliyo
Nyooka.
6. Hakika wale walio kufuru katika Watu wa Kitabu na washirikina
wataingia katika Moto wa Jahannamu, wala hawatatoka humo. Hao ndio waovu
wa viumbe kwa itikadi na vitendo.
7. Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda
vitendo vyema, hao ndio bora ya viumbe kwa itikadi na vitendo.
8. Malipo yao Akhera kwa Imani na vitendo vyema walivyo vitanguliza, ni Mabustani ya kudumu yenye kupitiwa na mito kati yake, watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu amepokea a'mali zao, na wao watamshukuru kwa hisani yake aliyo wafanyia. Hiyo ndiyo jaza ya mwenye kuiogopa adhabu ya Mola wake Mlezi, akaamini na akatenda mema.