1. Naapa kwa tini na zaituni, kwa baraka zao na ubora
wa manufaa yao.
2. Na kwa mlima ambao juu yake ndio Mwenyezi Mungu alimsemeza Musa.
3. Na kwa huu mji mtukufu wa Makka, ambao anaushuhudia utukufu wake
mwenye kwenda uzuru, na anapata amani mwenye kuuingia.
4. Kwa hakika bila ya shaka yoyote Sisi tumemuumba mtu amesimama
sawa kwa umbo bora kabisa lilio nyooka, na akasifika kwa sifa nzuri kabisa.
5. Kisha tukamteremsha cheo mpaka akawa ni wa chini kabisa katika
hao walioko chini, kwa kuacha kufanya waajibu wa hayo tuliyo muumbia.
6. Lakini walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao basi watapata
ujira usio wakatikia wala kuwapungukia.
7. Basi kitu gani kinacho kupelekea kukadhibisha kufufuliwa na kulipwa
baada ya kuwekwa wazi uweza wetu wa hayo?
8. Kwani Mwenyezi Mungu aliye yatenda hayo tuliyo kueleza si muadilifu kuliko mahakimu wote kwa kufanya na kupanga?