1. Naapa kwa mwangaza wa asubuhi unapo ufukuza usiku.
2. Na kwa masiku kumi yaliyo tukuzwa na Mwenyezi Mungu. (Na hayo
ni masiku kumi ya mwanzo wa Mwezi wa Alhaj, Mfungo Tatu).
3. Na shafi' yaani hisabu inayo gawika kwa mbili, kama 4, 6, 8 n.k.
na witri, yaani isiyo gawika kwa mbili, kama 1, 3, 5 n.k. katika kila kitu.
4. Na kwa usiku unapo pita kwa kwenda ulimwengu kwa namna ya ajabu.
5. Je! Katika vitu vilivyo tajwa vinavyo onekana kwa akili hapana
kiapo cha kukinaisha?
6,7. Kwani hujui jinsi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu
yake kaumu ya Hud, watu wa Iram wenye majengo marefu?
8. Ambayo haikupata kujengwa mfano wake kwa umadhubuti na ujenzi
katika nchi.
9. Kwani hukujua jinsi Mola wako Mlezi alivyo teremsha adhabu yake
kwa Thamudi, kaumu ya Saleh, walio chonga majabali kujengea nyumba zao
huko bondeni?
10. Au kwani hukujua vipi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu
yake Firauni mwenye majeshi yaliyo upa nguvu ufalme wake kama vigingi vinavyo
simamisha makhema?
11. Ambao walipita mipaka katika nchi?
12. Na wakazidisha kufanya uharibifu kwa ukafiri na udhalimu?
13. Basi Mola wako Mlezi aliwateremshia adhabu kali ya kuwaunguza.
14. Hakika Mola wako Mlezi anaviangalia vitendo vya watu, na anawahisabia,
na atakuja kuwalipa kwavyo.
15. Ama mtu akijaribiwa na Mola wake Mlezi na akamkirimu, na akamneemesha
kwa mali na cheo na nguvu, basi husema kwa kughurika na hayo: Mola wangu
Mlezi amenitukuza kwa kuwa ninastahiki haya!
16. Na pindi Mola wake Mlezi akimjaribu mtu kwa kumdhikisha riziki,
basi hughafilika na hikima ya hayo na husema: Mola wangu Mlezi kanidhalilisha!
17. Wacheni mtindo huo! Mambo siyo hayo kama msemavyo; bali nyinyi
hamumkirimu yatima;
18. Wala hamhimizani kuwalisha masikini;
19. Na mnakula mali ya urithi kwa pupa, hamchagui linalo faa na lisilo
faa.
20. Na mnayapenda mali mno, yanayo kupelekeeni kupapatika katika
kuyakusanya na ubakhili wa kuyatumia.
21. Wacheni vitendo hivyo! Kwani inakungojeeni siku itapo lazwa ardhi
iwe sawa sawa,
22. Na aje Mola wako Mlezi kama anavyo stahiki kuja kwake Subhanahu
na Malaika waje kwa safu safu;
23. Na siku hiyo iletwe Jahannamu, nyumba ya adhabu, siku hiyo
yatapo tokea hayo mwanaadamu atakumbuka aliyo yaharibu - lakini wapi! Kukumbuka
huko kumfae nini, na wakati umekwisha pita?
24. Atasema kwa majuto: Laiti ningeli jitangulizia katika dunia vitendo
vyema vya kunifaa katika maisha ya Akhera!
25,26. Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya
Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.
27. Ewe nafsi uliye tulia juu ya Haki!
28. Rejea kwenye radhi ya Mola wako Mlezi nawe uradhi kwa neema ulio
pewa, nawe umemridhisha kwa a'mali uliyo ikadimisha.
29. Basi ingia katika kundi la waja wangu walio wema!
30. Na ingia katika Pepo yangu, nyumba ya neema ya milele!