1. Je! Ewe Muhammad! Imepata kukujia hadithi ya Kiyama
ambacho kwa vitisho vyake kitawafanya watu wazimie?
2,3. Siku hiyo ya Kiyama zitakuwepo nyuso zimedhalilika, zimechoka,
taabani kwa shughuli na mashaka ya Motoni,
4. Zinaingia kwenye Moto unao waka kwa nguvu!
5. Wananywesha maji yanayo toka kwenye chemchem inayo tokota.
6. Hawana chakula ila chakula kiovu kabisa, anaadhibika mwenye kukila.
7. Hakileti nafuu yoyote katika mwili, wala hakiondoi njaa.
8,9,10. Na pia zitakuwapo nyuso zenye kutoa nuru Siku ya Kiyama,
kwa malipo ya vitendo vyao walivyo fanya duniani. Hao watakuwa wameridhia
kwa watayo yapata katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.
11,12. Humo halisikilizani neno la upuuzi. Humo mna chemchem isiyo
katika.
13. Humo vitakuwamo viti vilivyo nyanyuliwa kwa cheo na kwa hakika,
kama ni ziada ya neema.
14. Na bilauri (gilasi) zilio wekwa mbele yao,
15. Na mito na matakia yalio pangwa kwa safu.
16. Na mazulia mengi yaliyo tandazwa hapo barazani.
17. Je! Wanapuuza kuzingatia Ishara, basi hebu na wamuangalie ngamia,
vipi alivyo umbwa kwa namna ya peke yake kwa uweza wa Mwenyezi Mungu?
Katika kuumbwa ngamia zipo Ishara na miujiza yenye kuthibitisha
uweza wa Mwenyezi Mungu ambao yafaa wenye kuzingatia wauzingatie. Katika
sifa zake zinazo onekana ni hizo zinazo mfanya kweli awe ni jahazi ya jangwani.
Macho yake yamenyanyuka yako juu ya kichwa, na yanaelekea nyuma, na tena
yana kope za kuyakinga na mchanga na vumbi. Kadhaalika pua na masikio yamefunikwa
na nywele kwa sababu hiyo hiyo. Ukivuma mdharuba wa mchanga pua hufunga
na masikio hupinda, juu ya kuwa tokea hapo ni madogo na si yenye kudhihiri
mno, ukilinganisha na mwili wake. Ama miguu ni mirefu kwa kusaidia wepesi
wa kwenda, pamoja na kunasibiana na urefu wa shingo yake. Ama nyayo ni
pana zimetanda kwa ukhafifu ili kumwezesha ngamia kwenda juu ya mchanga
laini. Na ngamia kwa jumla chini ya kifua chake na chini ya viungo vyake
vya miguu pana kama mito inayo msaidia ngamia kupiga magoti na kulala juu
ya ardhi ngumu na imoto, kama vile vile pande zote mbili za mkia wake yapo
manyoya marefu ya kumlinda sehemu zake za nyuma na vitu vya kumuudhi.
Ama vipawa alivyo pewa ngamia kwa ajili ya kazi yake ni vya ajabu
zaidi. Siku za baridi hahitajii maji, bali anaweza asinywe maji muda wa
miezi miwili mfululizo, ikiwa chakula kimajimaji na laini, au wiki mbili
ikiwa kikavu. Pia anaweza kustahamili kiu hata siku za joto muda wa wiki
au wiki mbili, na hupungua muda huo zaidi ya thuluthi mbili ya uzito wake.
Na anapo yapata maji huyagugumia maji kwa wingi mno arejeshe uzito wake
wa zamani kwa dakika chache tu. Na ngamia hayarimbiki maji katika tumbo
lake kama ilivyo kuwa ikidhaniwa, bali katika mfumo wa mwili wake, na huyatumia
kwa uangalifu mkubwa mno. Kwa hivyo kabisa hapumui kama anavyo pumua mbwa,
mathalan, wala hatoi pumzi kwa mdomo wake, wala hatoki majasho kwenye ngozi
yake ila kwa uchache kabisa. Na hayo ni kuwa daraja ya joto ya mwili wake
inakuwa chini sana asubuhi mapema. Kisha hupanda kidogo kidogo zaidi ya
daraja sita kabla ya kuhitajia kuipoza kwa jasho na kutoa mvuke. Na juu
ya maji mengi mno yanayo toka katika mwili baada ya kiu kirefu kwa hakika
uzito wa damu hauathiriki ila kwa kiasi tu, na kwa hivyo kiu hakina athari
kitu juu yake. Na imethibiti mafuta ya nunudu yaliyo khaziniwa kwa ajili
ya nishat'i yanamkifu kumkinga na machungu ya njaa, lakini hayamfaidishi
sana kwa haja ya maji ambayo ni lazima kwa mwili wake.
Na bado wataalamu wangali wanagundua mapya katika ngamia kila wakichungua
ya kuhakikisha hadhi aliyo mpa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atazamwe katika
uumbaji wake wa muujiza.
18. Na waizingatie mbingu wanayo iona daima, vipi ilivyo nyanyuliwa
huko mbali bila ya nguzo!
19. Na milima wanayo ikwea mpaka wakafika vileleni kwake, vipi ilivyo
simamishwa kwa urefu, imeshikamana na ardhi, haiyumbi wala haitikisiki!
Mara nyingi katika Qur'ani tukufu inatajwa kuwa ardhi "imekunjuliwa".
Na makusudio ya hayo ni kuwa ardhi ijapo kuwa ni duara kama mpira kwa sura
yake, lakini inavyo onekana kwa watazamao ni kuwa imekunjuliwa. Na haya
hayagongani na yaliyo thibitishwa na sayansi katika jambo lolote.
20. Na ardhi wanayo ikalia na kuyendea juu yake, vipi ilivyo kunjuliwa
na kutandazwa!
21,22 Basi kumbusha kwa wito wako, kwani kazi yako muhimu ni kufikisha
wito tu. Hukuwa mtawala juu yao.
23,24 Lakini miongoni mwao ataye puuza na akakataa, basi Mwenyezi
Mungu atampa adhabu iliyo kubwa kabisa, isiyo kuwa na ya kuipita.
25. Hakika ni kwetu Sisi marejeo yao kwa kifo na kufufuliwa, wala
hapana penginepo isipo kuwa kwetu.
26. Tena ni juu yetu Sisi tu peke yetu kuwahisabia na kuwalipa.