1. Naapa kwa mbingu yenye Buruj au Manaazil, njia au
vituo ambavyo nyota hupitia katika nyendo zake,
Buruuj au Manaazil ndio huu mkusanyiko wa nyota unao onekana
kwa sura namna mbali mbali mbinguni. Hizo Buruuj zimegawika sehemu kumi
na mbili ambazo ardhi inazipitia inapo lizunguka jua.
2. Na kwa Siku iliyo ahidiwa kuwa ndiyo Siku ya Hisabu na Malipo,
3. Na kwa viumbe watao hudhuria Siku hiyo wakaona vitisho na ajabu
zitakazo kuwepo,
4. Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani watu walio chimba khandaki katika
ardhi,
5. Wakawasha moto kuwatumbukiza ndani yake Waumini ili kuwatesa,
6. Na wao wamekaa ukingoni mwake wakishuhudia mateso yanayo wapata
Waumini.
7. Na wao wapo hapo wamehudhuria kwenye mateso wanayo watendea Waumini.
8. Na hapana walilo lichukia kwa hao Waumini ila ni kuwa wakimuamini
Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu ambaye adhabu yake huogopwa, Msifiwa anaye
tarajiwa thawabu zake.
9. Ambaye, peke yake, ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na
Mwenyezi Mungu ni shahidi anashuhudia yote wayatendayo Waumini na makafiri
na atawalipa kwayo.
10. Hakika walio watia matatani Waumini wanaume na Waumini wanawake
kwa maudhi na kuwaadhibu kwa moto, kisha wasitubu na kurejea nyuma watapata
Akhera adhabu ya Jahannamu kwa ukafiri wao, na watapata adhabu ya kuunguzwa
kwa kule kuwaunguza moto Waumini.
11. Hakika hao walio kusanya kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu vitendo
vyema watapata Mabustani yapitayo mito kati yake. Neema hiyo waliyo lipwa
ni kufuzu kukubwa.
12. Hakika mshiko wa Mola wako Mlezi kuwashika majabari umefika ukomo
kwa ukali wake
13. Ni Yeye peke yake ndiye Mwenye kuanza kuumba, na kisha ni Yeye
anaye rejeza tena,
14. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha kwa mwenye kutubu na akarejea, na
Mwingi wa mapenzi kwa mwenye kumpenda na akamt'ii.
15. Yeye ndiye Mwenye Kiti cha Enzi na Mwenye kukimiliki, na Mkuu
kwa dhati yake na sifa zake.
16. Ni Mtendaji kwa alitakalo, na hendi kinyume na uweza wake yeyote
anaye taka.
17. Je! Imekujia, ewe Muhammad, hadithi ya kile kikundi kilicho a'si
katika mataifa yaliyo kwisha pita?
18. Kaumu ya Firauni na Thamudi na yaliyo washukia katika malipo
ya kushikilia kwao upotovu?
19. Bali hao makafiri katika kaumu yako ni shadidi zaidi katika kukukadhibisha
kuliko hawa walivyo wakadhibisha Mitume wao.
20. Na Mwenyezi Mungu anawaweza hao, na anawajua vilivyo.
21. Bali hii ulio waletea ni Qur'ani tukufu inadhihirisha hoja za
ukweli wako.
22. Imo katika Ubao Ulio Hifadhiwa, hapana uwezo unao weza kuipotoa au kuigeuza.