1,2,3. Wataangamia wanao punja, ambao wakijipimia wenyewe
kwa watu hujitwalia ya kutosha na kuzidi, na wakiwapimia watu kwa vipimo
au mizani huwapunguzia haki yao wanayo stahiki, kwa dhulma!
4,5. Hivyo haiwapitikii katika akili zao hawa wanao punja wenzao
kwamba watakuja fufuliwa katika siku ya vitisho vikuu?
6. Siku watapo simama watu kwa amri ya Mola Mlezi wa walimwengu wote
na hukumu yake?
7. Wacheni kupunja, na kughafilika na kufufuliwa! Kwani hakika
waliyo andikiwa wakosefu katika a'mali zao mbovu, bila ya shaka yamo katika
Sijjin.
8. Na nini kitakujuvya nini hiyo Sijjin?
9. Hicho ni Kitabu kilicho pigwa mistari baina ya maandishi yake.
10. Wataangamia wanao kadhibisha siku itapo kuwa kufufuliwa na kuhisabiwa.
11. Ambao wanaikanusha Siku ya Malipo.
12. Na wala haikanushi Siku ya Malipo ila kila mwenye kupindukia
mipaka mwingi wa madhambi.
13. Na akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu zenye kutaja kuwepo malipo
husema: Huo ni uwongo wa walio tangulia!
14. Ewe uliye kiuka mipaka! Wacha kauli hiyo potovu. Bali nyoyo za
wenye kupindukia mipaka imegubikwa na ukafiri na maasi waliyo yatenda.
15. Hakika ni kweli kuwa hao wanao kadhibisha watazuiliwa siku hiyo
rehema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya maasi waliyo yachuma.
16. Kisha hakika hao bila ya shaka wataingia Motoni.
17. Kisha wataambiwa kwa kuwakebehi: Hii basi ndiyo adhabu inayo
kuteremkieni ambayo mlikuwa mkiikanusha duniani!
18. Ni hakika kuwa vitendo vya watu wema bila ya shaka vimeandikwa
katika I'liyyin.
19. Na nini cha kukujuvya nini I'liyyin?
20,21. Hicho ni Kitabu kilicho andikwa wazi maandishi yake, wanakihudhurisha
na kukihifadhi Malaika walio kurubishwa.
22,23. Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema za
Peponi, juu ya viti vya enzi, wakiziangalia neema na ukarimu alio wakirimu
Mwenyezi Mungu.
24. Utaona katika nyuso zao uchangamfu na mng'aro wa neema.
25,26. Wakinyweshwa kinywaji safi kilicho hifadhiwa; kuhifadhiwa
huko hakukuzidisha ila uzuri wake. Na kupata neema hizo, basi, na washindanie
wanao shindana.
27,28. Cha kuchanganyia kinywaji hicho ni maji ya Tasniim ya Peponi,
nayo ni chemchem wanao inywa walio kurubishwa si wengineo, katika watu
wa Peponi.
29. Wale walio kuwa wakibeba madhambi kuipingia Dini walikuwa wakiwacheka
kuwakejeli Waumini duniani.
30. Na wakipita Waumini mbele yao basi wao hukonyezana kwa kuwabeza.
31. Na hao wakosefu wakirejea kwa ahali zao hurejea kwa furaha na
kuona ladha kwa vile kuwakejeli Waumini.
32,33. Na wakiwaona Waumini husema: Ama hakika hawa wamepotea kweli
kwa kumuamini Muhammad. Wala hao wakosefu hawakutumwa wawe wa kuwahukumu
Waumini kwa kuwaongoza au kuwapoteza, wala kuwa ni walinzi wa vitendo vyao.
34. Basi Siku ya Malipo walio amini watakuwa ndio wa kuwacheka hao
makafiri kwa kuwalipizia kile kicheko chao na kejeli yao ya duniani.
35. Ilhali wako juu ya vitanda na matakia watakuwa Waumini wakiziangalia
neema za Mwenyezi Mungu alizo wapa.
36. Je! Makafiri watalipwa huko Akhera kwa waliyo yatenda duniani?