2. Na nyota zitakapo pukutika na kutawanyika,
3. Na bahari zikafurika na kuingiliana kwa kuondoka viziwizi baina yao,
4. Na makaburi yakafunuliwa na wakatoka maiti walio kuwamo,
5. Hapo basi kila nafsi itajua nini kheri au shari iliyo tanguliza na iliyo chelewesha.
6. Ewe mwanaadamu! Kitu gani kilicho kukhadaa wewe na Mola wako Mlezi
Mtukufu hata ukafanya jeuri ya kwenda kumuasi? (Ni dhaahiri kuwa Sayyid
Abdulla bin Ali bin Nassir aliye tunga utenzi wa Kiswahili maarufu uitwao
Al Inkishaf aliiwaza Aya hii alipo tunga ubeti huu:
Moyo wangu nini huzundukani
Likughurielo hela ni nni?
Hunelezi nami kalibaini
Liwapo na sura nisikataye )
7. Mungu wako huyo ndiye aliye kuumba nawe hukuwa chochote, akakuumba na viungo vya kukuletea manufaa, akakufanya umenyooka kwa umbo sawa sawa.
8. Akakujenga na akakuleta katika sura yoyote aliyo itaka.
9. Hamwachi? Bali nyinyi mnakadhibisha malipo ya Siku ya Kiyama!
10,11,12. Na hakika wapo juu yenu Malaika walinzi, ambao ni waheshimiwa kwetu, wanasajili vitendo vyenu vyote mvitendavyo, vya kheri na shari.
13. Hakika wale walio ni wa kweli katika Imani yao wapo katika neema kubwa.
14,15. Na hakika walio iacha amri ya Mwenyezi bila ya shaka watakuwa katika Moto unao unguza, wataingia humo Siku ya Malipo.
16. Na wala hawatatoka katika Jahannamu!
17. Na nini kitakujuvya ni nini hiyo Siku ya Malipo, na mambo yake yamepindukia ujuzi wako na fikra zako?
18. Tena ni nini kitacho kujuvya ni nini hiyo Siku ya Malipo kwa vitisho vyake na shida zake?
19. Siku ambayo nafsi haitakuwa na mamlaka yoyote juu ya nafsi ya
kuifaa au kuidhuru; na amri yote siku hiyo itakuwa ni ya Mwenyezi Mungu
peke yake!