1. Ninaapa kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuving'oa
vitu kutokana na pahala pao kwa nguvu,
2. Na kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuvitoa vitu kwa utaratibu na
ulaini,
3. Na kwa kila kilicho pewa mbio za kutekeleza kazi yake kwa sahala
na wepesi.
4. Na kwa vinavyo shindania kutimiza waajibu ulio twikwa juu yao
kushindania kwa juhudi,
5,6,7. Na vinavyo dabiri, kupanga, mambo na kuyaendesha kwa mujibu
wa vilivyo khusishwa, bila ya shaka Saa ya Kiyama itafika; hiyo siku
ambayo mpulizo wa mwanzo wa barugumu utavitikisa viumbe vyote, na mpulizo
huo utafuatiwa na wa pili ambao ndio utakao kuwa wa kufufuliwa watu.
8. Siku hiyo nyoyo zitapapatika kwa khofu.
9. Macho ya watu yatakuwa na huzuni, manyonge.
10. Watu hawa husema duniani kwa kukanya kufufuliwa: Ati tutarudishwa
sisi baada ya kwisha kufa, tuumbwe tena kama tulivyo kuwa?
11. Tukisha kuwa mafupa yaliyo chakaa, ati tutarejeshwa tufufuliwe
upya?
12. Wanasema, kwa kukanya na kejeli: Kurejea huko kama kukitokea
basi ni marejeo ya khasara, na sisi si watu wa kukhasiri.
13,14. Msidhani kurejea huko ni kuzito. Kwani hayo ni ukelele mmoja
tu, mara maiti wote watahudhurishwa kwenye ardhi ya mkusanyiko!
15,16. Ewe Muhammad! Imekufikilia hadithi ya Musa, alipo mwita Mola
wake Mlezi katika bonde lilio takaswa, linalo itwa "T'uwa"?
17. Akaambiwa: Nenda kwa Firauni aliye pindukia mpaka katika udhalimu.
18. Umwambie: Je! Huelekei kut'ahirika?
19. Na mimi nikuongoze upate kumjua Mola wako Mlezi, umwogope.
20. Musa akamwonyesha Firauni miujiza mikubwa.
21. Lakini Firauni alimkadhibisha Musa kwa aliyo kuja nayo, na akamuasi
kwa aliyo mwitia.
22. Kisha akamgeuzia mgongo, akenda kujitahidi kumpinga.
23,24. Akawakusanya wachawi, na akawaita watu, akasema: Mimi ndiye
Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa.
25. Mwenyezi Mungu akampa adhabu kwa kauli yake ya mwisho, nayo ni
vile kusema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa. Na akampa
adhabu kwa kauli yake ya mwanzo, nayo ni kumkadhibisha Musa a.s.
26. Hakika katika hadithi hiyo yapo mawaidha kwa mwenye kumkhofu
Mwenyezi Mungu.
27,28. Enyi mnao kanya kufufuliwa! Kukuumbeni nyinyi ni taabu zaidi
au kuziumba mbingu, kuzikusanya sehemu zake zilio tawanyika mbali mbali,
na kunyanyua kimo chake, na zikakaa sawa hazina tafauti wala ila?
29. Na akatia kiza katika usiku wake, na akautokeza mchana wake ukawa
na mwangaza?
30. Na ardhi baada ya hayo akaikunjua, na akaisawazisha, ikasilihi
kukaliwa na watu wake?
31. Akatoa ndani yake maji yake yanayo tibuka katika chemchem zake,
na ikamiminika mito yake, na ikawa na mimea yake ya chakula kwa ajili ya
watu na wanyama;
32. Na milima akaithibitisha imara
33. Kwa ajili ya manufaa yenu na wanyama wenu mnao wafuga!
34. Kitakapo fika Kiyama ambacho vitisho vyake vitaenea kote,
35. Siku atakapo kumbuka mtu vitendo vyake vya kheri au shari,
36. Na Jahannamu ikadhihirishwa wazi, akaiona kila mwenye macho kuwa
ndio malipo,
37,38,39. Basi ama mwenye kupita mpaka kwa maasi yake, na akajichagulia
nafsi yake maisha yanayo pita njia, basi Moto wa Jahannamu unao babua
upepo wake ndio makaazi yake wala hana mengineyo.
40,41. Na ama mwenye kukhofu ukubwa na utukufu wa Mola wake Mlezi,
na akaizuia nafsi yake na matamanio ya kumpumbaza, basi huyo nyumba ya
neema ya Peponi ndio makaazi yake, wala hana penginepo.
42. Ewe Muhammad! Wanakuuliza, ati, khabari za Saa ya Kiyama, itakuwa
lini?
43. Ujuzi wa hayo hauko kwako hata uwatajie.
44. Ujuzi wa hayo uko kwa Mola wako Mlezi tu, si kwa mwenginewe.
(Nabii Isa a.s. ambaye Wakristo wanasema ni Mwana wa Mungu, au ndiye Mungu,
pia anasimuliwa katika Biblia kuwa hakuijua Saa na Siku ya Kiyama. Injili
ya Mathayo 24.36 inanukulu maneno ya Yesu: "Walakini habari ya siku ile
na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila
Baba peke yake.")
45. Kwani waajibu wako ni kuwaonya wanao khofu si kuwatangazia wakati
wake.
46. Na wao siku watakayo iona hiyo Saa ya Kiyama ni kama kwamba hawakuishi duniani zaidi kuliko jioni moja tu, au mchana wake.