1. Wanaulizana nini hao makafiri?
2,3. Wanaulizana khabari kubwa, khabari ya kufufuliwa, ambayo wao
wamezama ndani yake kukhitalifiana baina ya wenye kuikataa na wenye kuitilia
shaka.
4. Kuwazuia kuulizana huko wanaambiwa kuwa watakuja ujua ukweli wa
mambo hapo watapo ona kufufuliwa kumetokea khasa.
5. Tena kuwazuia, watakuja jua itapo wateremkia adhabu.
6. Kwani wao hawaoni Ishara za uweza wetu kwamba Sisi tumeifanya
ardhi imetandikwa upatikane utulivu juu yake na iwezekane kutembea juu
yake?
7. Na tukaifanya milima ni vigingi vya ardhi vya kuituliza?
Sehemu ya gamba gumu lilio juu ya ardhi linfikilia kiasi ya kilomita
60 unene wake, na inazidi mikunjo, mifimbi, inapanda juu kuwa milima, na
huteremka chini kuwa ni vina vya bahari; na hiyo hulingana kwa sababu ya
uzito unao patikana kutokana na milima. Na kulingana huko hakuharibiki
ila kwa kubugunyika, kwani gamba kavu la ardhi linazuiliwa na milima, kama
vigingi vinavyo zuilia khema. (Rejea Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 7 ya
Surat Qaf).
8. Na tukakuumbeni kwa jozi, wanaume na wanawake?
9. Na tukafanya kulala kwenu ni mapumziko ya machofu ya kazi?
Kulala usingizi ni kusita nishat'i ya sehemu ya ubongo yenye
kutambua na kuwa macho. Yaani gamba la ubongo, au kupunguka nishat'i yake
kwa wingi, ukilinganisha na daraja za nishat'i ya sehemu za viungo vilio
baki. Na kwa hivyo kunapunguka nguvu na joto la mwili, tena mwili hapo
wakati wa usingizi hupata kutua na kupumzika baada ya kuhangaika viungo
au akili au vyote viwili. Basi kazi za kimwili zote hupunguka isipo kuwa
kazi za kusaga chakula, na kupitisha mkojo katika mafigo, na kutoka majasho
katika ngozi, kwani yakisita hayo hupatikana madhara juu ya maisha ya mtu.
Ama kuvuta pumzi huko nako hupunguka, na huwa ni kwa ndani zaidi, na huwa
kwa kifua zaidi kuliko kwa tumbo. Na mpigo wa mishipa hupungua kasi kwa
kunavyo tokana na moyo, na hudhoofika mkazano wa musulo (muscular tension),
na kwa hivyo huwa taabu kupata harakati za kinyume. Na yote haya ni ili
binaadamu apate kupumzika wakati wa kulala.
10. Na tumeufanya usiku ni sitara kwenu kwa kiza kinacho kufunikeni.
11. Na tumeufanya mchana ni wakati wa kuhangaika kwenu kutafuta cha
kukusaidieni katika maisha yenu.
12. Na tumesimamisha juu yenu mbingu saba zenye nguvu madhubuti.
13. Na Sisi tumeliumba jua lenye mwangaza na linalo waka.
Makusudio ya Assiraj Alwahhaaj, Taa yenye mwanga na joto,
ni Jua. Na hayo kama ilivyo thibiti katika sayansi kuwa daraja ya joto
la uso wake inafika daraja 6000. Ama kati yake daraja yake inazidi
daraja 30 milioni kwa sababu ya mdidimizo mkubwa unao patikana juu ya madda
ziliomo ndani yake. Na jua linatoa nishat'i hizi zifuatazo: 9 katika 100
ya miale ya Ultraviolet rays, 46 katika 100 ya miale ya mwangaza,
45 katika 100 miale ya joto, au Infra red rays. Na kwa hivyo hii Aya tukufu
imeliita kuwa ni Taa yenye mwangaza na joto.
14. Na tumeteremsha kutokana na mawingu yaliyo karibia kunyesha maji
yenye kumiminika kwa nguvu.
Mvua ndio kitu pekee kinacho toka asli yake maji matamu katika ardhi.
Na asli ya mvua ni kukusanyika vijisehemu vya maji yanayo panda kutoka
baharini, na maziwa na mito, yakakusanyika kama mawingu na yakageuka chembe
za mvua au vipande vya barafu, na khatimaye yakaanguka kwa sura ya mvua
au theluji.
15. Ili tutoe kwa maji haya nafaka na mimea kuwa ni chakula kwa ajili
ya watu na wanyama.
16. Na mabustani yenye miti iliyo fungamana na matawi yake yameingiliana.
17. Hakika siku ya uamuzi baina ya viumbe imewekewa miadi ilio kwisha
kadiriwa kwa ajili ya kufufuliwa.
18. Siku litakapo pulizwa barugumu na kufufuliwa watu, mtakuja kwenye
mkutano makundi kwa makundi.
19. Na mbingu zitapasuliwa kila upande hata zitakuwa ni milango milango.
20. Na milima itaondolewa baada ya kung'olewa mwahala mwake, na kuvurugwa,
ikawa unaiona kama sura ya milima na hali hiyo ni kifusi tu kilicho rindikwa,
kama uonavyo mangati, sarabi, unaona kama sura ya maji nayo si maji.
21. Hakika Jahannamu imekuwa kama ni kitu kinacho ngojea, walinzi
wake wanawangojea watu watakao kuja kuingia.
22. Yawe ni marejeo na mafikio kwa wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi
Mungu.
23. Watakaa humo dahari baada ya dahari.
24. Hawataonja humo hata chembe ya upepo wa kuburudisha joto lake,
wala kinywaji cha kupoza kiu chao.
25. Lakini watakunywa maji yalio pita ukomo kwa umoto wake, na usaha
unao miminika kutokana na ngozi za watu wa Motoni.
26. Malipo ya kuwafikiana na vitendo vyao viovu.
27. Kwani hao hawakutaraji kuwa itakuwapo kuhisabiwa, hata watende
ya kuwaokoa humo.
28. Wakazikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuthibitisha
kufufuliwa kwa mkadhibisho mkali.
29. Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.
30. Basi onjeni, wala hampati kwetu ila kuzidishiwa adhabu tu.
31. Hakika wenye kumcha Mola wao Mlezi watapata kuokoka na adhabu,
na wataipata Pepo,
32. Na mabustani yenye matunda, na mizabibu mizuri,
33. Na wanawari walio watipwatipwa wa hirimu yao,
34. Na bilauri safi zilizo jaa pomoni,
35. Hawasikii huko Peponi upuuzi wala uwongo.
36. Ni malipo kutokana na Mola wako Mlezi, kwa fadhila yake na ihsani
ya kutosha.
37. Mola Mlezi wa mbinguni na duniani na vilio baina yao, ambaye
rehema yake imeenea juu ya kila kitu. Hapana yeyote mwenye madaraka ya
kusema mbele yake.
38. Siku atakapo simama Jibrili na Malaika walio teuliwa nao wamenyenyekea,
hasemi mmoja wao ila akipewa idhini na Arrahman, Mwingi wa rehema, kuwa
aseme, naye atasema lilio sawa tu.
39. Hiyo ndiyo siku isiyo na shaka. Basi atakaye na ashike njia ya
kwenda kwa Mola wake Mlezi arejee kwa Imani, na a'mali njema.
40. Hakika Sisi tumekuhadharisheni na adhabu itakayo tokea karibu, siku atakapo angalia mtu vitendo vyake vilivyo tangulizwa na mikono yake, na atakapo sema kafiri kwa kutamani kuokoka: Laiti ningeli bakia udongo baada ya kufa, nisifufuliwe wala nisihisabiwe!