1,2,3,4,5,6,7. Naapa kwa Aya zilizo tumwa kwa ulimi
wa Jibrili kumpelekea Muhammad kwa upole wa kawaida na kheri, na kwa Aya
zenye kuzitwaa kwa nguvu dini nyengine zote za uwongo zikizipeperushia
mbali, na kwa Aya zenye kueneza hikima na uwongofu katika nyoyo za walimwengu
kwa uenezi mkubwa mno, na zenye kufarikisha baina ya kweli na uwongo kwa
mfarakano ulio wazi kabisa, na zenye kuwapa watu mawaidha ya kuwanufaisha,
ili iwe ni udhuru kwao na onyo wasiwe na hoja, hakika haya mliyo ahidiwa
ya kuja Kiyama kwa yakini yatatimia tu bila ya shaka yoyote.
8,9,10,11. Basi nyota zitapo ondolewa kabisa, na mbingu zitapo pasuka,
na milima ikavurugwa na ikapeperushiwa mbali na upepo, na Mitume wakawekewa
wakati maalumu wahudhurie kwa ajili ya kuwatolea ushahidi kaumu zao.
12,13,14,15. Kwa ajili ya siku gani yametayarishwa mambo haya makubwa
makubwa? Kwa ajili ya siku watakapo pambanuliwa baina ya viumbe. Na nini
cha kukujuvya ina nini hiyo siku ya kupambanua? Ni maangamio ya milele
siku hiyo kwa hao wanao kadhibisha walio waahidi Mitume!
16,17,18. Kwani hatukuwaangamiza mataifa ya zamani yaliyo kadhibisha,
na kisha tukawafuatilizia hao wenginewe tukawateketeza hali kadhaalika,
kwa madhambi waliyo yafanya na walivyo mkataa Mwenyezi Mungu?
19. Siku hiyo ni siku ya kuteketezwa walio kadhibisha, kama tulivyo
waahidi.
20,21,22,23,24. Kwani hatukukuumbeni kutokana na maji yaliyo dhalili,
nayo ni manii, na tukayaweka maji haya katika pahala patulivu, mpaka kutimilia
kuumbwa kwake na kutengenezwa kwake kwa muda anao ujua Mwenyezi Mungu.
Nasi tukaweka vipimo katika kuumbwa kwake, na kutengenezwa kwake, na kutoka
kwake. Basi wabora wa kupima na kukadiria ni Sisi. Ole wao hao wanao kadhibisha
neema za kuumba na kukadiria.
25,26,27,28. Kwani hatukuifanya ardhi kuwa imekusanya juu ya mgongo
wake viumbe vilivyo hai visio hisabika, na vilio kufa visio kadirika, na
tukaweka milima iliyo thibiti imara mirefu, na tukakunywesheni maji matamu?
Wataangamia siku hiyo hao wanao kadhibisha neema hizi!
29,30,31. Siku ya kupambanua wataambiwa makafiri: Nendeni huko Motoni
mliko kuwa mkikukanusha. Nendeni kwenye joto la moshi wa Jahannamu ulio
gawika kwa ukubwa wake mapande matatu. Hapana cha kujikinga na joto la
siku hiyo, wala kivuli hicho hakipunguzi joto la mwako hata kidogo.
32,33,34. Moto huo hutupa macheche yenye ukubwa kama majumba, au
utaona hayo macheche kama ngamia weusi wenye kuingia rangi ya manjano.
Wataangamia siku hiyo wanao kanusha kwamba hizi ndizo sifa za Moto.
35,36,37. Haya uliyo simuliwa yatatokea katika siku ambayo hawatatamka
kitu cha kuwanufaisha, wala hawatakuwa na idhini ya kutamka, wala hawatatoa
udhuru, kwani hawana udhuru. Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha siku
hii.
38,39,40. Hii ndiyo siku ya kufafanua baina ya mwenye ukweli, na
mwenye uwongo, kwa kuwa kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa anavyo
stahiki. Enyi mnao mkadhibisha Muhammad! Tumekujaalieni nyinyi na walio
kutangulieni walio kadhibisha mfano wenu, kama mnayo hila ya kujikinga
na adhabu basi fanyeni hila hiyo. Basi njooni muepukane na adhabu yangu.
Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha ahadi ya Mwenyezi Mungu.
41,42,43,44,45. Hakika wachamngu wenye kujikinga na adhabu ya Mwenyezi
Mungu watakuwa katika kivuli kikubwa, na chemchem zinazo miminika, na matunda
wanayo yaonea ladha, na wanayo yapenda, wataambiwa kwa kuamkiwa na kukirimiwa:
Kuleni na mnywe chakula na vinywaji kwa starehe kwa sababu ya vitendo vyema
mlivyo kuwa mkivitenda duniani. Hakika Sisi huwalipa mfano wa malipo hayo
matukufu watu wema. Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha Pepo.
46,47. Na makafiri wataambiwa: Kuleni na mjistareheshe kwa starehe
isiyo baki muda mrefu, kwani hakika nyinyi ni wakosefu kwa kumshirikisha
kwenu Mwenyezi Mungu. Wataangamia siku hiyo wanao ikadhibisha neema.
48,49. Na wakiambiwa: Salini kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na mnyenyekeeni
Yeye, hawanyenyekei wala hawasali; bali hushikilia kiburi chao! Wataangamia
siku wanao kadhibisha amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake.
50. Basi maneno gani hawa watayaamini ikiwa hawaiamini Qur'ani, na hali hii ni muujiza ulio toka mbinguni?