1. Hakika kimempitia mwanaadamu kipindi cha zama kabla
hajapuliziwa roho, naye hata bado hakuwa ni kitu cha kutajika kwa jina
lake, wala hajuulikani nini atakuwa.
2. Hakika Sisi tumemuumba mwanaadamu naye ana sifa namna mbali
mbali, kwa ajili ya kumtia mtihanini, majaribioni, baadaye. Kwa hivyo tukamjaalia
awe anasikia na anaona, ili apate kuzisikia Aya na azione Ishara.
3. Hakika Sisi tumembainishia Njia ya Uwongofu, ama awe Muumini au
awe kafiri.
4. Hakika Sisi tumewawekea tayari makafiri minyororo kuwafungia miguu
yao, pingu za kuwafungia mikono na shingo, na moto unao waka.
5,6. Hakika walio kuwa wakweli katika Imani yao watakunywa mvinyo
iliyo changanywa na maji ya kafuri. Hiyo ni chemchem wanayo inywa waja
wa Mwenyezi Mungu, na wanaipitisha watakapo kwa sahala.
7. Wanatekeleza yaliyo wajibikia , na wanaikhofu Siku
kubwa hiyo ambayo madhara yake yataenea kote kote,
8. Na huwalisha chakula mafakiri wasio weza kazi, na watoto walio
fiwa na wazee wao, na wafungwa wasio miliki kitu, ijapo kuwa wao wenyewe
hao watoaji wanakipenda hicho wanacho kitoa, na wanakihitajia.
9. Na hujiambia nafsi zao: Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya
kutaka thawa;bu za Mwenyezi Mungu. Sisi hatutaki kwenu malipo
au zawadi, wala hatutaki kushukuriwa na kusifiwa.
10. Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku ya kumletea
msiba atakaye kuwapo siku hiyo, na siku ya watu kukunja nyuso zao na vipaji
vyao.
11,12. Basi Mwenyezi Mungu akawalinda na shida za siku hiyo, na
badala ya mkunjo wa wenye maasi, akawapa nyuso za kupendeza, na ukunjufu
na furaha katika nyoyo zao, na akawajazi kwa ile subira yao Pepo imeenea
furaha, na nguo zake ni hariri laini.
13. Wakiegemea huko Peponi juu ya makochi, hawaoni joto la jua, wala
shida ya baridi.
14. Na Pepo ambayo vivuli vya miti yake vimeenea kote kote, na matunda
yake mepesi kuyachuma.
15,16. Na wakiwazungukia watumishi wao kwa bilauri za kunywea zilio
fanywa kwa fedha, lakini unaona kiliomo ndani kama kwamba ni kigae, na
vinapimwa vinywaji kwa kadiri wanavyo penda wanywaji.
17,18. Na watu wema hupewa kunywa huko Peponi mvinyo inayo fanana
na sharubati ya tangawizi kwa utamu. Hiyo ni kutokana na chemchem ya Peponi
inayo itwa Salsabil, kwa sababu ya wepesi wa unywaji wake na uzuri wake.
19. Na watakuwa wanawazunguka vijana ambao hawabadiliki hali yao,
kwa furaha na sururi. Ukiwaona wanapo zunguka kwa wepesi na uchangamfu,
utawadhania kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao, kama lulu zilizo tandazwa
mbele yako zinang'ara.
20. Na ukitazama popote katika hiyo Pepo utaona neema kubwa, na ufalme
ulio tanda.
21. Juu yao zipo nguo za hariri nyepesi za kijani, na nguo za hariri
nzito. Na mapambo yao yaliomo mikononi mwao ni vikuku vya fedha.
Na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji kingine kilio safi, hakina uchafu
wala najisi.
22. Hakika neema hizi ameziandaa kwa kukulipeni kwa vitendo vyenu.
Na hizo juhudi zenu duniani ni zenye kusifika kwa Mwenyezi Mungu, na zinampendeza,
na zimekubaliwa.
23. Hakika Sisi, kwa rehema yetu na hikima yetu, tumekuteremshia
wewe Qur'ani kwa njia ya kukutuza moyo wako, na uweze daima kuihifadhi,
basi huto isahau kabisa.
24. Basi subiri, uivumilie hikima ya Mola wako Mlezi kwa kuakhirisha
kushinda kwako kuwashinda maadui zako, na wewe ukapata mitihani kwa maudhi
yao. Wala usiwat'ii washirikina, wingi wa madhambi, walio zama katika ukafiri.
25,26. Na dumisha kumkumbuka na kumtaja Mola wako Mlezi, na sali
alfajiri mapema, na adhuhuri, na alasiri jioni, na usiku sali magharibi
na isha. Na fanya ibada za usiku kwa muda mrefu.
27. Hakika hawa makafiri wanaipenda dunia, na wanaifadhilisha kuliko
Akhera. Na wanaiacha migongoni mwao siku yenye misiba mikubwa, na vitisho
vikali. Wala wao hawajui nini cha kuwaokoa wao na hayo!
28. Sisi tumewaumba wao, na tumefanya kwa hikima kuumbwa kwao.
Na tukitaka tutawateketeza wao na tutawaleta mfano ya wao badala yao, ambao
hao watakuja kumt'ii Mwenyezi Mungu kinyume na wao.
29. Hakika Sura hii ni mawaidha kwa walimwengu wote. Basi mwenye
kutaka atafuata njia ya Imani na uchamngu kwendea kwa Mola wake Mlezi imfikishe
kwenye maghfira yake na Pepo yake.
30. Wala nyinyi hamwezi kutaka kitu chochote ila wakati anapo taka
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zenu, Mwenye
hikima kwa anayo yataka na akayakhiari.
31. Humuingiza amtakaye katika Pepo yake. Basi kuingia Peponi ni kwa fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu. Naye amewadhalilisha wenye kudhulumu, amewatengenezea adhabu iliyo chungu.