1,2,3. Ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi kwa Siku
ya Kiyama, na hiyo ni kweli iliyo thibiti; na ninaapa na natilia mkazo
kiapo hichi kwa nafsi inayo mlaumu mtu kwa dhambi zake na upungufu wake,
ya kwamba bila ya shaka yoyote mtafufuliwa baada ya kukusanywa mafupa yenu
yaliyo tawanyika. Hivyo mtu anadhani baada ya kuwa Sisi tulimuumba naye
hakuwa kitu chochote, tutakuja shindwa kuyakusanya mafupa yake yaliyooza
na yakatapanyika?
4. Hasha! Sisi tuna uweza wa kuviweka sawa hata vifupa vya vidole
vyake vilivyo vurugika, wachilia mbali mafupa yake makubwa makubwa ya mwili
wake.
5. Hivyo mtu anakanya kufufuliwa? Anataka abakie katika uasi
wake katika siku zote zilizo mbakilia katika umri wake ulio salia?
6. Anauliza kwa kuona haiwezi kutokea saa ya Kiyama: Lini itakuwa
hiyo Siku ya Kiyama?
7,8,9,10. Jicho litapo tahayari kwa kufazaika na kushtuka, na mwangaza
wa mwezi ukapotea, na jua likakusanyika na mwezi kuchomoza magharibi, mtu
hapo atasema: Yako wapi makimbilio kuikimbia hii adhabu?
11,12. Huachi, ewe mtu, kutafuta makimbilio? Leo huna pa kukimbilia
wewe, ila kwa Mola wako Mlezi peke yake, ndipo penye matulivu ya waja,
Peponi au Motoni.
13. Siku hiyo mtu ataambiwa vitendo vyake alivyo vitanguliza na alivyo
viakhirisha.
14,15. Bali mtu yeye mwenyewe ni hoja iliyo wazi juu ya nafsi yake
inayo mkazania kwa anayo yatenda na anayo yaacha. Na ijapo kuwa atajitolea
chungu nzima ya udhuru na akazieneza, hawezi kabisa kuepukana na hoja hizo.
16,17. Usiuharikishe ulimi wako kwa kuisoma Qur'ani na kujaribu kuihifadhi
kwa haraka pale unapo teremshiwa kwa Wahyi. Hakika ni juu yetu Sisi kuikusanya
hiyo katika kifua chako, na kuithibitisha katika ulimi wako.
18,19. Akikusomea Mjumbe wetu (Jibril) basi nawe ifuatilize kama
unavyo isikia. Kisha baada ya hayo ni juu yetu kuibainisha ikiingia tatizo
lolote juu yako.
20,21. Wacheni kukanya kufufuliwa, na hilo ni jambo la kweli. Lakini
nyinyi mnaipenda dunia na starehe zake, na mnaiacha Akhera na neema zake.
22,23. Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye kumwangalia Mola wao
Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa gani.
24,25. Na nyuso nyengine zitakuwapo zimenuna, zimekunjana mno, zinangojea
zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja uti wa mgongo.
26,27,28,29,30. Mna nini na kuipenda dunia ambayo mnaifariki roho
inapo fika katika mafupa ya kooni, na walio hudhuria wakasema: Yupo wa
kumganga huyu kwa haya aliyo nayo? Akayakinisha yule yaliyo mfika mauti
kama lililo mshukia ni kuiacha dunia inayo pendwa, na imekwisha mfika shida
yake kikomo cha mwisho. Na muundi wa mguu umekwisha ambatana na wa pili
wakati wa kutoka roho. Kwa Mola wako Mlezi tu siku hiyo ndio machungio
ya waja, ama Peponi au Motoni.
31,32,33. Binaadamu amekanya kufufuliwa, na kwa hivyo hakumsadiki
Mtume wala Qur'ani. Wala hakumtimizia Mwenyezi Mungu faridha za Sala. Lakini
aliikadhibisha Qur'ani, akaipuuza Imani, na akatoka kwenda kwa watu wake
wa nyumbani kwa maringo na kujitapa.
34,35. Ewe unaye kadhibisha, utaangamia! Tena utaangamia! Na tena
utaangamia, na utaangamia!
36. Hivyo anadhani huyu mtu anaye kanya kufufuliwa kuwa ataachwa
hivi hivi akiringa tu katika maisha yake, na akisha kufa iwe basi, wala
asifufuliwe akahisabiwa kwa vitendo vyake?
37,38. Kwani yeye mtu hakuwa ni tone tu ya manii, ilio jaaliwa kuwemo
katika tumbo la uzazi? Kisha hiyo tone ikawa kipande cha damu iliyo ganda,
na Mwenyezi Mungu akaiumba, akaisawazisha mpaka ikawa na umbo zuri?
39. Akajaalia namna mbili, mwanamume na mwanamke?
40. Je! Huyo Muumba wa mwanzo aliye fanya yote haya, basi si muweza wa kuwahuisha maiti baada ya kuyakusanya mafupa yao?