1,2,3,4. Ewe uliye jigubika kwa maguo! Inuka hapo kitandani,
na uwahadharishe watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa hawaamini. Na
mkusudie Mola wako Mlezi makhsusi kwa kumtukuza. Na safisha nguo zako kwa
maji kuzitoa najisi.
5,6,7. Na iache adhabu, yaani kuwa daima mwenye kujitenga na yanayo
pelekea kupata adhabu. Wala usimpe mtu yeyote kwa kutumai kupata zaidi
kwake katika kile unacho mpa; na kwa ajili ya kumridhi Mola wako
Mlezi subiri na stahamili juu ya maamrisho na makatazo, na kila jambo la
juhudi na mashaka.
8,9,10. Na litakapo pulizwa barugumu, huo ndio wakati wa siku ya
shida kwa makafiri, wala si wepesi kwao kujitoa na majadiliano ya hisabu,
na vitisho vyenginevyo.
11,12,13,14,15. Niache peke yangu na huyo niliye muumba. Kwani hakika
Mimi ninatosha kukukifia mambo yake. Nimemjaalia mali yaliyo kunjuliwa
yaliyo enea, yasio tindikia, na wana wanao tokea hadharani naye, na nikamkunjulia
cheo na ukubwa kwa ukunjufu ulio timia. Kisha tena anatumai nimzidishie
mali na wana na cheo bila ya shukrani yoyote!
16,17. Kuivunja hiyo tamaa yake, tunasema kwamba kwa kuwa yeye
alikuwa akiikaadhibisha Qur'ani kwa inda, tutamgubika kwa adhabu yenye
mashaka, wala hataweza kuikwepa.
18,19,20. Hakika yeye amejifikiria nafsi yake, na akajitengenezea
ya kuyasema ya kuitia ila Qur'ani, basi kwa hivyo amestahiki kuangamia
huko. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo! Kisha akastahiki maangamizo
hayo. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo!
21,22,23,24. Kisha akaziangalia nyuso za watu. Kisha akakunja uso
wake, na akazidi kuukunja, kisha akaipa mgongo haki na akajivuna kuwa ati
haitambui, na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa kutokana
na watu wa kale.
25. Maneno haya si chochote ila ni maneno ya viumbe aliyo jifundisha
Muhammad, na akadai kuwa ati yametoka kwa Mwenyezi Mungu.
26,27,28,29,30. Nitamtia Motoni aungue humo. Na nini kitakujuvya
hiyo Jahannamu ni nini? Haibakishi nyama wala haisazi fupa ila italiunguza
tu, ngozi ibabuke iwe nyeusi. Juu yake wako kumi na tisa wanao angalia
kazi yake, na kuwaadhibu waliomo.
31. Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, na wala hatukuifanya
idadi yao ya kumi na tisa ila kuwapa mtihani walio kufuru wapate yakini
walio pewa Kitabu (yaani Biblia, Mayahudi na Wakristo) kwamba inayo sema
Qur'ani juu ya walinzi wa Motoni ni kweli tupu itokayo kwa Mwenyezi Mungu
Mtukufu, kwa kuwa hayo yanakubaliana na vinavyo sema vitabu vyao; na ili
walio muamini Muhammad ipate kuzidi Imani yao. Na wala wasiyatilie
shaka hayo walio pewa Kitabu na Waumini. Na wenye maradhi ya unaafiki katika
nyoyo zao na makafiri waseme: Mwenyezi Mungu anataka nini kwa idadi hii
ya ajabu? Kwa mfano kama huu ulio tajwa, wa kupoteza na kuongoa, ndio Mwenyezi
Mungu huwapoteza makafiri na huwaongoa Waumini. Na hapana anaye wajua askari
wa Mola wako Mlezi, jinsi walivyo kuwa wengi mno, ila Yeye Subhanahu wa
Taala. Na huo Moto si chochote ila ni kumbusho na kitisho kwa binaadamu.
32,33,34,35,36. Kuzidi kumhadharisha anaye onywa naye asiogope, ninaapa
kwa mwezi na usiku unapo ondoka, na kwa asubuhi inapo angaza na kuchomoza,
kwamba huu Moto ni moja katika vitisho vikubwa kabisa vya kuonya na kukhofisha.
37. Ni onyo kwa binaadamu kwa atakaye kuja mbele katika nyinyi kutenda
kheri, au kubaki nyuma asitende.
38,39. Kila nafsi itashikwa kwa iliyo yatenda, ila Waislamu walio
zigomboa shingo zao kwa ut'iifu.
40,41,42. Hao watakuwa katika Mabustani ya Peponi, ambayo hayawezekani
kusifika. Wataulizana wao kwa wao khabari za wakosefu, wakiuliza hali zao
nini kilicho watia Motoni?
43,44,45,46,47. Waseme: Hatukuwa miongoni mwa wenye kusali kama wasalivyo
Waislamu. Wala hatukuwa tukiwalisha masikini kama Waislamu walivyo kuwa
wakilisha. Na tulikuwa tukijisoza na kuzama katika upotovu na mazungumzo
ya uwongo pamoja na hao walio kuwa wakiporojoka. Na tulikuwa tukiikadhibisha
Siku ya Hisabu, mpaka ikatujia yakini, yaani mauti.
48. Basi hao hakuto waokoa kuombewa msamaha na waombezi, wakiwa ni
Malaika, au Manabii, au watu wema.
49. Basi wana nini hata wanajitenga na mawaidha ya Qur'ani?
50,51. Hao hakika wamekuwa kama punda wanao toka mbio kumkimbia
anaye wafukuza.
52. Bali kila mmoja wao anataka apewe ukurasa unao toka mbinguni
uwazi ulio funguliwa unao thibitisha ukweli wa Mtume s.a.w. (yaani kama
shahada ya Ujumbe wake kwao!)
53. Juu ya kuzidi kuwaonya kwa hayo wayatakayo bali hawaikhofu Akhera,
na wakapuuza mawaidha, na wakavumbua mbinu mbali mbali za kutaka miujiza
na Ishara.
56. Na wala hawatakumbuka ila Mwenyezi Mungu atake Mwenyewe, kwani Yeye ndiye anaye stahiki kuogopwa, na Yeye ndiye wa kumsamehe mwenye kumcha.