1,2. Ewe Muhammad! Waambie watu wako: Nimepata wahyi
kwamba kikundi cha majini kimesikia kusoma kwangu Qur'ani, nao wakawaambia
wenzao: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya namna ya peke yake, hatujapata
kusikia mfano wake kabla yake, inaitia kwenye uwongofu na usawa. Kwa hivyo
tumeiamini hiyo Qur'ani tuliyo isikia; na kabisa hatutamshirikisha Mola
wetu Mlezi aliye tuumba na kutulea na chochote katika waja wake.
3. Na kwamba hakika cheo na utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka;
hana mke wala mwana.
4. Na hakika wajinga katika sisi walikuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu
maneno yaliyo kuwa mbali kabisa na ukweli na kuwa sawa.
5. Na hakika sisi tulikuwa tunadhani kuwa haiwi binaadamu au jini
kumzulia Mwenyezi Mungu jambo ambalo si laiki naye kusifika nalo.
6. Na walikuwako wanaume katika wanaadamu wakitafuta ulinzi kwa wanaume
wa kijini. Basi hao binaadamu hawakuwazidishia majini ila kuzidi uasi na
ujinga na ujeuri.
7. Na hakika majini walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, enyi binaadamu,
kwamba Mwenyezi Mungu hatamfufua yeyote baada ya kwisha kufa, wala hatowaletea
watu Mtume yeyote wa kibinaadamu.
8. Na hakika sisi tulitaka kufikilia mbinguni, tukakuta kumejaa walinzi
wa kimalaika wenye nguvu, na vimondo vinavyo unguza kutoka upande huo.
9. Na sisi kabla ya leo tulikuwa tukikaa pande za mbinguni kwenye
makao kwa ajili ya kuchunguza khabari za mbinguni. Lakini sasa mwenye kutaka
kusikiliza anakuta vimondo vinamngojea kumzuia na kumteketeza.
10. Na hakika sisi hatujui imekusudiwa adhabu kwa walioko katika
ardhi kwa huku kulindwa mbingu hata ikazuiliwa kusikilizwa, au Mola wao
Mlezi anawatakia kheri na uwongofu?
11. Na hakika miongoni mwetu wapo walio wema wachamngu, na miongoni
mwetu pia wapo walio kinyume na hivyo. Na hao ni walio wastani katika wema
wao. Kwa hivyo sisi ni wa makundi mbali mbali.
12. Na hakika sisi tumeyakinika kwamba hatutamshinda Mwenyezi Mungu
popote tutapo kuwapo katika ardhi, wala hatutamshinda hata tukifanya tuikimbie
hukumu yake kwendea mbinguni.
13. Na hakika sisi tulipo isikia Qur'ani tuliiamini. Na mwenye kumuamini
Mola wake Mlezi basi hachelei kupunguziwa chochote katika mema yake, wala
kudhulumiwa kwa kuzidishiwa maovu yake.
14. Na hakika kati yetu wapo Waislamu wenye kuikubali Haki, na miongoni
mwetu wapo wenye kuiacha njia ya uwongofu. Basi wenye kusilimu hao wameifuata
njia ya Haki, na ni wenye kufanya jitihada katika kuikhiari njia hiyo.
15. Ama majeuri walio iacha njia ya Uislamu basi hao watakuwa ndio
kuni za Jahannamu.
16. Na hakika lau kuwa watu na majini wakifuata Njia ya Uislamu,
wala wasende upogo wakaiwacha, basi bila ya shaka tutawanywesha maji mengi
yatakayo enea nyakati za haja.
17. Ili tuwajaribu tuwaone vipi watavyo mshukuru Mwenyezi Mungu kwa
neema anazo waneemesha. Na mwenye kukengeuka na ibada ya Mola wake Mlezi
atamtia katika adhabu ya mashaka asiyo yaweza kuyachukua.
18. Na imefunuliwa kwangu kwamba kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi
Mungu peke yake. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
19. Na imefunuliwa kwangu kwamba alipo simama Mja wa Mwenyezi Mungu,
Muhammad, katika Sala yake akimuabudu Mwenyezi Mungu, majini walijikusanya
makundi kwa makundi, wakistaajabu kwa waliyo kuwa wakiyaona na wakiyasikia.
20. Sema: Hakika mimi namuabudu Mola wangu Mlezi peke yake, wala
simshirikishi na yeyote katika ibada.
21. Sema: Mimi sina uweza wowote juu yenu wa kukuondoleeni madhara,
wala kukuleteeni uwongofu na manufaa.
22. Sema: Hakika mimi hapana yeyote awezae kuniondolea adhabu nikimuasi
Mwenyezi Mungu. Wala sipati pa kukimbilia, kuikimbia adhabu yake.
23. Lakini niliwezalo ni kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu na Risala
zake alizo nituma nizifikishe. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, na akaipuuza Dini ya Mwenyezi Mungu, basi hakika mtu huyo atapata
Moto wa Jahannamu abakie humo milele.
24. Hata watakapo iona adhabu waliyo ahidiwaa, hapo basi watajua
wakati itapo shuka, nani mwenye msaidizi dhaifu asiye na nguvu, na yupi
mchache wa idadi. Ni wao au Waumini?
25. Sema: Enyi makafiri! Sijui ni karibu hiyo adhabu mliyo ahidiwa,
au Mola wangu Mlezi ataifanya iwe mbali?
26,27. Yeye ndiye Mjuzi wa ghaibu, yaliyo siri. Hapana mmoja katika
viumbe vyake anaye ijua siri yake, ila Mtume aliye mridhia kumjuvya baadhi
ya hiyo siri. Naye humwekea mbele ya huyo Mtume na nyuma yake Malaika wa
kumkinga na wasiwasi.
28. Ili Mwenyezi Mungu ayajue hayo yametokea kwa kuwafikiana na alivyo kadiria, ya kwamba Manabii hakika wamefikisha Risala za Mola wao Mlezi. Na kwa hakika Yeye kesha jua kwa kufananua yote waliyo nayo, na anajua idadi ya viumbe vyote. Hapana kitu kinacho mpotea Yeye.