1. Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake, na tukamwambia:
Waonye watu wako kabla haijawajia adhabu yenye machungu makali.
2,3,4. Nuh'u akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu,
nina risala kutoka kwa Mola wenu Mlezi kwa lugha mnayo ijua, ya kwamba
mumt'ii Mwenyezi Mungu, na mumnyenyekee katika kutimiza waajibu zote; na
mwogopeni Yeye kwa kuacha mnayo katazwa, na nit'iini mimi katika ninayo
kunasihini. Ndipo Mwenyezi Mungu atapo kusameheni madhambi yenu, na atakupeni
umri mrefu mpaka ifike ajali iliyo wekwa mwisho wa umri wenu. Hakika mauti
yakija hayaakhirishwi kabisa! Lau kuwa mngeli jua majuto mtakayo kuwa nayo
utapo kwisha muda wenu mngeli amini.
5,6. Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu
wangu waamini usiku na mchana bila ya kuchoka, hawakuzidishwa na wito wangu
ila kuukimbia ut'iifu wako.
7. Na mimi kila nikiwataka wakuamini Wewe upate kuwasamehe, hubandika
vidole vyao kwenye masikio yao ili wasisikie wito wangu, na hujifunika
kwa maguo yao ili wasiuone uso wangu! Na wakasimama kidete juu ya ukafiri
wao, na wakatakabari kutakabari kukubwa mno!
8,9. Kisha nikawaita waje kwako kwa sauti ya juu, kisha nikaudhihirisha
wito kwa namna moja, na nikawaita kisirisiri kwa namna nyengine, ili nijaribu
kila njia.
10,11,12. Nikawambia watu wangu: Takeni kwa Mola wenu Mlezi maghfira
kwa kufru zenu na maasi yenu. Kwani Yeye bado ni Mwingi wa kusamehe madhambi
ya mwenye kurejea kwake. Atakuleteeni mawingu yatakayo miminika mvua kwa
wingi, na atakupeni mali na wana, na hayo ndiyo mapambo ya dunia, na atakupeni
mashamba mtayo starehea kwa uzuri wake na matunda yake, na atakujaalieni
mito ya kunyweshea mazao yenu na mifugo yenu.
13,14. Mna nini nyinyi hata hamumtukuzi Mwenyezi Mungu kama anavyo
stahiki kutukuzwa, ili mtaraji akukirimuni kwa kukuokoeni na adhabu, na
hali Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa madaraja, tangu tone ya manii, kisha
pande la damu, kisha pande la nyama, kisha mafupa na nyama?
15,16. Kwani huoni vipi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba mbingu saba,
moja juu ya moja, na akaufanya mwezi katika mbingu hizo unatoa nuru, na
akalifanya jua ni taa ambayo kwayo watu wa duniani ndio wanaona kwa mwangaza
wake yote wanayo hitajia kuyaona?
17,18. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi,
akakuotesheni kama miema kwa njia ya ajabu, kisha baada ya kufa atakurejesheni
huko huko kwenye ardhi, na tena atakutoeni huko kwa hakika hapana hivi
wala hivi.
19,20. Na Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi iliyo kunjuliwa ili mpate
kwenda humo katika njia zenye wasaa.
21,22. Alisema Nuh'u: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikatalia
mimi niliyo waamrisha ya kuamini na kutaka msamaha, na wakawafuata madhaifu
miongoni mwao ambao mali yao na watoto wao hawawazidishii ila khasara tupu
katika Akhera. Na vitimbi vya hao wenye mali mengi, na wana wengi, kwa
wanyonge wanao wafuata ni vitimbi vilivyo fika ukomo kwa ukubwa.
23,24. Na wao wakiwaambia: Msiache kuiabudu miungu yenu, wala msimwache
Wadda, wala Suwaa' , wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. Na hawa walikuwa
miungu ya masanamu iliyo chongwa kwa sura ya wanyama namna mbali mbali.
Na miungu hii iliwapoteza watu wengi. Na wala huwazidishii wenye kuzidhulumu
nafsi zao kwa ukafiri na inda, ili kuzidi kubaidika na Haki.
25. Kwa sababu ya madhambi yao wakazamishwa kwa tofani, na baada
ya kuangamizwa kwao wakatiwa Motoni kwenye moto mkali wa kuwaka na kuteketeza,
na wala wasipate yeyote baada ya kumkosa Mwenyezi Mungu, wa kuwanusuru
na kuwakinga na adhabu!
26. Na Nuh'u akasema baada ya kukata tamaa nao watu wake: Mola wangu
Mlezi! Usimwache yeyote katika hao wanao kukataa Wewe akabaki akizunguka
juu ya ardhi!
27. Ewe Mola wangu Mlezi! Ukiwaacha hao bila ya kuwateketeza na kuwang'oa
watawatia waja wako katika upotovu, na wao hawatozaa ila wenye kupotoka
vile vile wakaiacha haki, na wakakithiri kukukanya na kukuasi.
28. Mola wangu Mlezi! Nisamehe mimi na wazazi wangu ambao ndio walio kuwa ni sababu ya kuzaliwa mimi, na kila mwenye kuingia nyumbani kwangu kwa kukuamini Wewe, na uwasamehe Waumini wote wanaume na wanawake. Na usiwazidishie makafiri ila kuwaangamiza.